Afrika na Ulaya: Ni Wakati wa Kuchua Hatua

Get monthly
e-newsletter

Afrika na Ulaya: Ni Wakati wa Kuchua Hatua

Tusipoteze fursa hii ya kurudisha upya uhusiano na uchumi wetu
Afrika Upya: 
16 February 2022

Wakati viongozi wa Afrika na Ulaya wakikutana katika mkutano muhimu wa Umoja wa Ulaya – Umoja wa Afrika jijini Brussels, waafrika bado wako njia katika panda kama wawe na hisia za kusubiri kwa matumaini au hofu ya uchovu.

Vera Songwe

Matumaini kwa sababu mkutano huo unahusu nafuu ya kifedha, ufadhili wa kutosha na endelevu kwa ajili ya urejesho ambao ndiyo hasa unahitajika. Hofu, kwa sababu mikutano mingi mno imefanyika na haijaleta matokeo katika miaka michache iliyopita, na ni viongozi wachache pekee kutoka kaskazini au kusini mwa Bahari ya Shamu wana uelewa wa changamoto kubwa zilizopo – na hata fursa kubwa zaidi – zilizo mbele yetu katika wakati huu wa kipekee kihistoria.

Baada ya miongo michache, idadi ya vijana wa Afrika itakuwa mara sita zaidi ya idadi ya vijana wa Ulaya. Ni ubunifu wa vijana wetu, mabadiliko na uwezo wa kutatua matatizo utakaowawezesha kutatua changamoto kadhaa ambazo zinaikumba Ulaya leo na kwa siku zijazo.

Je, tunawezaje kushirikiana ili kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuhimiza demokrasia?  Tunawezaje kushirikiana ili kuhakikisha mifumo ya afya inahakikisha afya salama kwa wananchi wote wa ukanda huu? Je, ni jinsi gani waafrika walio ughaibuni wanaweza kuwa muhimu katika kuleta mabadiliko Ulaya? Tunawezaje kuweka juhudi za pamoja kupambana na mizunguko haramu ya kifedha?

Wazungu na Waafrika wanakubaliana – duniani kote, tunahitaji wastani wa 2-3% zaidi pato la taifa kuwekezwa katika miundombinu endelevu ili kuzuia janga la hali ya hewa na kuwezesha ukuaji jumuishi unaotoa kazi kwa wengi. Kwa nchi za Afrika, hitaji la uwekezaji ni zaidi kiuwiano kwa sababu ufadhili kwa ajili ya urejesho wa hali ya awali haukuwepo, vijana wetu wana matarajio makubwa, na tunaanzia kwenye uwekezaji katika ngazi ya chini kabisa na mapato kiwango cha mapato ya mtaji.

Leo, kuna mgawanyiko hatari na unaobadilika katika viwango vyetu vya urejesho – viwango vya chanjo vinatugawanya, tofauti zilizopo katika ufikiaji wa misaada ya kifedha zinaongeza mapungufu ya urejesho; na hali inayoendelea sasa Marekani na Ulaya ambapo serikali inanunua dhamana kutoka kwa watu pamoja shinikizo la mfumuko wa bei vinahujumu uchumi wetu. Hali zote hizi zinaongeza ukosefu wa usawa duniani, na tayari tunashuhudia mgororo unaoendelea huku wananchi wakitaka viongozi wao kuwafanyia zaidi.

Mwitikio kwa mashinikizo haya lazima uwe tofauti katika mkutano wa Brussels. Tunahitaji matrilioni zaidi kuwekezwa katika hadithi mpya ya ukuaji wenye manufaa kwa wote, maono mapya na jumuishi ya ukuaji utakaoleta kazi nyingi. Mpango kazi wa Urejesho wa Mazingira wa Umoja wa Afrika pamoja na Eneo la Biashara Huru Barani Afrika unatoa maelekezo kuhusu urejesho huu na mpango wa kufanya mambo upya. Viongozi wa Afrika wakiwa Ethiopia mnamo Februari waliahidi kuendesha kwa kasi utekelezaji wa programu hizi. Mkutano wa Brussels unatoa nafasi ambapo Ulaya inaweza kushirikiana na Afrika kuharakisha utekelezaji wa ajenda hii ili kujenga Afrika inayofana.

Ifuatayo ni njia muhimu ya maamuzi kwa vitendo ambayo viongozi walio katika mkutano wa Brussels wanaweza kufuata ili kufanya mkutano huu kuwa na maana na wenye matokeo ambao utasaidia kuongeza kasi kwa hatua zaidi ya kimataifa na ushirikiano na Afrika.

Kwanza, Ulaya lazima ihakikishe kwamba uchumi wa Afrika unaweza kukidhi changamoto zake za kupatikana kwa pesa taslimu kwa kutimiza au kupitisha ofa ya China ya kutumia tena angalau asilimia 25 ya sarafu zao za SDR - SDR bilioni 162 kati ya SDR bilioni 650 zilizotolewa.  Hii ikiambatana na makubaliano ya Paris na mwito wa Rais Macron, dola bilioni 100 kati ya hizi zinafaa kutengewa Afrika, ikijumuisha nchi za uchumi wa kati zilizo hatarini.  Takribani nchi 7 za Ulaya na Uingereza zimeahidi kutumia tena SDR au kiasi sawa cha bajeti cha kima cha dola bilioni 15 kwa SDR. 

Kuna mengi yanahitajika, na mkutano wa Brussels unaweza kusaidia kuinua idadi ya ahadi hizi.  Asilimia 94 ya SDR za nchi zilizoendelea hazijatumiwa, huku Afrika ikitumia asilimia 52 ya SDR zake.  Nchini Senegal, SDR zimetumika kusaidia kujenga uwezo wa kutengeneza dawa za tiba.

SDR hizi zinaweza kutumika tena kwa maeneo kadhaa ya kimkakati: Mfuko wa Kupunguza Umaskini na Ukuaji wa IMF (PRGT), - ambapo nchi zilizo na mahitaji zinaweza kuzifikia; mfuko mpya wa ustahimilivu na uendelevu, kituo kipya cha ukwasi na uendelevu ili kusaidia kupunguza viwango vya riba kwa ajili ya miundombinu endelevu; Benki ya Maendeleo Afrika na Afreximbank.

Taasisi hizi za Afrika zinaongoza juhudi za ukuaji kimazingira na biashara ya kikanda na kuziimarisha kukuza uaminifu na usawa zaidi katika ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.

Pili, kuunda kundi kazi la pamoja na mawaziri wa Fedha wa Afrika kupitia na kurekebisha Muundo wa Kawaida wa Madeni na kurejesha DSSI.  Karibu mwaka mmoja baada ya kutangazwa na zaidi ya miaka miwili baada ya janga hili, nchi nyingi zinazohitaji mfumo laini wa deni hazina uwezo wa kufikia vifaa vikubwa vinavyofanya kazi kwa kasi.

Watoa mikopo kutoka Ulaya pia wanaweza kuwa wabunifu zaidi kuhusiana na deni kwa ajili ya hali za hewa zinazobadilika kwa kujumuisha chaguo hili kwenye Mfumo wa Deni wa Pamoja. Uzinduzi wa DSSI wenye kikomo cha muda na kuongeza ustahiki wake utakuwa ni hatua muhimu katika kusaidia nchi zenye uchumi wa chini na  za wastani zilizo hatarini.

Tatu, makubaliano ya kufanya kazi na nchi za Afrika kuhusu ajenda  za kuaminika, huru na haki ya mpito kuwasilishwa na COP ya Afrika nchini Misri. Nchi za Afrika zimetia saini kwa pamoja makubaliano ya Paris ya kuondoa uchafuzi wa hewa kufikia 2050.

Ili kufanya hili, Afrika inahitaji bei ya kaboni duniani iendane na malengo ya Paris, na mazungumzo ya ukweli zaidi kuhusu kuwezesha mkakati wa hasara na uharibifu - ili nchi zilizo katika hatari ya mabadiliko ya hali hewa ziweze kufidiwa kutokana na athari za sasa na za kihistoria za utoaji wa kaboni.

Umoja wa Ulaya pia unapaswa kuunga mkono mwito wa viongozi wa Afrika wa kupata asilimia 50 ya ufadhili kuhusu hali ya hewa ili kuwasaidia kupambana na mabadiliko na kuboresha mikopo au kutoa sehemu ya dhamana ili kuboresha kiwango cha utoaji wa dhamana za kudumisha mazingira ili kukabiliana na umaskini.  Isitoshe, ili kuhakikisha kwamba mataifa ya Afrika hayasakamwi na maendeleo yao, gesi ya kupikia na kiwango cha chini zaidi cha nishati inayohitajika lazima iwe ni sehemu inayofadhiliwa itakayowezesha mpito wa haki.

Nne, vita dhidi ya Uviko-19 inaendelea lakini leo watoto zaidi wa Afrika wanakufa kutokana na Malaria kwa hivyo mwitikio wa afya ni sharti uwe mpana. Ni lazima ulaya iongeze kifurushi cha uwekezaji cha uwezo wa kutengeza chanjo, ikubali kutoa Hakimiliki kwa watengenezaji wa chanjo kutoka Afrika, na kuongeza ufadhili wa mifumo ya afya ya Afrika. 

Ujerumani na Marekani zinakaribia kuandaa mikutano muhimu kuhusu usawa wa kupata chanjo na kupambana na tandavu ijayo, kwa hivyo mkutano huu wa Umoja wa Afrika-Umoja wa Ulaya unaashiria nia ya pamoja na ya dhati ya Ulaya kuhusu afya na usalama.  Ni sharti Ulaya na Afrika zisaidie utengenezaji wa mpango wa kujitayarisha kupambana na tandavu.

Mwisho, kuwekeza katika sekta halisi lazima kupewe kipaumbele. Ulaya na Afrika zinapaswa kujitolea kufanya ushirikiano wa kibiashara kwa kupitia AfCFTA na kutengeneza minyororo ya usambazaji bidhaa inayoongeza thamani, stahimilivu na endelevu. CFTA imetengeneza fursa kubwa ya uwekezaji. Kwa mfano, katika sekta ya uchukuzi pekee zaidi ya dola bilioni 400 zinahitajika kuwekezwa ili kupata manufaa kamili ya CFTA.

Mipango ya pamoja ya Timu za Afrika na Ulaya katika nishati, uchukuzi na dijitali inaweza kusaidia kasi ya uwekezaji huu, kutengeneza nafasi za kazi, kuhamisha teknolojia na kuboresha maisha kwa wote hususan kwa vijana na SME.

Mpango uliotangazwa hivi karibuni wa mradi wa Lango la Kimataifa umekabirishwa. Kwa kuwa kufanya vitu kidijitali barani Afrika ni nguzo muhimu ya kuleta maendeleo, nchi za Afrika zinatazamia kuwa na usawa na uwezo wa kuifikia teknolojia bora duniani kwa ajili ya maazimio yao.

Serikali za Afrika nazo zinatakiwa kuendelea kuboresha mifumo yao ya utawala. Muhimu zaidi ni kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya mataifa yao, kukabiliana na mizunguko haramu ya fedha na kutoa nafasi kwa raia kwa ajili ya majadiliano jumuishi zaidi. Kuboresha mazingira ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki na hususan kuhimiza ukuzaji wa ujasiriamali miongoni mwa vijana kuhusu mikakati kama vile Compact with Africa kunaendelea kuwa muhimu.

Malengo yetu ya kimataifa, ajenda ya 2030 na Makubaliano ya Paris pamoja na maazimio yetu kama bara yaliyoakisiwa katika Ajenda ya 2063 yanatoa msingi mkubwa wa ushirikiano wa pamoja na wenye ufanisi. Mkutano wa Brussels ni mkutano wa kujenga imani baada miaka miwili yenye misukosuko ambapo mataifa yalianza kujijali badala ya kushirikiana.

Ulaya na Afrika hazipaswi kupoteza fursa ya urejesho na kuweka upya mahusiano yetu na uchumi wetu.


Bi. Songwe ni Afisa Chini ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika (UNECA).

More from this author