Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

UNICEF Kenya yaungana na wafanyakazi wa kujitolea kutokomeza Corona

Get monthly
e-newsletter

UNICEF Kenya yaungana na wafanyakazi wa kujitolea kutokomeza Corona

UN News
6 May 2020
By: 
Wafanyikazi katika makazi duni ya Kibera jijini Nairobi, Kenya wanachukua hatua za kujikinga na virusi vya Corona
UN-Habitat/Julius Mwelu
Wafanyikazi katika makazi duni ya Kibera jijini Nairobi, Kenya wanachukua hatua za kujikinga na virusi vya Corona

Nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na jamii ili kusaidia kuepusha kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 hususan kwenye maeneo ya makazi duni

Harakati hizo mathalani zinatekelezwa kwenye maeneo yasiyo rasmi ya Kibera nje kidogo ya mji mkuu, Nairobi ambako wahudumu wa kujitolea wa kijamii kama vile Violet Chemesunde wanafanya kazi kutwa kucha kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona.

Bi. Chemesunde mkazi wa kijiji cha Kichinjio eneo la Kibera jijini Nairobi anasema kuwa, “tangu mlipuko wa janga la Corona, nimekuwa naelimisha jamii  napita nyumba kwa nyumba, kuelimisha familia jinsi virusi vya Corona vinaambukizwa na kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga na kuelimisha familia jinsi ya kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni. Pia nawaelimisha jinsi ya kuepuka kuchangamana. Nimetaka kuwa mfanyakazi wa kujitolea wa kijamii ili kusaidia jamii kwenye masuala ya afya ya jamii.”

Hata hivyo mfanyakazi huyo wa kujitolea anataja baadhi ya changamoto anazokumbana nazo kuwa ni pamoja na kwamba baadhi ya familia huko Kibera ni hohehahe kiasi kwamba haziwezi kununua sabuni ya kunawia mikono na hazina maji tiririka.

Licha ya changamoto hizo, wakazi wa Kibera wananufaika na kazi inayofanywa na Bi. Chemesunde ambapo Bi. Joyce Mterengo mkazi wa eneo la Kichinjio anasema kuwa, “mfanyakazi wa kujitolea wa kijamii amenifundisha jinsi ya kunawa, na unaponawa si tu unahesabu muda unaonawa bali kila unapotoka na kurejea unanawa. Unapokohowa hakikisha mdomo umefunika vizuri, inafaa mpatiane umbali kidogo, usiwe karibu na mwenzako. Na kama ni kuketi, wenyewe sisi tumezoea kuketi karibu karibu, lakini kwa sasa kwa hili janga inabidi tujipatie nafasi ndio tuepuke hii shida tuliyo nayo nchini kwetu.”

Wafanyakazi wa kujitolea wanaomba kuwepo kwa vituo zaidi vya kijamii vya kunawa mikono kwa sababu na maji tiririka kama njia ya kutokomeza Corona.

John Obisa ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano UNICEF nchini Kenya, yeye ana ombi maalum kwa wakazi wa Kenya akisema kuwa ni, “tunataka wewe ufanye yafuatayo, mosi , nawa mikono yako kwa sabuni na maji tiririka kwa angalau sekunde 20, pili, unapotoka nje, vaa barakoa, kwa sababu unapotumia barakoa unalinda uwapendao, iwapo tayari wewe umeshaambukizwa, ujumbe mwingine sote tuwe macho, kile kidogo unachoweza kufanya kujilinda wewe na kulinda wapendwa wako ili kukomesha Corona.”

Tayari Kenya ni miongoni mwa mataifa yenye maambukizi ambako tayari watu 490 wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huo huku wengine  24 wakifariki dunia.