Ni lazima kila juhudi ifanyike kumaliza ukiukwaji wa haki za binadamu Mali-Mtaalam

Get monthly
e-newsletter

Ni lazima kila juhudi ifanyike kumaliza ukiukwaji wa haki za binadamu Mali-Mtaalam

UN News
By: 
Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali. Picha: UN /Marco Dormino
Picha: UN /Marco Dormino Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali.
Picha: UN /Marco Dormino Kundi la maafisa polisi wa UN waliopo ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, wakizungumza na raia wakati wa doria mjini Menaka, kaskazini mwa Mali.

Hali ya haki za binadamu nchini Mali inatia wasiwasi wakati huu ambapo usalama na hali ya kibinadamu katika maeneno ya kati na kaskazini mwa nchi hiyo ikiendelea kudorora, amesema mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Mali, Alioune Tine.

Taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imenukuu ripoti ya mtaalam huyo kufuatia ziara yake nchini Mali, akisema kuwa hali ya ukatili ukilenga makabila tofauti pamoja na ukatili unaotekelezwa na makundi yaliyojihami, operesheni za kukabiliana na ugaidi zinazotekelezwa na vikosi vya Mali na vya kimataifa, uhalifu wa kupanga vyote vimezua hali ya hofu na kutokuwepo usalama.

Ameongeza kuwa katika eneo la Mopti, wanakijiji wengi wanaishi kwa maagizo na amri kutoka vikundi vya kijihadi, vinavyowazuia wanakijiji kuendesha shughuli zao za kila siku za biashara na kilimo na hivyo kusababisha kutokuwepo uhakika wa chakula na njaa.

Mtaalam huru huyo ameongeza kuwa, “ni lazima kila juhudi ifanyike kumaliza hali hii ambayo haikubaliki na mikakati ya serikali ya kukabiliana na hali ya sasa ni lazima iwezeshwe kwa ajili ya kupata majibu kwa hali iliopo sasa.

Bwana Tine amesema, “ukatili na ukiukaji wa haki za bindamu wa mara kwa mara ikiwemo madai ya mauaji kiholela, kutekwa, mateso, na kuzuiliwa kusio halali vinatekelezwa bila kuwajibishwa na maeneo ambayo hayakuwa yameathiriwa miezi michache iliyopita sasa yanakabiliwa na ukatili huo.”

Amesema ni lazima kwenda mbali zaidi na kuhakikisha kuwa uwajibishaji wa waleo wote walihusika katika ukiukaji wa haki za binadamu wanafikishwa mbele ya mahakama kama njia pekee ya Mali kutokomeza saratani ya uwajibishaji.

Halikadhalika, mtaalam huru huyo amekaribisha juhudi za serikali ya Mali za kupeleka vikosi vya ulinzi na usalama kufuatua mashambulizi ya kiaktili katika kijiji cha Koulogon Peul, na hatua ya Rais Ibrahim Boubacar Keïta na Waziri Mkuu Soumeylou Boubèye Maïga kuzuru eneo hilo kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na watu.

Wakati wa ziara yake, Bwana Tine ametembelea maeneo ya Bamako na Mopti ambako alikutana na Rais Keita na Waziri Mkuu na viongozi wengine kutoka serikalini, wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa na vikosi vya ulinzi na usalama. 

Aidha alizungumza na wawakilishi wa baadhi ya vikosi vya makundi yaliyojihami ikiwemo Plateforme, la Coordination des mouvements de l’Azawad na Mouvement pour le Salut de l’Azawad (MSA), pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kiraia, viongozi wa kidini na kiramaduni na kamisheni ya kitaifa ya haki za binadamu.

Mtaalam huru huyo atawasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za binadamu mjini Geneva, Uswisi, mwezi Machi mwaka huu wa 2019.