Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Ongezeko la kasi la ugonjwa wa kisukari Afrika lakoleza makali ya COVID-19

Get monthly
e-newsletter

Ongezeko la kasi la ugonjwa wa kisukari Afrika lakoleza makali ya COVID-19

Kukabili mlipuko wa kisukari katika Afrika ni muhimu kama kukabili COVID-19
World Health Organization
Afrika Upya: 
13 November 2021
Na: 
WHO
Kupambana na janga la kisukari barani Afrika ni muhimu kama vile vita dhidi ya COVID-19.

Ongezeko la kasi la ugonjwa wa kisukari katika Afrika linasadifiana na janga la COVID-19 na hali mbaya ya kupata chanjo.

Viwango vya vifo katika Afrika kutokana na maambukizi ya COVID-19 viko juu zaidi miongoni mwa wagonjwa wa kisukari, kulingana na uchanganuzi wa awali uliowasilishwa leo na Shirika la Afya Duniani (WHO) kabla ya Siku ya Kisukari Ulimwenguni tarehe 14 Novemba.

“COVID-19 inawasilisha ujumbe dhahiri: kukabili mlipuko wa kisukari katika Afrika ni muhimu kwa njia nyingi kama kukabili janga la sasa,” alisema Dkt. Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika. “Janga la COVID-19 litapungua hatimaye, ila Afrika inatabiriwa kushuhudia ongezeko la juu zaidi la kisukari kimataifa katika miaka ijayo. Ni lazima tuchukue hatua sasa kuzuia maambukizi mapya, kuwachanja watu walio na hali hii, na muhimu pia, kuwatambua na kuwasaidia mamilioni ya Waafrika wasiojua kwamba wanaugua maradhi haya yanayoua.”

Kisuakari kinalemaza uwezo wa mwili kuzalisha au kutoa insulini, dutu muhimu katika kukabiliana na ongezeko hatari la sukari ya damu. Maradhi haya yanasababisha mwako na hali mbaya ya kuzunguka kwa damu, ambayo huongeza hatari, ikiwa ni pamoja na vifo kutokana na COVID-19.

Uchanganuzi wa hivi majuzi wa WHO ulitathmini data kutoka mataifa 13 kuhusu hali changizi au hali ya mgonjwa kuugua maradhi zaidi ya moja miongoni mwa Waafrika walioambukizwa COVID-19. Ulibainisha asilimia 10.2 ya vifo miongoni mwa wagonjwa wa kisukari ikilinganishwa na asilimia 2.5 kwa wagonjwa wa COVID-19 kwa jumla.

Viwango vya vifo miongoni mwa wagonjwa wa kisukari vilikuwa maradufu pia kuliko miongoni mwa wagonjwa waliougua maradhi zaidi ya moja.  Mbali na wagonjwa wa kisukari, hali nyingine changizi maarufu zilihusisha wagonjwa walio na VVU na shinikizo la damu.

Mataifa yaliyochangia data ya uchanganuzi huo yalikuwa Burkina Faso, Chad, Cote d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Guinea, Namibia, Nijer, Rwanda, Senegali, Ushelisheli, Sao Tome na Principe na Uganda.

Takriban watu milioni 24 katika Afrika wana kisukari mwaka 2021, kulingana na Shirika la Kisukari Ulimwenguni (International Diabetes Federation).

Bara hili linatarajiwa kushuhudia ongezeko la juu zaidi la kisukari kimataifa, huku idadi ya Waafrika wanaougua ugonjwa huo ikitabiriwa kuongezeaka hadi milioni 55 kufikia 2045, ongezeko la asilimia 134 ikilinganishwa na 2021. Afrika ndio kanda yenye idadi kubwa zaidi ya watu wasiofahamu hali yao – takriban asilimia 70 ya wagonjwa wa kisukari hawajui kwamba wanaugua maradhi haya.

“Maafisa wa Afya katika Afrika wanastahili kutumia fursa ya ongezeko la kuwepo vipimo nafuu vya utambuzi kwa kasi kuwapima wagonjwa kila mara katika vituo vya kisukari ili kuhakikisha ugunduzi wa mapema na uangalizi,” alisema Dkt. Benido Impouma, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yanayoambukizwa na Yasiyoambukizwa katika Ofisi ya Kanda ya Afrika ya WHO “Vituo hivi pia vinaweza kuwa mahali muhimu pa kutolea chanjo.” 

Tangu siku za mwanzo kabisa za janga hili, wagonjwa wa kisukari katika mataifa ulimwenguni wamepewa kipaumbele kupata chanjo za COVID-19. Afrika imekabiliwa na changamoto katika mkakati huu.

  • Takriban watu milioni 24 wanaishi na kisukari katika Afrika mwaka 2021.
  • Afrika inatarajiwa kushuhudia ongezeko la juu zaidi kimataifa.
  • Idadi ya Waafrika wanaougua kisukari inatabiriwa kuongezeka hadi milioni 55 kufikia 2045, ongezeko la 134% ikilinganishwa na 2021.
  • Afrika ndio kanda yenye idadi kubwa zaidi ya watu wasiojua hali yao – takriban 70% wanaougua kisukari hawajui wana maradhi haya.
  • Uchanganuzi wa majuzi wa WHO ulitathmini data kutoka mataifa 13 kuhusu hali changizi au hali ya mgonjwa kuugua maradhi zaidi ya moja miongoni mwa Waafrika walioambukizwa COVID-19.
  • Mataifa yaliyochangia data kwa uchanganuzi huo yalikuwa Burkina Faso, Chad, Cote d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Guinea, Namibia, Niger, Rwanda, Senegal, Ushelisheli, Sao Tome and Principe pamoja na Uganda.
  • Uchanganuzi huo ulibainisha vifo vya 10.2% kwa wagonjwa wa kisukari, ikilinganishwa na 2.5% kwa wagonjwa wa COVID-19 kwa jumla.

Hali ya kufikia chanjo imekuwa mbaya. Kufikia sasa, ni asilimia 6.6 pekee ya watu wa Afrika waliochanjwa kikamilifu dhidi COVID-19, ikilinganishwa na takribani asilimia 40 kimataifa.

Data kutoka mataifa 37 inaonyesha kwamba tangu Machi 2021, zaidi ya dozi milioni 6.5 za COVID-19 zimewaendea Waafrika wanaougua maradhi zaid ya moja, wakilisho la asilimia 14 ya chanjo zote zilizotolewa kufika sasa.

Juhudi za kuwapa kipaumbile wagonjwa wanaougua maradhi zaidi ya moja, kama kisukari, zinashika kasi huku nusu ya hizo dozi milioni 6.5 zikitolewa katika miezi miwili iliyopita pekee. Hata hivyo, kazi kubwa bado inastahili kufanywa ili kuhakikisha kwamba watu walio katika hatari wanazipata chanjo wanazozihitali.

“Miezi tisa tangu kampeni za chanjo za COVID-19 zilipoanza kutolewa katika Afrika, bado tuko mbali sana na tunakostahili kuwa ili kuwalinda watu wetu walio katika hatari kuu,” Dkt. Moeti alisema. “Kuna haja ya dharura kuongeza kasi ya utoaji chanjo na huduma nyingine muhimu kwa watu walio katika hatari kuu, ikiwa ni pamoja na wanaougua kisukari.”

Kuna aina mbili kuu za kisukari:

Aina 1 — inasababishwa na hali fulani mapema maishani, hali inayoharibu kongosho na kuulemaza uzalishaji wa insulini. 

Aina 2 — inahusishwa na lishe mbovu, unene na ukosefu wa mazoezi — ambapo mwili unakazana kuzalisha insulini.

Takriban 90% ya visa vya kisukari ulimwenguni, na vingi mno katika Afrika, ni vya Aina 2, huku viwango vya ongezeko katika Afrika vikuhusishwa na lishe mbovu, na mtindo tuli wa maisha ukisababisha ongezeko la kisukari Aina 2 ulimwenguni kote.

Mbali na hatari za COVID-19, kisukari pia kinaweza kusababisha ongezeko la mshtuko wa moyo, kiharusi, maradhi ya kibofu, kukatwa miguu, ulemavu wa macho, upofu, na uharibifu wa neva pamoja na shida ya kusimika.

“Waafrika wote walio katika hatari ya kisukari wanastahili kupimwa,” Dkt. Moeti alisema. “Tunaweza pia kuzuia mauaji zaidi ya kisukari kwa kuendeleza lishe bora na nafuu, pamoja na mazoezi ya kila mara.”

Wakati wa janga la COVID-19, kupata huduma ya kisukari kumevurugwa zaidi katika kanda ya Afrika. Amri za kutotembea ili kupunguza maenezi ya COVID-19, kwa mfano, zimezuia kupata huduma za afya na vipengele vya kimsingi vya uangalizi wa ugonjwa kama vile uangalizi wa kawaida wa  viwango vya sukari na kupata lishe bora.  

Ili kuboresha uwezo sawa wa kupata huduma bora za kisukari, WHO ilizindua Mfumo wa Kimataifa wa Kukabili Kisukari (Global Diabetes Compact) mwezi Aprili 2021.  Hii ni nyongeza ya kazi zilizofanywa miaka ya hivi majuzi kuanzisha Furushi la Msaada Muhimu wa Magonjwa Yasiyoambukizwa la WHO (WHO PEN) kwa huduma msingi za afya katika mazingira ya raslimali chache.

Kufikia sasa, mataifa 21 ya Afrika yameanza kutumia furushi hili. Mataifa ya Benin, Eritrea, Eswatini, Lesotho na Togo yametimiza upanuzi wa kitaifa kufikia vituo vyote vya kimsingi vya afya.