Rais wa Bunge la Afrika atoa wito wa amani na umoja

Get monthly
e-newsletter

Rais wa Bunge la Afrika atoa wito wa amani na umoja

Tunataka Bunge la Afrika liwe Bunge la Wananchi
Afrika Upya: 
11 January 2024
Fortune Charumbira
Fortune Charumbira

Wakati Fortune Charumbira, chifu na seneta nchini Zimbabwe, alipochaguliwa kuwa Rais wa Bunge la Afrika zaidi ya mwaka mmoja uliopita, aliahidi kuangazia amani na umoja miongoni mwa nchi za Afrika. Katika mahojiano haya na Mkhululi Chimoio kwa manufaa ya Afrika Upya, Bw. Charumbira anajadili mafanikio yake kufikia sasa na mtazamo wake kuhusu vita vya Urusi na Ukraine. Haya ni madondoo kutoka kwa mahojiano hayo:

Ulichukua madaraka katika Bunge la Afrika huku kukiwa na mgawanyiko fulani kufuatia uchaguzi wako. Hali imekuwaje tangu wakati huo?

Awali ya yote, jukumu langu kama kiongozi lilikuwa kushughulikia migawanyiko hiyo. Unapochukua ofisi ya hadhi hiyo katika nafasi ya kidemokrasia, hata katika uchifu wa kurithi, wakati mwingine kuna mashindano. Inamwimarisha kiongozi. Hujenga tabia na kumfanya kiongozi kutulia haraka katika nafasi mpya ya uongozi.

Watu kutoka kanda zote wanafanya kazi nami. Nilimkumbatia kila mtu. Ninahakikisha haki katika ugavi wa nafasi kwa watu katika kanda mbalimbali katika kamati mbalimbali. Makamu wa rais sasa wanatoka katika kanda tofautitofauti. Kila mmoja wetu anatoka katika kanda zinazozungumza Kiarabu, Kifaransa na Kireno. Kama matokeo, kila mtu anajihisi kwenye bodi.

Sarakasi za uchaguzi zimekwisha, na sasa ni wakati wa kumkumbatia kila mtu na kufanya kazi pamoja.

Ulizungumza kuhusu kuunganisha Bunge la Afrika kwa ajili ya Afrika yenye maendeleo. Hilo linaendeleaje?

Kuunganisha Afrika ni jukumu letu sote, sio bunge hili pekee. Ujumbe wa Umoja wa Afrika umekuwepo kila wakati na umeenea katika kila mkutano wa AU, hata kabla ya kuundwa kwa Muungano wa Afrika [mtangulizi wa Umoja wa Afrika] mwaka wa 1963. Katika nafasi na taasisi zetu, sote tunafuatilia umoja kwa ajili ya Afrika. Ni jukumu takatifu.

Tunataka Bunge la Afrika liwe bunge la wananchi.

Niliposhika hatamu, niliamua kubadili jina la taasisi hii na kuachana na fikra za kikoloni ambazo zilitugawanya katika mstari wa kuwa ama Waanglofoni, Wafrankofoni au Walusofoni.

Ni lazima tuukumbatie umoja licha ya changamoto. Ni wajibu wetu usioepukika. 

Afrika inayumbayumba chini ya urekebishaji mpya sasa wa kisiasa na kijiografia. Je, urekebishaji huu umeiathiri vipi kazi yako?

Ni kweli. Fikiria masuala yanayotokana na vita vya Russia na Ukraine, kwa mfano.

Mnamo Desemba 2022, wabunge 17 wa Bunge la Afrika walisafiri hadi Bunge la Ulaya. Tulifanya majadiliano kuhusu masuala mengi. Bunge la Ulaya lilikuwa limeandaa taarifa kuhusu vita vya Urusi na Ukraine. Tulipoombwa kuitia sahihi, tulisema, “Hapana, Afrika si sehemu ya vita hivyo.”

Tulikuwa wazi kama Bunge la Afrika nzima: dhamira yetu ilikuwa kuhubiri amani. Jukumu letu halikuwa kuchagua upande mmoja; lilikuwa ni kuhimiza Urusi na Ukraine kuitafuta amani.

Kutoka kwa Vita Baridi kuliibuka Vuguvugu Lisiloegemea Upande Wowote kwa sababu viongozi wa Afrika walitambua kwamba kuegemea upande hakungesaidia Afrika. Hatutaingizwa kwenye migogoro ya kisiasa na kijiografia.

Kuhusu Bunge la Afrika
  • Bunge la Afrika (PAP) ni chombo cha kutunga sheria cha Umoja wa Afrika chenye mataifa 55 wanachama
  • Lina wabunge 275 kwa jumla - watano kwa kila taifa mwanachama wa AU - ambao wamechaguliwa au kuteuliwa na mabunge yao ya kitaifa.
  • Lilianzishwa Machi 2004
  • Linafanya vikao vyake Midrand, Afrika Kusini
  • Linaongozwa na ofisi ambayo inajumuisha Rais na Makamu wanne wa Rais wanaowakilisha kanda tano za bara hilo.
  • Linalenga kuwa taasisi yenye mamlaka kamili ya kutunga sheria na wanachama waliochaguliwa kupitia upigaji kura wa watu wazima.
  • Linawajibikia ajenda, sera na malengo ya AU kwa kujadili, kuchunguza na kutoa maoni kuhusu masuala yanayohusu haki za binadamu, utamaduni wa demokrasia, kukuza utawala bora na utawala wa sheria.

Je, unadhani Bunge la Afrika na Afrika kwa ujumla linapaswa kutumia vipi ubora wake kwa nchi za Magharibi na Mashariki, zikiwaniaa sehemu ya bara hili?

Hakuna bara linaloweza kutuunga mkono bila kutarajia kufaidika kutoka kwetu. Wakati Marekani imekuwa ikitoa wito wa ushirikiano, Ulaya ulitangulia, wakati China ilikuja baadaye kwa mtindo wake, ukarabati na ujenzi wa miundomsingi.

Changamoto halisi si Uchina wala Marekani. Hakuna hata mmoja wao anayewajibika katika kuzipanua chumi zetu. Wengine wanaweza kufanya uchimbaji madini hapa na pale — ila kwa manufaa yao wenyewe — wanaporudisha pesa zao badala ya kuziwekeza tena ili kuzipanua chumi zetu au kutengeneza ajira. 

Kuwategemea wafadhili wa nje kuendeleza chumi zetu hakuhalisi. Hatimaye, tunahitaji uhamasishaji wa kifedha wa ndani ya Afrika.

Zimbabwe sasa inajulikana kwa kaulimbiu yake, “Nyika inovakwa nevene vayo,” ambayo ni Kishona yenye maana “Ni raia wa nchi pekee wanaoweza kuendeleza nchi yao wenyewe.”

Hatutaingizwa kwenye mapigano ya kisiasa na kijiografia ambayo hayasaidii Afrika kwa vyovyote.

Je, unafikiri uchaguzi wa hivi majuzi nchini Kenya, Lesotho na Naijeria utaathiri vipi kazi ya Bunge la Afrika na azma ya kuwa na Afrika yenye maendeleo?

Wapiga kura katika nchi hizi walizitekeleza haki zao za kidemokrasia, ingawa kulikuwa na mashindano. Wale wanaoshinda wanapaswa kuwakumbatia wale wanaoshindwa.

Kilichoiangamiza Afrika siku za nyuma ni mtazamo huu wa mshindi kuchukua kila kitu. Labda ulikuwa mzuri chini ya utawala wa chama kimoja lakini si katika demokrasia ya Afrika.

Pia, Waafrika wamekomaa kisiasa, na wanajua kuwa kuhakiki chama tawala ni kuzuri, ili kitekeleze ahadi zake kwa wananchi.

Upinzani unaweza kuleta mchango muhimu. Huo ni ukweli.

Kwa Bunge la Afrika, somo hapa ni, “Msitupilie mbali upinzani; ukumbatieni.”  

Kwa upande mwingine, sio lazima upinzani upinge kwa ajili ya kufikiri tofauti tu bali ufanye hivyo ili kuongeza thamani ya utawala bora.

Wajibu wetu katika Bunge la Afrika ni kuhakikisha kuwa kuna upinzani unaowajibika na mshindi asitie chuku ushindi.

Kutegemea wafadhili wa nje au ufadhili hakuleti ukuaji kamili wa kiuchumi.

Je, unaweza kusema ni yapi baadhi ya mafanikio makuu ya Bunge la Afrika chini ya uongozi wako?

Tumeyatimiza mengi.

 

Wajibu wetu ni kutoa majukwaa ya mijadala. Kwa hali hiyo, tumewaalika wadau kadhaa, vikiwemo vyombo vya habari, kujadili demokrasia barani humo.

Tumefanya mengi katika sekta ya afya pia.

Tumependekeza zaidi ya sheria kielelezo 10 katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kilimo na uhamiaji - kuhusu masuala muhimu sana ya visa, polisi na ushirikiano. Tunapendekeza sheria kwa sababu, kwa sasa, hatuna mamlaka ya kutunga sheria. Tunashauri kupitia sheria kielelezo kwa kusema: "Ikiwa unataka kuitawala kanda fulani vyema, basi hizi ndizo sheria."

Kila mwaka tunaandaa Kongamano la Kila Mwaka la Wanawake, jukwaa la wanawake katika bara hilo kuyazungumzia masuala yanayowaathiri.

Tumeyaandaa makongamano ya kila mwaka kama hayo kwa manufaa ya vijana pia. Mwaka jana, vijana  walikutana nchini Moroko, ili kushiriki maoni yao kuhusu utawala na kuzijadili sekta nyinginezo.

Tunayajadili masuala mengine mengi pia, kama vile utoshelevu wa chakula. Hivi majuzi tulihitimisha kikao kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Ni raia/wakazi wa nchi pekee wanaoweza kuiendeleza nchi yao.

Mabunge ya kitaifa yanaweza kuchagua mawazo kutoka kwa mijadala yetu kwa ajili ya uundaji wao wa ndani, nasi tunaweza kuchagua kutoka kwenye majadiliano yao pia kwa lengo la kuboresha. Tuna wanachama watano kutoka kila taifa mwanachama wa AU. 

Kwa mfano, kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Rais William Ruto wa Kenya aliwasilisha maazimio kutoka kwa mkutano wa bunge letu huko Midrand, Afrika Kusini, Mei 15 na 16, 2023, kwenye Mkutano wa Kilele wa Tabianchi  wa Afrika mnamo Septemba 2023 jijini Nairobi kwa wakuu wote wa mataifa ya Afrika kuyaandama. Akiwa bingwa wa mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa wakuu wa mataifa, Rais Ruto alikuwa mgeni rasmi Midrand.

Vipi kuhusu Eneo la Biashara Hura la Bara Afrika? 

Pia tulikuwa na mkutano kuhusu Eneo la Biashara Hura la Bara Afrika, ambalo tunatarajia kubadilisha utajiri wa bara hilo kupitia biashara na kukuza chumi zetu.

Tunataka Bunge la Afrika liwe bunge la wananchi na kuhakikisha kuwa AU inawatimizia wananchi wa bara hili.

Tunahitaji kutekeleza jukumu hilo la uangalizi ili kuhakikisha kuwa Afrika inatimiza malengo yake ya Ajenda 2063.

 Ni lazima tufuatilie kama tunapata thamani ya fedha zinazotumiwa na nchi zetu kwenye programu za AU.

Ni lazima tubainishe Waafrika wanataka nini kisha tuishauri AU, ili iboreshe na itimize kwa manufaa ya bara bora. Mabara yaliyoendelea yameendelea kwa kuungana na kuepuka (migawanyiko) missing in the original draft

Ni wakati mwafaka wa sisi kuuchukua mwelekeo chanya kwa manufaa ya bara letu.

More from this author