Waafrika wengi waliohitimu wanagundua kuwa shahada zao za chuo kikuu hazitoshi kupata kazi katika soko la sasa la kazi.
Ruth Rono alihitimu kutoka Chuo kikuu cha Chuka, Kenya mwaka 2015 na shahada ya daraja ya kwanza. Baada ya kutafuta kazi kwa miaka mingi, Bi. Rono alilazimika kufanya kazi za sulubu kama vile kuwalimia watu mashamba yao.
Katika eneo la Kusini, Banji Robert alihitimu na shahada ya uchumi na hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Zambia mwaka wa 2016 na angependa kupata kazi za ngazi za mwanzo katika mojawapo ya taaluma hizi. Baada ya kutofanikiwa kwa miaka miwili baadaye, Bw. Robert kwa sasa anafanyakazi ya kupokea pesa katika duka la mboga.
"Sio rahisi kulipia mahitaji yako, sisemi kuanza familia," Bw. Robert mwenye umri wa miaka 25, aliiambia Afrika Upya. "Kuna shinikizo kubwa ikiwa una elimu lakini huna kazi."
Mhitimu wa Masuala ya Maendeleo, Robert Sunday Ayo, mwenye umri wa miaka 26, anajipata katika hali kama iyo hiyo. "Ni jambo la kusikitisha sana kwamba haiwezekani kupata kazi hata ukiwa na wasifukazi kama wangu," anasema kwa uchungu, huku akiongeza kuwa kwa sasa anaendesha teksi jijini Abuja, Nijeria.
Afrika Upya ilihoji vijana wengi kutoka bara la Afrika ambao walieleza kushangaa kwao kwamba elimu yao haiwasaidii kusonga mbele katika taaluma zao.
Ujuzi wa Kimsingi
Sababu mojawapo ya waliohitimu kukosa ajira ni kuwa "vijana wengi kutoka Afrika iliyo kusini mwa Sahara hutoka chuoni bila ujuzi wa kimsingi wa kuendeleza maisha yao," asema Siddarth Chatterjee, Mratibu wa Makazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya. "Inamaanisha kuwa kuna tatizo kuhusu uekezaji katika elimu."
Kwa ujumla, kwa mujibu wa Benki ya Dunia, asilimia 60 ya waliokosa ajira ni vijana na ukosefu huu unawafanya wengi kujiingiza katika uhalifu, itikadi kali au safari hatari ya uhamiaji kwenda bara Ulaya kupitia Mediterranean kutafuta kazi bora, anasema Bw. Chatterjee
Kutokana na matumizi ya teknolojia, hali hii huenda ikawa mbaya zaidi kwa waliohitimu hasa katika siku zijazo.
Kulingana na mbabe wa sera, Kituo cha Mageuzi ya Kiuchumi cha Afrika kilichoko jijini Accra, karibu asilimia 50% ya waliohitimu kutoka vyuo vikuu barani Afrika hawapati kazi.
Sababu kuu ya tatizo hili ni kutowiana kwa elimu wanayoipata na matakwa ya soko la kazi, anasema Sarah Anyang Agbor, Kamishna wa Umoja wa Afrika wa Wafanyakazi, Sayasi na Teknolojia.
Joseph Odunga, ambaye amefundisha hisabati nchini Kenya na Botswana anakubaliana naye na anasema, "Masomo tuliyokuwa tunafundisha katika miaka ya tisini bado ndiyo tungali tunafundisha hadi leo." Anaeleza kuwa mtaala wa sasa wa baadhi ya masomo umepitwa na wakati.
Maoni hayo pia yanashikiliwa na Bi. Agbor anayesema kuwa "kwa ujumla ni kweli kuwa katika mataifa mengi [barani Afrika], mifumo ya elimu imebuniwa kuwezesha watu kuhitimu kuliko kupata ujuzi na stadi zinakazowezesha mtu kufaulu katika mazingira ya kazi.”
Sekta zenye matumaini
Huku wengine wakilalamikia ugumu wa kupata kazi, sekta kama vile ujenzi, viwanda, uchumi wa kidijitali, uchukuzi, benki, huduma za afya na uhandisi bado zinahitaji wataalamu, anasema Anne-Elvire Esmel, Afisa wa Mawasiliano Madhubuti wa shirika la AfroChampions Initiative ambalo linaendeleza makampuni yenye asili yake barani Afrika.
Kutowiana kwa matakwa ya soko la kazi na ujuzi wa wahitimu wengi Afrika kumedhihirishwa na serikali ya Kenya ambayo imezindua "Mtaala Unaolenga Umilisi," unaotumiaa teknolojia ya kidijitali kufundisha wanafunzi wanaolenga habari na mawasiliano. Watahitaji ujuzi wa kiteknolojia kuingia katika sekta inayokua haraka nchini humo ya programu za kidijitali.
Bi. Esmel angependa mataifa yaandae "kozi nyingi zinazolenga kusuluhisha changamoto zinazohusu uchumi, kuwapatia wahitimu ujuzi unaofaa soko la kazi na kuekeza katika sayasi, teknolojia, uhandisi na hisabati [STEM] — Jambo ambalo kwa sasa halizingatiwa sana.”
Shirika lake linapendekeza ukuzaji wa muundomsingi katika Afrika utakaotumia ujuzi wa wenyeji kutekeleza miradi.
"Tuna mahitaji mengi ya muundomsingi ambao unafaa kutoa nafasi kwa idadi kubwa ya vijana katika mwongo ujao," anasema Bi. Esmel. Anasisitiza haja ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi na ufundi katika sekta ya ujenzi pamoja na viwanda vya kawi na nishati.
Hata hivyo, tatizo ni kuwa, "Elimu ya Mafunzo ya Kiufundi [TVET] inadunishwa kuwa masomo ya hali ya chini, licha ya uwezo wake wa kuimarisha kupata na kuendeleza ujuzi wa kijasiriamali na uvumbuzi wa mtu kujiajiri," analalamika Bw. Chatterjee.
Pamoja na ugavi wa rasilimali za kutosha, anasema "kutumia vifaa vya kisasa vya mafunzo na masomo katika Taasisi za Mafunzo ya Kiufundi na mafundisho na maendeleo ya kitaaluma ya walimu wa Taasisi hizi" kutawezekana.
Kwa ujumla Mataifa ya Kusini mwa Sahara hutumia asimilia 5 ya Pato la Taifa kwa elimu. Mwaka 2015, kule Incheon, Korea Kusini, Jukwaa la Elimu la Dunia liliidhinisha mkataba unaohitaji mataifa kutumia asilimia 4-6 ya Pato la Taifa au asilimia 15-20 ya matumuzi yao ya umma kwa elimu. Shirika la UNESCO liliandaa jukwaa hilo kwa msaada kutoka asasi nyingine za Umoja wa Mataifa pamoja na Benki ya Dunia.
Ripoti ya hivi majuzi inaonyesha kwamba taifa la Zimbabwe, Eswatini (lililojulikana kama Swaziland awali) na Senegali yametimiza au kupita asilimia 6 ya Pato la Taifa, huku Sudan Kusini, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea-Bissau, Uganda na Madagascar miongoni mwa mengine, yanatumia chini ya asilimia 2.5 ya Pato la Taifa katika elimu.
Wasiwasi mwingine ni kuwa kiasi kikubwa cha matumizi ya elimu (kiwango cha asilimia 85) ni ya mambo ya kawaida, ikiwa ni pamija na asilimia 56 ambayo hutumika kulipia mishahara.
Waziri wa awali wa elimu nchini Kenya, Amina Mohammed, hatoi hana msimamo mkali kwa mifumo ya elimu Afrika na ansema, "Mifumo mingi ya elimu ina mitaala inayojumuisha ukuzaji wa ujuzi. Hii ndiyo sababu kwa miaka mingi mataifa mengi ya Afrika yameimarisha wafanyakazi wengi wanaoimarisha ajenda yake maendeleo.
Katika mahojiano na Afrika Upya, Bi. Amina alisema, "Kivyake, ukosefu wa ajira sio tatizo la mifumo ya elimu na ujuzi pekee. Kuna masuala mengi yanaochangia ukosefu wa ajira, kama vile ustawi wa kijamii na kisiasa, mifumo ya kiuchumi na mabadiliko ya kilimwengu pamoja na maendeleo ya kijumla ya uchumi wa mataifa."
Bara Afrika lahitaji waundaji wa kazi
Bi. Amina anapendekeza kuwa bara la Afrika linahitaji waundaji kazi — hasa wajasiriamali. "Tunahitaji Silicon Valley za Afrika katika kila pembe la bara hili. Chumi zinazostawi duniani zimejengwa kwa msingi wa wa mazingira yanayowezesha ujasiriamili kukua.”
"Makampuni ya kimataifa kama vile Facebook, Twitter, LinkedIn na WhatsApp yanaajiri mamia ya maelfu ya watu moja kwa moja au vinginevyo," alizidi kusema Bi. Mohammed.
Wengi wanasubiri maeneo huru ya biashara barani Afrika, na soko moja la Afrika la bidhaa na huduma linalotarajiwa kuanzishwa katika miezi ijayo ambalo litawezesha vijana Waafrika walio na ujuzi kusafiri kutafuta kazi bila vizuizi katika masoko.
Pia, Aya Chebbi, Balozi wa Vijana wa Umoja wa Afrika anasema kuwa bila kuwa na ujuzi unaofaa, huenda vijana wasifaidike vilivyo kutokana na muungano wa kiuchumi barani. Anashikilia wito wa wengine kuhusu kubadilishwa kwa mitaala ya elimu barani Afrika ili iwiane na soko la kazi la sasa.
Bi. Chebbi anasema kuwa vijana wanaweza kunoa ujuzi wao wa kijasiriamali wakilenga sayansi, teknolojia, uhandisi, ujasiriamali na hisabati na wapate mafundisho kwenye kazi.
Mnamo Desemba 2018, Jukwaa la kwanza la Mafundisho ya Kiufundi lilikutana Moroko. Lengo lilikuwa kukuza ushirikiano miongoni mwa Mataifa ya Afrika kuimarisha upatikanaji wa mafundisho ya kiufundi kwa vijana. Jukwaa hilo liliashiria kuwa mataifa ya Afrika yanazidi kutambua umuhimu wa mafundisho ya kiufundi.
Bi. Esmel anashauri kuwa sekta ya kibinafsi sharti ichangie juhudi za serikali.
Bi. Agbor anakubaliana naye na kusema, "sekta ya kibinafsi inafaa kuhusishwa kisawaswa katika mifumo ya elimu na mafundisho ili kutimiza matakwa ya soko." Anahimiza makampuni kutoa nafasi ya mazoezi ya kazi, kazi kwa muda, ushauri wa mafunzo kwa vijana pamoja na programu za vyeti vya ujuzi.