Afrika lazima iwazie mzigo wake wa deni pindi tu janga hili litakapodhibitiwa

Get monthly
e-newsletter

Afrika lazima iwazie mzigo wake wa deni pindi tu janga hili litakapodhibitiwa

— asema Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia
Raphael Obonyo
Afrika Upya: 
28 September 2020
Kituo cha umeme cha joto huko Takoradi, Ghana
Jonathan Ernst/World Bank
Wafanyakazi wanadumisha kituo cha umeme cha Takoradi, Ghana, Juni 21, 2006.

Carlos Felipe Jaramillo aliteuliwa hivi karibuni kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia wa Kanda ya Marekani Kusini na Karibia. Hadi kuteuliwa kwake hivi karibuni, alikuwa mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Kenya, Rwanda, Uganda na Somalia, jijini Nairobi. Raphael Obonyo alimhoji Bwana Jaramillo kuhusu juhudi za Benki ya Dunia katika kusaidia nchi za Afrika kukabili na kupata nafuu kutoka kwa COVID-19.

Carlos Felipe Jaramillo
Carlos Felipe Jaramillo

Afrika Upya: Je, Benki ya Dunia inasaidiaje nchi kama Kenya na nyingine kukabili na kushinda athari za janga la COVID-19?

Bw. Jaramillo: Tumekuwa tukilenga sana kusaidia nchi kama Kenya kukabili janga la COVID-19 kupitia juhudi pana za kiulimwengu. Katika ya miezi mitatu ya kwanza ya janga hili, tuliweza kuidhinisha kwa haraka mikopo 100 ya dharura kwa nchi 100, zikiwemo Kenya, Somalia, Uganda na Rwanda.

Kwa Kenya haswa, tulitekeleza malipo ya dharura haraka, kutoka kwa mradi unaoendelea, ya dola milioni 10 katikati ya mwezi wa Machi ili serikali ianze mara moja kununua vifaa vya upimaji, vifaa vya kujikinga kibinafsi (PPEs), vifaa vya maabara na bidhaa nyingine muhimu. Hii iliiwezesha Kenya kuandaa vyumba vya kutenga watu na matendo mengine ya dharura. Mapema Aprili, tuliidhinisha mkopo wa kwanza wa dola milioni 48 kusaidia mahitaji ya ufadhili wa Wizara ya Afya na mfumo mzima wa afya.  

Janga lilipozidi kuongezeka na kuathiri uchumi mpana na njia za kupata riziki, tulianzisha hatua ya pili, ambayo ni mkopo wa dhamana wa dola bilioni 1 kusaidia serikali kuendelea kufadhili shughuli zake na kutoa huduma za umma. Isitoshe, tuliongeza mgao wa Benki ya Dunia wa programu za kulinda Wakenya.

Tunaendelea kusaidia mpango wa Inua Jamii unaosaidia familia masikini, mayatima na wazee. Familia zingine milioni 1.1 za Kenya zimefaidika kutokana na mpango huu. Tunataka kuweka kipaumbele msaada wa biashara ndogondogo (MSMEs), ambazo hutoa ajira na njia za kupata riziki kwa Wakenya wengi wa kawaida.

Je, vipi kuhusu kupata nafuu baada ya janga. Benki ya Dunia inawezaje kusaidia? 

Kuna vipaumbele vitatu kuu kwa Kenya ambavyo pia nadhani vinafaa sana kwa Afrika Mashariki yote. Kwanza ni ajira na biashara ndogondogo (SMEs), ambazo ndio uti wa mgongo wa uchumi. Tunasaidia kukuamua hizi biashara ambazo nyingi zinaongozwa na wafanyabiashara wachanga na kuajiri vijana wengi.

Pili ni kuimarisha uchumi wa kidijitali. Uwezo wa kidijitali umedhihirika kuwa nyenzo muhimu wakati wa janga hili, ukiruhusu watu kufanyia kazi nyumbani na watoto kuendelea kusoma. Hata wagonjwa wanaweza kupata ushauri wa kimatibabu kupitia njia za kidijitali na kwa kweli tuna malipo ya kidijitali na huduma zingine za kifedha za kidijitali.

Uchumi wa kidijitali utakuwa sehemu ya njia tutakazotumia kufanya biashara siku zijazo. Kenya inaongoza katika hili ulimwenguni, na nadhani inahitaji kuendelea kuwa mfano bora kwa Afrika na kwa ulimwengu. Lakini kuna haja ya kuwa na uwekezaji zaidi katika sekta hii ili kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya Wakenya wa kawaida wanapata mtandao mpana.

Tatu ni maji na usafi wa mazingira. Aidha, janga hili limefunua jambo ambalo tulilijua hapo awali, ambalo ni kwamba nchi zetu zinakabiliwa na uhaba sugu wa maji, kwamba miji mikubwa na vituo vya uchumi vimepungukiwa sana na maji na kwamba kilimo mara nyingi kinatatizwa na ukame. Wakenya wengi sana hawapati maji na hawana mazingira safi. Kwa mfano, katika kaunti za Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa Kenya, maji salama ya kunywa hupatikana kwa chini ya nusu ya watu na thuluthi moja tu ndio wanaofikia usafi wa mazingira ulioboreshwa.

Select Author: 

Je, unaweza kusema mafanikio yako makubwa ni yapi baada ya kuhudumu Kenya, Rwanda, Uganda na Somalia? 

Benki ya Dunia ina lengo la kumaliza umaskini ulimwenguni kote na kukuza ustawi wa pamoja, na ninajivunia kazi ambayo tumefanya katika maeneo mengi. Tunahusika katika kuimarisha afya, elimu, usalama wa jamii, uendelevu wa mazingira na kilimo na kusaidia sekta binafsi. Ninajivunia pia ukabili wa COVID-19 katika miezi iliyopita. Ninafurahia miradi yetu ya kilimo nchini Kenya na nchi zingine.

Mradi wa Kilimo Bora kwa Hali ya Hewa Kenya, wenye thamani ya dola milioni 250, unakusudia kuongeza uzalishaji wa kilimo na kujenga uwezo wa kukabiliana na hatari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wakulima wadogo na kwa jamii za wafugaji.   Mradi huo ni bunifu sana, unakuza utafiti na mafundisho kwa wakulima kuhusu mazoea bora kwa hali ya hewa.

Nafurahia pia msaada tuliotoa kwa programu ya e-voucher ya serikali ya Kenya kwa wakulima wadogo maskini. Wakulima hawa hupokea hela za kununua mbegu na mbolea.

Nchini Rwanda, tulisaidia kuimarisha uafikiaji wa umeme. Mwaka wa 2009, ni asilimia 6 tu ya wakaazi wa Rwanda walikuwa na huduma ya umeme; leo hii imeongezeka hadi asilimia 40 hivi. Pia, asilimia 100 ya hospitali nchini Rwanda na asilimia 80 ya shule sasa zimeunganishwa na umeme.

Nchini Uganda, katika miaka mitatu iliyopita tulitafuta dola milioni  500 ya ufadhili kusaidia wakimbizi na jamii wenyeji wao katika kuboresha vituo vya afya, elimu, huduma za maji, miongoni mwa nyingine.   Hii ilikuwa katika katika kusaidia sera bora ya Uganda ya uwazi kwa wakimbizi.

Mwishowe, tulirekebisha uhusiano kati ya Benki ya Dunia na Somalia kupitia malipo ya madeni yote yaliyokuwa yakidaiwa na benki, IMF na wengine. Somalia, kwa mara ya kwanza kwa karibu miongo mitatu, sasa inaweza kunufaika kutoka kwa rasilimali za Benki ya Dunia. Nina matumaini makubwa kuwa haya yatasaidia kuirejesha nchi hii katika njia inayofaa.

Je, Benki ya Dunia  inasaidiaje Kenya kuyafikia malengo yake ya maendeleo?

Ninajivunia Mpango wa Maendeleo ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki (NEDI) ambao Benki ya Dunia ilizindua mwaka wa 2018, na ufadhili wa dola bilioni 1. Maeneo ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa Kenya kihistoria hayajatumikiwa vilivyo na yako chini ya wastani wa kitaifa kwa mujibu wa vipimo vya maendeleo. Tumelenga umeme, maji, kilimo na shughuli za wafugaji na afya, na tunajaribu kusaidia eneo hilo na kaunti hizo kuboresha maisha ya watu wao.

Pili ni Ugatuzi. Tuna miradi kadhaa inayoendelea kama vile Programu ya Uwajibikaji wa Ugatuzi ya Kenya na Programu ya Usaidizi wa Ugatuzi ya Kenya ambayo inayolenga kusaidia serikali za kaunti kukwamuka, kuwapa msaada wa kiufundi na kujenga uwezo. Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa serikali za ugatuzi, serikali mbili za kaunti zilipata ripoti bora katika ukaguzi wa hesabu za matumizi. 

Kuendelea mbele, ni maeneo yapi ambayo nchi za Afrika lazima zishughulikie katika suala la utawala? 

Ufisadi ni tatizo. Benki ya Dunia inajiunga na serikali zote na raia katika kupambana na tatizo hili. Wakati wa hatamu ya uongozi wangu, tulishinikiza kuimarishwa kwa uwazi, udhibiti wa ndani na ukaguzi wa hesabu ili kuzuia matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Tulisaidia katika kuanzisha [nchini Kenya] Mtandao wa Habari ya Ununuzi wa Umma www.tenders.go.ke, unaochapisha maelfu ya kandarasi za serikali zilizotolewa, pamoja na habari za kiwango cha fedha, kampuni iliyopatiwa kandarasi, na wamiliki wa kampuni hilo. Mtandao huo unajumuisha habari kuhusu taasisi za serikali na wafanyakazi waliounda jopo la uteuzi. Huu ni mfano bora wa jinsi ya kutumia zana za kidijitali kukuza uwazi na uwajibikaji serikalini.

Tunahitaji kuendelea kuimarisha taasisi, michakato na uwezo.

Ninajivunia Mpango wa Maendeleo wa Kaskazini na Kaskazini Mashariki (NEDI) ambao Benki ya Dunia ilizindua mnamo 2018, na ufadhili wa $ 1 bilioni.

Je, Benki ya Dunia inasaidiaje familia zilizo hatarini zaidi?

Tuna miradi kadhaa inayolenga hayo. Ningependa kuzungumzia miwili. Mojawapo iliyo bunifu nchini Kenya, na nadhani ya kwanza ya aina yake, inaitwa Programu ya  Bima ya Mifugo ya Kenya iliyoanzishwa mwaka wa 2015. Mradi huu unalinda wafugaji, haswa katika kaunti masikini na zenye ukame, dhidi ya upotezaji wa mifugo yao kukiwa na ukame. Njia ya kufanya hivyo ni kupitia picha ya setilaiti. Upotezaji wa malisho ukitambuliwa na setilaiti, malipo kwa familia huanzishwa. Mwaka jana tulikuwa na familia 20,000 zilizo katika hali hatarishi zilizopewa bima na tunajaribu kuongeza.

Mradi wa pili ni Mradi wa Ajira na Fursa kwa Vijana wa Kenya ambao unalenga kufundisha vijana, kuwasaidia kupata ajira zao za kwanza na kuwafanya wawe na tija.

Tumejitolea pia kuwapa wanawake uwezo ili kuhakikisha kuwa Kenya inaongeza tija katika uchumi wake na kuimarisha matokeo ya maendeleo. Benki inasaidia serikali katika kujumuisha usawa wa kijinsia katika muundo wa miradi na utekelezaji. Janga la COVID-19 limefichua hatari iliyopo kwa wanawake na wasichana na aina tofauti za unyanyaswaji wa kijinsia (GBV), kumekuwa na ongezeko kubwa la visa vilivyoripotiwa katika miezi ya hivi karibuni.

Je, ni kwa namna gani ambayo Benki ya Dunia inashughulikia viwango vya madeni ya nchi?

Kwa bahati mbaya, nchi nyingi za Afrika zina viwango vya juu vya madeni na hiyo inamaanisha kuwa hazina rasilimali za kutosha za kifedha kukabili janga hili na kusaidia watu na biashara ndogondogo kuhifadhi ajira. Ni muhimu kuwa na viwango vya wastani vya madeni ili kuweza kukabili mshtuko usiotarajiwa. Na tunayo furaha kuendelea kufanya kazi na nchi kuimarisha mifumo ya kifedha. Janga litakapodhibitiwa na uchumi kuanza kupata nafuu, kisha kipaumbele kitakuwa kushughulikia suala la madeni.