Kukabiliana na urithi wa utumwa kwa kulipa fidia

Get monthly
e-newsletter

Kukabiliana na urithi wa utumwa kwa kulipa fidia

Bi. Epsy Alejandra Campbell Barr, Mwenyekiti wa Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Kiafrika, anawahimiza wazawa wa Kiafrika na Waafrika kushirikiana katika kushughulikia changamoto zinazofanana.
Kingsley Ighobor
Afrika Upya: 
20 March 2024
UN
Epsy Barr - Mwenyekiti, Jukwaa la Watu Wenye Asili ya Kiafrika.

Epsy Alejandra Campbell Barr aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Kosta Rika kuanzia 2018 hadi 2022 na kwa sasa ni mwenyekiti wa Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Afrika lililoanzishwa na Umoja wa Mataifa, linalolenga kuboresha hali ya kijamii na kiuchumi ya vizazi vya Afrika. Katika mahojiano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York na Kingsley Ighobor wa Afrika Upya, Bi Campbell Barr anajadili juhudi za Jukwaa hilo kushughulikia changamoto zinazowakabili wazawa wa Afrika. Hapa kuna madondoo kutoka kwa mahojiano hayo:

Jukwaa la Kudumu la Watu Wenye Asili ya Kiafrika, ulilo Mwenyekiti wake, lilianza mwaka wa 2021. Je, unaweza kutoa maelezo zaidi kuhusu malengo yake?

Kwanza, ninataka kusisitiza kwamba kuna zaidi ya watu milioni 200 wenye asili ya Kiafrika katika mabara ya Amerika na Karibiani. Brazil pekee ina idadi ya watu zaidi ya milioni 100 wenye asili ya Kiafrika.

Mizizi yetu inaanzia Afrika, hasa kutokana na biashara ya utumwa iliyovuka Atlantiki inayohusisha ulanguzi wa Waafrika kwenda maeneo ya Amerika. Idadi kubwa ya watu wa asili ya Kiafrika ni wazawa wa wale ambao walivumilia wakati huu kutisha katika historia.

Kwa miaka mingi, tumekuwa tukishiriki mijadala kuhusu haki za watu wenye asili ya Kiafrika.

Hatua kubwa ilifikiwa wakati wa Kongamano la Dunia la Kupinga Ubaguzi wa Rangi, Ubaguzi dhidi ya Watu kutoka Mataifa mengine na Kutovulimiana Kwingineko  lililoofanyika Durban, Afrika Kusini, mwaka wa 2001, ambapo, kwa mara ya kwanza, vizazi vya Waafrika vilitambuliwa rasmi kuwa kundi linalokabiliwa na ubaguzi wa kimfumo na ubaguzi wa rangi.

Utambuzi huu ulikuwa hatua muhimu, ikizingatiwa kuwa mapambano yetu ya haki yalianza na utumwa wa mababu zetu.

Ilichukua muda mrefu kwa jumuiya ya kimataifa kututambua kama watu wa asili ya Kiafrika, na kutambuliwa zaidi kulipatikana kupitia Umoja wa Mataifa. Azimio la Baraza Kuu la Mwongo wa Watu wa Asili ya Kiafrika [2015 hadi 2024] linaashiria utambuzi wa Umoja wa Mataifa wa uhalisia wetu wa ubaguzi wa rangi na kutengwa kwa msingi wa rangi.

Hata hivyo, tunaendelea kutafuta maendeleo ya programu maalum kwa manufaa ya Waafrika na watu wa asili ya Kiafrika.

Tunatoa wito wa kuungwa mkono zaidi kutoka kwa jumuiya mbalimbali za wazawa wa Kiafrika katika mabara ya Amerika, Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika, kuungana na kudai haki zao.

Kulingana na data iliyopo, watu wa asili ya Kiafrika wako katika matabaka ya chini kabisa katika jamii, iwe katika nyanja za kijamii, kiuchumi au kisiasa. 

Katika enzi yangu kama Makamu wa Rais wa taifa langu [Kosta Rika], serikali yetu ilisimamia kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili ya Kiafrika, ambayo sasa inaadhimishwa tarehe 31 Agosti. Kwa kushirikiana na Chad, tuliongoza juhudi za kutafuta uungwaji mkono kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha Azimio la kutekeleza Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Afrika

Je, watu milioni 200 wa Asili ya Kiafrika wanaoishi ughaibuni wanafanana nini na Waafrika?

Kwanza, unaponiona, unaona mwanamke wa Kiafrika. Tayari tunajitambulisha kama wazawa wa Kiafrika.

Pili, tunashiriki historia moja iliyoanzia Afrika.

Tatu, historia hii iliwekwa alama na ukoloni.

Nne, tumedumisha utamaduni wa Kiafrika, ambao umepitia mageuzi katika sehemu mbalimbali za dunia huku ukidumisha mizizi katika historia ya Kiafrika. Tunachukuliwa kama watu weusi duniani kote.

Hatimaye, tunatambuliwa kama watu weusi duniani kote, ambayo ina maana kwamba tunakumbana na changamoto sawa na mataifa ya Afrika.

Umoja wa Afrika unatambua Dayaspora ya Afrika kama kanda ya sita ya bara hilo.

Tunakabiliwa na ubaguzi wa kimfumo, hata ndani ya mataifa yetu wenyewe, hata baada ya karne nyingi za kuishi katika ulimwengu huu.

Tumechangia maendeleo ya mataifa haya, lakini hatuchukuliwi kuwa sawa. Tunavumilia viwango vya juu vya umaskini, fursa chache za maendeleo ya kiuchumi, na mara nyingi tunatengwa katika nyanja za kisiasa.

Nilipochaguliwa kuwa makamu wa rais wa taifa langu, iliwashangaza wengi kuwa mwanamke mwenye asili ya Kiafrika anaweza kushika wadhifa huo katika nchi isiyo ya watu weusi.

Je, Jukwaa linashirikiana na serikali za Afrika?

Tunahitaji ushirikiano zaidi na serikali za Afrika. Ni lazima tuwe na uelewa wa kisiasa kwamba uhalisia wetu unafungamana na ule wa Afrika.

Hivi majuzi, niliwasilisha ripoti yangu kama mwenyekiti wa Jukwaa la Kudumu kwa Kamati ya Tatu ya UN, na hakuna nchi moja ya Kiafrika iliyochukua nafasi ya kushiriki.

Nilifurahi kupokea mwaliko kutoka kwa Rais wa Ghana kuhudhuria mkutano mkuu kuhusu ulipaji fidia [14 – 17 Novemba 2023]. Kama Jukwaa, tunaamini kwamba fidia ni suala muhimu kwa Waafrika na vizazi vya Kiafrika. 

Je, unashirikiana vipi na mashirika mbalimbali ya UN, fedha, na programu?

Tunashirikiana kwa karibu na mashirika kadhaa ya UN, kama vile UNFPA, ambapo Bi. Natalia Kanem, mkurugenzi mkuu, anajishughulisha kikamilifu na kazi yetu. Pia tunashirikiana na UN Women, hasa kuhusu masuala yanayohusiana na wanawake wa asili ya Kiafrika katika Karibiani.

Ingawa tunashirikiana na mashirika mengine, tunahitaji usaidizi mkubwa zaidi, kwa kuzingatia mamlaka yetu, ambayo ni pamoja na kuyashauri mashirika haya na Baraza Kuu.

Hata hivyo, tunahitaji usaidizi zaidi wa kiutaratibu na kiusimamizi. Ni muhimu kuanzisha uhusiano wa karibu zaidi wa kufanya kazi na mashirika mbalimbali ya UN, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu.

Je, mnashirikiana na asasi za kiraia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali?

Bila shaka, tuna wajibu wa kushauriana na mashirika ya kiraia. Tumekuwa na vikao vya wazi huko Geneva na New York, na zaidi ya mashirika ya kiraia 1,600 na mashirika ya kijamii yakishiriki. Mnamo Disemba, tunapanga kufanya mashauriano na mashirika ya kiraia barani Ulaya, Amerika Kusini, Karibiani na Mashariki ya Kati.

Tuko katika harakati za kukusanya taarifa kuhusu watu wa asili ya Kiafrika katika Mashariki ya Kati na maeneo mengine. Mashirika ya kiraia yanatoa usaidizi wa thamani sana, kuwezesha kazi yetu ndani ya UN. Bila uungwaji mkono wao, hatua zetu zingekwazwa. Hatuwezi kutegemea tu vikundi vichache vya wataalam; lazima tushirikiane na vikundi mbalimbali vya kiraia duniani kote.

Jukumu lenu linaonekana kulenga zaidi utetezi. Je, utetezi unageuka vipi kuwa sera zinazoweza kutekelezeka? Je, kwa mfano, mnatoa mapendekezo ya sera kwa serikali?

Hakika, tumepewa mamlaka ya kutoa mapendekezo na kutoa ushauri kwa Baraza Kuu. Mojawapo ya malengo yetu ni kufikia azimio la haki za binadamu kwa watu wa asili ya Kiafrika, ambalo lingetumika kama mfumo wa haki zao.

Jukumu letu linaenda zaidi ya mazungumzo tu; pia tunawezesha ubadilishanaji wa tajriba, ikiwa ni pamoja na mbinu bora katika nyanja mbalimbali na kukusanya data muhimu ili kuonyesha uhalisia wao kwa usahihi.

Ajenda ya SDG inajumuisha malengo ya kushughulikia ukosefu wa usawa wa rangi. Lazima tushiriki katika Mkutano wa Upeo wa Usoni.  Tunahitaji kushiriki katika majadiliano kuhusu akili unde, kwa kuzingatia pengo la algorithi ya rangi ambalo linatuathiri isivyo sawa.

Jukwaa lenu pia lina jukumu la kukusanya data iliyogawanywa kuhusu watu wa asili ya Kiafrika, kwa kuzingatia masuala kama vile jinsia, umri, rangi, kabila na mengineyo. Je, mmepiga hatua zipi katika suala hili?

Uchanganuzi wa data ni muhimu kwa sababu hutuwezesha kufahamu jinsi ubaguzi wa rangi unavyojitokeza katika nyanja mbalimbali za maisha—uchumi, afya, makazi na mengineyo—ili tuweze kutunga sera zinazoshughulikia changamoto zilizopo. Tumepiga hatua kubwa katika eneo hili. Kwa mfano, nchi nyingi za Amerika ya Kusini zimejumuisha maswali yanayohusiana na kujitambulisha katika sensa zao.

Tume ya Uchumi ya UN katika Amerika ya Kusini pia inashiriki kikamilifu katika kukusanya data muhimu.

Juhudi hizi zimesababisha data muhimu na wasifu wa kina wa watu wa asili ya Kiafrika.

Hata hivyo, bado tunahitaji data iliyogawanywa zaidi, hasa katika mfumo wa afya duniani.

Nchi lazima zifanye zaidi. Katika sensa ya Panama ya 2010, kwa mfano, takriban asilimia 9 ya watu walijitambulisha kama watu wa asili ya Kiafrika. Hata hivyo, katika sensa iliyofanyika mwaka jana, zaidi ya asilimia 30 ya watu walijitambulisha hivyo.

Muda wako unapokamilika, unatarajia kuacha urithi gani, na unafafanuaje mafanikio?

Kwanza, tunapaswa kufikia azimio la haki za binadamu kwa watu wa asili ya Afrika, ili kuboresha maisha ya mamilioni ya watu kwa kiasi kikubwa.

Pili, tunahitaji nia njema ya kisiasa kuhusu suala la fidia. Lazima tukabiliane na urithi wa kudumu wa siku za nyuma, kwani unaendelea kuathiri maisha ya mamilioni ya watu binafsi.

Tatu, ninatazamia kuanzishwa kwa mfuko wa kifedha wa kimataifa wa watu wa asili ya Kiafrika. Tunahitaji rasilimali za ziada kushughulikia changamoto zinazokabili mamilioni ya watu, hasa wanawake na vijana ambao wanawakilisha sasa na siku za usoni.