Tutashinda janga hili tukisaidiana na kishirikiana pamoja

Get monthly
e-newsletter

Tutashinda janga hili tukisaidiana na kishirikiana pamoja

-Dkt. Theo-Ben Kandetu (Namibia)
Africa Renewal
19 May 2020
Dr. Theo-Ben Kandetu (Namibia)
-Dkt. Theo-Ben Kandetu (Namibia)

Tufahamishe kidogo kukuhusu?

Jina langu ni Dkt. Theo-Ben Kandetu umri wangu ni miaka 31. Nilizaliwa na kukulia Windhoek, jiji kuu la Namibia. Mimi ni Afisa Mwandamizi wa Matibabu katika Idara ya Tiba ya Ndani (Nephrology) katika Hospitali kuu ya Windhoek, hospitali ya rufaa ya kitaifa nchini Namibia.

Dr. Theo-Ben Kandetu (Namibia)
Dr. Theo-Ben Kandetu (Namibia)

Je, umekuwa ukifanya kazi kama mhudumu wa afya kwa muda gani? Je, nini lipi lilikufanya kuchagua kazi ya huduma ya afya? Uko na hofu au majuto yoyote?

Nimekuwa nikifanya kazi kama mhudumu wa afya kwa miaka mitano sasa. Kwangu ni ''mwito''. Nimekuwa nikitaka kuwa daktari kutoka ujanani. Kilichonivutia kwa udakatari ni kuweza kuingilia kati na kumsaidia mgonjwa kupata nafuu kamili. Kusoma bayolojia katika shule ya upili, haswa jinsi mwili wa binadamu unavyofanya kazi, kuliongeza hamu yangu ya kusomea udaktari.

Nimebarikiwa kupata huduma ya afya kama wito wangu maishani na naweza kusema kwa kweli sina majuto. Ingawa, ukiniuliza swali hilo hilo saa nane usiku wakati wa zamu ya masaa 24 katika kituo cha dharura, jibu langu labda litakuwa tofauti. Hiyo ni kusema kuna siku nzuri na siku mbaya, kama taaluma nyingine yoyote.

Uko na hofu yoyote?

Hakika! Kama madaktari wengine, hofu ya kosa katika uamuzi wa kimatibabu, au kusahau kitu katika maelezo ya kimatibabu. Lakini hofu hiyo pia ndiyo inayonichochea kuwa macho wakati wote kwenye kazi, haswa wakati wa zamu ya usiku.

Je, unasaidiaje kupambana na COVID-19 katika nchi yako? Je, kazi yako imebadilikaje tangu kulipuka kwa COVID-19?

Kwa sababu ya uzoefu wangu katika matibabu ya ndani na kama mkuu wa Timu ya Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi katika hospitali, nilipendekezwa kwa Jopokazi la Kitaifa la COVID-19 nchini Namibia.

Tangu COVID-19 kufika Namibia, ratiba yangu ya kila siku imebadilika sana, siku hizi sioni tu wagonjwa katika kiwango cha hospitali, bali nawajibika na kuwa tayari na majibu ya nchi nzima. Timu yangu inawajibika kwa usimamizi wa visa vya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na COVID-19. Hii inajumuisha kuweka sera za kitaifa za usimamizi wa visa, kuratibu juhudi za timu ya kukabiliana na visa kote nchini, na kibinafsi, kufuata usimamizi wa visa vyote vilivyothibitishwa vya COVID-19 nchini.

Je, nini hukuathiri sana katika janga hili la COVID-19? Je, nini hukufanya kuzidi kuendelea na unavyokabili hali hii?

Kile ninachopata kuvunja moyo sana katika mapambano dhidi ya COVID-19 katika nchi yangu ni habari potofu na bandia zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine. Hii labda inatokana na ukweli kwamba mengi kuhusu virusi vipya vya Korona bado hayajulikani. Kwa bahati mbaya, inaonekana ni tabia ya binadamu "kujaza nafasi zilizo wazi" ikiwa watu hawatapata habari au majibu wanayotafuta, iwapo nia yao ni mbaya au la. Jambo la kufadhaisha kuhusu taarifa hizi potofu ni kwamba zinalemaza juhudi na bidii ya timu ya kukabiliana na kutoa taarifa kuhusu COVID-19 kwa kuwa husababisha kutokuaminika na umma.

Kinachonifanya niendelee ni upendo mwingi na msaada mkubwa wa familia yangu. Kwa sababu ya ratiba yangu ya kazi, mara nyingi huwa sili chakula. Familia yangu inahakikisha kuwa ninatunzwa vizuri na kuwa na vifaa vya kuendelea na vita dhidi ya COVID-19 ninapoondoka nyumbani kila asubuhi.

Dr. Theo-Ben Kandetu (Namibia)
Dr. Theo-Ben Kandetu (Namibia)

Kwa mtazamo wako, ni mkakati gani, uliofanya vyema katika mapambano haya na ni upi haukufanya vizuri? Je, nini inafaa kufanywa kushinda vita dhidi ya COVID-19?

Nchini Namibia haswa, nadhani mwitikio wetu wa haraka katika kufunga bandari zetu za kuingia kwa wasafiri wa kimataifa kulituwezesha kudhibiti maambukizi ya COVID-19. Hii, pamoja na hatua zetu kali za kufuatilia ugonjwa huu, kufuatilia waliotagusana na karantini/kufungiwa ndizo zinazosababisha kufanikiwa kwetu kumaliza kuenea kwa ugonjwa wenyewe.

Namibia pia inaripotiwa kuwa nchi ya pili yenye watu wachache ulimwenguni wenye ugonjwa huu (karibu watu 3 kwa kila kilomita ya mraba), ukweli ambao haswa unatufaa ukizingatia jinsi virusi hivi vinavyoenezwa.

Kuhusu jinsi ya kushinda COVID-19?

Kwa maoni yangu, njia ya kushinda vita hivi ni kushirikiana kwa sekta mbalimbali. Watu wote lazima wafanye kazi. Ni muhimu kwa wataalamu wote kutoka sekta zote kujumuishwa katika kutafuta suluhu mahsusi kwa nchi zao. Kila nchi iko katika hatua yake

katika janga la COVID-19, kwa hivyo, suluhisho la nchi A huenda lisitumike kwa nchi B. Kilicho muhimu kwa maoni yangu ni kwa serikali kutoa majukwaa kwa wataalamu wao kujadili suluhisho liwezekanalo kwa shida hii. Aidha, ni muhimu kwa nchi pia kuhusisha mamlaka za kimataifa kama WHO, CDC na CDC ya Afrika katika mchakato wa mjadala. Namibia imefanya vizuri sana katika kushirikisha sekta nyingi.

Je, ujumbe wako kwa watu wa nchi yako na kwa wengine barani Afrika wakati huu wa COVID-19 ni upi?

Ingawa tunaishi katika nyakati zisizo na uhakika, tusije tukasahau ubinadamu wetu. Tusiwachukie walio na COVID-19, au tuwaone kama adui. Tutashinda janga hili tukisaidiana na kushirikiana pamoja.