COVID-19 na kuzinyamazisha Bunduki: Msururu wa Majadiliano kuhusu Afrika 2020 wataka mabadiliko

Get monthly
e-newsletter

COVID-19 na kuzinyamazisha Bunduki: Msururu wa Majadiliano kuhusu Afrika 2020 wataka mabadiliko

Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifaa kuhusu Afrika
Ms. Bience Gawanas
21 May 2020
Bience Gawanas, Special Adviser on Africa

Miaka miwili na nusu iliyopita OSAA ilizindua Msururu wa Majadiliano ya Afrika ukiwa na malengo mawili: kuwezesha majadiliano ya sera kuhusu masuala yenye umuhimu mkuu kwa Afrika; na kuhakikisha kwamba Afrika i katika ngazi ya juu ya ajenda ya Umoja wa Mataifa.

Huenda hii ni mara ya tatu ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika (OSAA) kuandaa Msururu wa Majadiliano ya Afrika kwa utaratibu huu, ila ni mara ya kwanza kabisa kufanyika katika mtandao.

Baada ya Msururu wa Majadiliano ya Afrika kwa nusu siku kwa siku tatu, tunaweza kusema kwamba tumefaulu.

Tumeandaa majadiliano mapevu kuhusu Kuzinyamazisha Bunduki na kukabili COVID-19 barani Afrika, kwa ajili ya wahusika kadhaa.

Kwa sababu hiyo, ningependa kushukuru nchi wanachama, mashirika ya Afrika na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kwa kushiriki kwao katika majadiliano haya. Ninapenda pia kutoa shukrani za dhati kwa wawakilishi wa asasi za kiraia na wasomi ambao wameshiriki majadiliano hayo katika kipindi hicho cha nusu siku kwa siku tatu.

Nilivyosema awali, uongozi hauhusu viunzi, unahusu watu. Na ili kuwasikia watu sharti tujumuishe asasi za kiraia. Ningependa, kwa hivyo, kukariri kujitolea kwa OSAA katika kuendelea kutumiwa kama jukwaa la kuziunganisha asasi za kiraia pamoja na watunga sera na wanaofanya maamuzi.

Katika hotuba yangu ya makaribisho, nilitambua kwamba lengo la Msururu wa Majadiliano ya Afrika lilikuwa kujitokeza na mapendekezo tekelezi kuhusu namna ya kutekeleza mageuzi ya Afrika. Mapendekezo haya yataboreshwa kwa kina katika ripoti itakayoandaliwa na OSAA, hata hivyo, hebu nidokeze baadhi ya hoja hizi.

· Ni muhimu kupunguza tofauti za vizazi na kupiga jeki uongozi jumuishi kwa kuinua maarifa na utaalamu wa viungo vyote katika jamii na kuimarisha ushiriki wa vijana katika kufanya maamuzi.

· Ni muhimu kuchukua mwelekeo mpya kuhusu jinsi tunafanya biashara, kuongoza mifumo ya afya na kuboresha vitekauchumi. Mwelekeo mpya unahitaji uwekezaji mkuu katika elimu na na kuboresha ujuzi. Aidha, uwekezaji wastahili kufanywa katika afya, maji na usafi, ulinzi wa malipo ya uzeeni, ajira na miundomsingi endelevu.

· Uendelevu unastahili kuzingatiwa katika michakato ya kufanya mipango. Janga hili lina athari kuu katika utekelezwaji wa mipango ya maendeleo na mikakati katika viwango vyote na katika mipango muhimu kama ule wa Umoja wa Afrika (AU) wa Kuzinyamazisha Bunduki. Ni muhimu kuzingatia njia bora za kupunguza makali ya matokeo ya majanga kama hili katika michakato ya kuweka mipango.

· Mshikamano wa kimataifa na vitendo vinahitajika kuimarisha mifumo ya afya ya Afrika, kuhakikisha utoaji wa chakula, kuzuia matatizo ya kifedha, kusaidia elimu, kulinda ajira, kulinda jamaa na biashara, pamoja na kulinda bara hili kutokana na athari za mapato na faida za bidhaa ziuzwazo ng’ambo yaliyopotea.

· Mfumo wa kina kuhusu mikopo unahitajika, kuanzia kusitisha kulipa mikopo kwa mataifa yote yasiyoweza kulipa, kukifuatiwa na kuondoa mzigo wa mikopo na mwelekeo wa kina kuhusu masuala ya kimfumo katika usanifu wa mikopo ili kuzuia hali ya nchi kukosa kulipa mikopo yake.

· Jamii ya kimataaifa inastahili kusaidia juhudi za Afrika katika kukabili COVID-19 kupitia kwa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kwa kutumia ununuzi wa pamoja na kuimarisha uwezo wa viwanda asilia kutengeneza bidhaa muhimu; kutoa misaada ya utaratibu wa usafirishaji na ugavi wa bidhaa za matibabu; kuihusisha sekta ya kibinafsi katika kupiga jeki uwezo wa uwajibikaji wa serikali; na kutumia pamoja na kuimarisha ubunifu na matumizi ya teknolojia.

· Kuna haja ya kutekeleza upesi Soko Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) ili kupata usawa kwa manufaa ya watu maskini na vikundi vilivyotengwa vya Afrika.

· Ni muhimu kusahilisha taratibu za usajili na kutoa vichochezi vya kibiashara kwa washikadau katika sekta zisizo rasmi ili kuwawezesha kurasimisha shughuli zao kwa kutoa misaada kwa biashara ndogondogo na zile wastani nyakati za matukio mabaya kwa biashara kimataifa.

· Kusitisha vita kimataifa ni muhimu ili mataifa ya Afrika yaweze kuendeleza juhudi zao katika kuzinyamazisha bunduki na kulikabili tatizo la itikadi kali, na kuweza kulenga juhudi zote katika janga la COVID-19.

· Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano kamili wa serikali za Afrika na washikadau wa kieneo, wanastahili kutathmini na kurekebisha vyombo vya kuzuia na kusuluhisha mizozo ili kusaidia kukabili kikamilifu mizozo, vurugu na uhalifu unaochukua sura mpya kila mara barani Afrika.

· Serikali kuu zinastahili kuhakikisha kwamba wanawake na vijana wanahusishwa katika vipengele vyote vya mizozo na michakato ya kupata amani ya baada ya

mizozo. Hili ni muhimu kwa ufanisi wa juhudi za amani za kusuluhisha mizozo, ikiwa ni pamoja na mikakati ya kina ya upatanishi.

· Ni muhimu pia kuimarisha uwezo wa asasi za umma ili ziweze kutekeleza majukumu yake katika kuwezesha uhusika na ujumuishwaji wa wote mbali na kutimiza majukumu yake kwa umma.

· Janga la COVID-19 limezidisha vyanzo vya ukosefu wa amani na mizozo. Uwajibikiaji janga hili unastahili kuchangia ukuzaji wa uaminifu na kuwezesha majadilino na uhusiano wa washikadau wote.

· Haja ya kuwepo kwa uhusiano uliokitwa katika uaminifu na ruwaza ya kitaifa iliyokitwa katika makubaliano kati ya serikali na jamii ni muhimu. Uongozi unastahili kujengwa katika mshikamano kati ya serikali na jamii, huku ukitoa uwazi, uwezo wa kutabirika na kupunguza hali ya kutoridhika.

· Uongozi unaojali ni muhimu na kuujenga uongozi kama huo kwahitaji serikali zinazoelewa raia wake na zinazozielewa vyema jamii zao na masuala ya ndani kuliko kuwajibikia shinikizo kutoka nje. Serikali zinastahili kuhusisha vikundi vilivyo hatarini, hasa wanawake na vijana, pamoja na wakimbizi, wakimbizi wa ndani kwa ndani na wahamiaji wakati wanapowajibikia COVID-19, ikiwa ni pamoja na kutathmini mahitaji, mfumo wa elimu na mambo mengineyo ili kuhakikisha ufanifu wa uwajibikaji huo.

· Kama COVID-19 ilivyoonyesha, uongozi wa wanawake umekuwa bora zaidi katika kulikabili janga hili kwa kutumia mkabala wa kina na jumuishi. Wacha tuhakikishe kwamba hatua zilizowekwa kulikabili janga hili zitaimarisha mchango ambao wanawake na wasischana wanaweza kutoa katika jamii zao.

· Ningependa kutoa rambirambi zetu kwa walioaga katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 na kutangaza msaada wetu kwa wale wanaojaribu kupata afueni kutoka kwa maradhi haya – kimwili, kifikra, kijamii na kiuchumi.

*Imenukuliwa kutoka kwa hotuba ya kufunga kikao ya Bience Gawanas, Katibu Mkuu Mwandamizi, Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika.