Watu wa asili wapigia chepuo lugha zao wakisema kutoweka kwake ni janga

Get monthly
e-newsletter

Watu wa asili wapigia chepuo lugha zao wakisema kutoweka kwake ni janga

UN News
By: 
Kanen'tó:kon Hemlock, Chifu wa kabila la Kahnawà:ke kutoka jamii ya Mohawk inayopatikana maeneo ya Kaskazini mwa Marekani na Canada, wakati wa tukio lilifanyika New York. Picha: UN Photo/Manuel Elias
Picha: UN Photo/Manuel Elias. Maonyesho ya kitamaduni na wachezaji wa dansi wa Kwakwaka katika tukio la ngazi ya juu cha kuzindua mwaka wa lugha za asili mwaka 2019
Picha: UN Photo/Manuel Elias. Kanen'tó:kon Hemlock, Chifu wa kabila la Kahnawà:ke kutoka jamii ya Mohawk inayopatikana maeneo ya Kaskazini mwa Marekani na Canada, wakati wa tukio lilifanyika New York.

 

 

 

Kufuatia ukweli ya kwamba lugha 600 za kiasili hupotea kila baada ya wiki mbili, Umoja wa Mataifa hii leo kwenye makao yake makuu mjini New York, Marekani umezindua rasmi mwaka wa kimataifa wa lugha hizo.

 

Hotuba ya uzinduzi imetolewa na Kanen'tó:kon Hemlock, Chifu wa kabila la Kahnawà:ke kutoka jamii ya Mohawk inayopatikana maeneo ya Kaskazini mwa Marekani na Canada, ambaye kwa kiasi kikubwa hotuba  yake ilijikita katika kusifia mama dunia.

“Tukiwa watu wa asili, lugha zetu ni lugha za dunia na ni lugha hizo ambazo tunatumia tukizungumza na mama dunia,” amesema akiongeza kuwa “uimara wa lugha zetu umeunganika moja kwa moja na uimara wa ustawi wa dunai yetu, ambayo hivi sasa inatumiwa vibaya.”

Ameenda mbali zaidi akisema  “tunapoteza muunganiko huo na mbinu za wazee wetu za utambuzi wa dunia pindi sauti zetu zinapokuwa kimya. Kwa manufaa ya vizazi vyetu vijavyo lazima tuhakikishe kuwa nao pia wanaweza kuzungumza lugha za mababu zetu.”

Lugha za asili zifundishwe shuleni ili zisipotee- Espinosa

Tukio hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa ambapo fursa iliwadia kwa Rais wa Baraza hilo, María Fernanda Espinosa Garcés kuhutubia ambaye amesisitiza uhusiano wa karibu baina ya lugha za asili, tamaduni za mababu na ufahamu.

Amesema mambo hayo matatu ni zaidi ya mbinu za mawasiliano, ni njia ya kuhamisha ujuzi mmoja kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine.

 “Kila lugha ya asili ina thamani yake ya kipekee kwa binadamu,” amesema Bi. Espinosa akifananisha lugha hizo na hazina iliyosheheni historia, maadili, fasihi, imani, mitazamo, ufahamu, maendeleo yaliyobebwa zaidi ya milenia .

Amewaeleza washiriak kuwa pindi lugha inapotoweka, inachukua kumbukumbu zote ambazo zilikuwemo ndani yake kwa kuwa “lugha za asili ni ishara za utambulisho wa watu, hubeba maadili, mbinu za maisha na maelezo ya kuwaunganisha wahusika na jamii yao na kwamba ni muhimu kwa watu hao waweze kuishi.

“Lugha za asili hufungua milango ya vizazi vya sasa kwa milango ya ufahamu wa mababu kama vile masuala ya kilimo, bailojia, unajimu na dawa. Ijapokuwa bado kuna lugha zaidi ya 4000 za asili duniani, nyingi bado ziko hatarini kutokwe,” amesema Bi. Espinosa.

Kwa mantiki hiyo amesema ni muhimu mwaka huu wa kimataifa wa lugha za asili ni lazima utumike kama jukwaa la kubadili mwelekeo huo wa kutoweka kwa lugha na badala yake zihifadhiwe ikiwemo kwa kuwa na mifumo ya elimu inayopatia kipaumbele matumizi ya lugha za asili.

Lugha za asili zilionekana dhalili wakati wa ukoloni, tuzitunze sasa- Rais Morales

Kwa upande wake, Rais Evo Morales, wa Bolivia aliangazia ustawi wa watu wa asili na lugha zao chini ya mazingira ya ukoloni.

 “Leo hii, tumekuja hapa tukiwa tumehimili zama za ukoloni ambazo zilijaribu kuwafanya viongozi wetu wapige magoti na kuwakandamiza kwa ukosefu wa haki. Natoa wito kwenu mliopo tufanye kazi kupitia mazungmzo ili kuendeleza sera ambazo zitatunza maisha, utambulisho, maadili na tamaduni za watu wa asili,” amesema Morales.

Kwa mujibu wa Morales hivi sasa kuna zaidi ya watu wa asilimi milioni 770 kwenye mataifa 90, wakichangia asilimia 6 tu ya idadi ya watu wote duniani. “Hata hivyo amesema ‘ulafi wa mabeberu’ umewaacha baadhi yao kuwa miongoni mwa asilimia 15 walio hohehahe.”

Ameonya kuwa ulafi huo unafanya watu wa asili kufurushwa kwenye maeneo yao kutokana na rasilimali zilizomo na cha ajabu zaidi, kuna ukimya wa aina yake miongoni mwa viongozi wa dunia katika kubadili hali hiyo.