Watu milioni 24 wanahitaji msaada wa kuokoa maisha Sahel -OCHA

Get monthly
e-newsletter

Watu milioni 24 wanahitaji msaada wa kuokoa maisha Sahel -OCHA

UN News
15 May 2020
By: 
Familia eneo la Kaya jimbo la Sanmatenge nchini Burkina Faso ikipata mlo baada ya kupokea mgao kutoka WFP.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Familia eneo la Kaya jimbo la Sanmatenge nchini Burkina Faso ikipata mlo baada ya kupokea mgao kutoka WFP.

Mashirika manne ya misaada ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s yanayofanya kazi kusaidia ukanda wa Sahel leo yameonya kwamba watu milioni 24, nusu yao wakiwa ni watoto wanahitaji msaada wa kuokoa maisha na ulinzi.

Katika taarifa ya mashirika hayo kuhusu mtazamo wa hali ya kibinadamu  Sahel iliyochapishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA , “idadi hiyo ni sawa na kila mtu mmoja kati ya 5 ya watu wote wa eneo hilo milioni 120 na hii ni idadi kubwa zaidi ya watu wanaohitaji msaada kuwahi kurekodiwa katika eneo la Sahel.”

 

Maeneo yaliyoathirika zaidi katika ukanda huo ni Mali, Niger, Burkina Faso, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, Chad na Kaskazini mwa Cameroon.

Mashirika hayo yanasema mgogoro wa sahel inachochewa na kuzorota kwa hali ya usalama ambayo imesanabisha maelfu ya watu kutawanywa ndani ya nchi zao na nje ya mipaka yao, kuongeza tatizo la njaa, pengo la usawa na athari za moja kwa moja na zilizojificha za janga la virusi vya corona au COVID-19 ikiwemo kuripotiwa kuongezeka kwa visa vya ukatili wa kijinsia.

“Katika ukanda wa Sahel kuna wakimbizi na wakimbizi wa ndani milioni 4.5, watu milioni 12 hawana uhakika wa chakula na watoto milioni 1.6 wana utapiamlo uliokithiri.” Taarifa imeeleza. 

OCHA inasema mipango ya mashirika hayo kwa mwaka huu inalenga kuwafikia watu milioni 17 na inahitaji jumla ya dola bilioni 2.8, na hadi kufikia sasa ni asilimia 18 tu ya fedha hizo ndio zimepatikana. Pia shirika hilo linasema janga la Corona limeongreza gharama ya dola milioni 638.

Fedha hizi ni sehemu ya hatua za kimataifa za kupambana na janga la COVID-19.

Mashirika hayo yametoa onyo hilo wakati msimu wa muambo ukinyemelea na janga la COVID-19 likizidi kushika kasi katika ukanda huo ambao tayari kuna wagonjwa waliothibitishwa 9,000.

Mkuu wa OCHA kanda ya Afrika ya Kati na Magharibi amesema “Endapo hatutochukua hatua sasa mgogoro huu utakatili maishaya watu wengi Zaidi, kuathiri jamii na huenda ukaingia katika kanda zingine nan chi za mwambao wa afrika Magharibi. Mustakbali wa mamilioni ya watu wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka 35 uko njiapanda.”