Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Watu 80,000 waathiriwa na mafuriko makubwa DRC

Get monthly
e-newsletter

Watu 80,000 waathiriwa na mafuriko makubwa DRC

UN News
22 April 2020
By: 
Wakimbizi wa Burundi katika makazi ya Mulongwe huko Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UNHCR/Georgina Goodwin
Wakimbizi wa Burundi katika makazi ya Mulongwe huko Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

 Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Andrej Mahecic hii ameviambia vyombo vya habari mjini Geneva Uswisi kuwa UNHCR inashirikiana na mamlaka pamoja na wadau nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kutoa msaada kwa watu 80,000 ambao wameathiriwa na mafuriko makubwa katika jimbo la Kivu Kusini. 

Msemaji huyo wa UNHCR ameeleza kuwa mvua kubwa katika mji wa Uvira kwenye jimbo la Kivu Kusini  pamoja na maeneo jirani na mji huo, ilinyesha kati ya Alhamis na Jumamosi na kusababisha mafuriko kuyakumba maeneo yaliyo na watu wengi katika mji na vijini vinavyozunguka eneo hilo ambavyo pia vinawahifadhi watu waliofurushwa makwao, wakiwemo wakimbizi.

Taarifa zinaonesha mafuriko yameharibu zaidi ya nyumba 15,000 huku tathimini ikiendelea ingawa tayari ni dhahiri hali hii imeongeza ugumu katika eneo ambalo tayari limeathiriwa na kukosekana kwa usalama na migogoro.

Msemaji wa UNHCR amesema, “hali inayoendelea itaongeza hofu ya wakazi ambao tayari wanakabiliwa na adui mwingine, janga la virusi vya corona.”

Taarifa za awali zimesema zaidi ya watu 25 wamefariki dunia kutokana na mafuriko hayo na zaidi ya watu wengine 40 wamejeruhiwa huku ikihofiwa kuwa wengine wengi huenda wamesombwa na mafuriko. Kiliniki moja katika moja ya viunga vya Uvira kimesambaratishwa na maji na pia maeneo ya kujisafi katika mji ulio na watu wengi nayo yamesambaratishwa. 

UNHCR inaharakisha kupeleka  misaada kutoka katika ghala lake la Uvira yakiwemo mahema kwa ajili ya makazi, magodoro, ndoo na vyandarua. 

“Tutakuwa tunatoa vifaa vya makazi zaidi katika siku zijazo kusaidia kupunguza mateso ya baadhi ya watu ambao nyumba zao zimesambaratishwa. Wakuu wa serikali za mitaa na mkoa wanaongoza majibu kwa msaada kutoka kwa MONUSCO.” Ameeleza Bwana Mahecic

Ingawa hakuna mgonjwa yeyote wa COVID-19 katika eneo la Uvira hadi sasa, hatari ya kipindupindu imeongezeka kutokana na hali ya sasa ya mvua. 

Jimbo la Kivu Kusini pia ni mwenyeji wa wakimbizi kutoka Burundi, kati ya wakimbizi nusu milioni waliko nchini humo.