Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Wanaohoji utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi, waende Ethiopia- Grandi

Watoto wakimbizi kutoka Somalia wakiwa kwenye kambi ya Buramoni nchini Ethiopia. Picha: WFP/Jiro Ose.
Picha: WFP/Jiro Ose. Watoto wakimbizi kutoka Somalia wakiwa kwenye kambi ya Buramoni nchini Ethiopia.

Wanaohoji utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi, waende Ethiopia- Grandi

Akiwa nchini Ethiopia kwa ziara ya siku nne, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi amepongeza serikali kwa uwazi wake na mbinu mpya za kuboresha maisha ya wakimbizi zaidi ya 900,000 na jamii zinazowahifadhi.

Tupo kwenye kambi ya wakimbizi ya Melkadida nchini Ethiopia, iliyoko mpakani na Somalia, ambayo ni makazi ya wakimbizi 200,000 kutoka Somalia, wakionekana wakikwatua mashamba na wengine wakipanda mbegu. Ugeni ni Kamishna Mkuu wa wakimbizi duniani, Filippo Grandi ambaye baada ya kujionea hali halisi anasema..

“Kile kilichofanyika hapa ni mfumo wa kipekee wa wakimbizi kujitegemea ambapo serikali ya Ethiopia imefungua mno milango yake; imekuwa wazi kwenye mipango bunifu vile vile. Jamii mbili, yaani wakimbizi wa kisomali na wenyeji ambao ni waethiopia wameweza kufanya kazi kwa pamoja na kwa amani.”

Kamishna Grandi ametembelea pia mradi wa kuzalisha umeme kwa nguvu za jua, mradi ambao unawezesha eneo hili kame kuwa na ufanisi iwe katika umwagiliaji kwenye kilimo na hata nishati ya umeme.

Kampuni ya kiswidi, IKEA imetoa dola milioni 100 kwenye mradi wa umwagiliaji, nishati na elimu na imetia saini makubaliano ya kufadhili miradi mingine mitatu. Bwana Grandi akafunguka..

“Kwa mara ya kwanza, tunatekeleza mkataba wa kimataifa wa wakimbizi. Watu kila mara wananiuliza, ‘utaanza lini kuutekeleza?’ Naam, tayari tunatekeleza hapa kwa ushirikiano na wadau lukuki kwenye miradi ya umwagiliaji, elimu na mafunzo stadi.”

Kambini pia Bwana Grandi amezungumza pia na wanawake wakimbizi wanaojipatia kipato kwa kufuma vitambaa.

Ethiopia ina historia ndefu ya kuhifadhi wakimbizi na imekuwa ikifungua milango yake kwa kuwapatia huduma za kibinadamu na ulinzi kwa wale wanaosaka hifadhi.