Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Vita isiyo na mipaka yaendelea kuighubika Sahel

Get monthly
e-newsletter

Vita isiyo na mipaka yaendelea kuighubika Sahel

UN News
8 July 2020
By: 
Mwanamke aliyefurushwa Kaskazini mwa Mali ukanda wa Sahel akiwa katika makazi ya muda karibu na kituo cha basi Mopti
UNDP/Nicolas Meulders
Mwanamke aliyefurushwa Kaskazini mwa Mali ukanda wa Sahel akiwa katika makazi ya muda karibu na kituo cha basi Mopti

Licha ya kuzuka kwa janga la corona au COVID-19 ambalo limechangia usitishaji uhasama wa kimataifa katika baadhi ya sehemu, eneo la Sahel mapigano yanaendelea bila kukoma hususan katika nchi za Burkina Faso, Mali na Niger limesema shirikisho la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu ICRC.

Kwa mujibu wa taarifa ya ICRC iliyotolewa leo hali ya usalama na kibinadamu katika jimbo la Liptako Gourma lililo katika viunga vya Burkina Faso na mpakani mwa Mali na Niger ni mbaya sana na inaendelea kuzorota, na mapigano yanacharuka kila uchao ikimaanisha kwamba watu nao wanalazimika kufungasha virago kila wakati kwenda kusaka usalama.

Taarifa hiyo imesema vita sio hatari pekee inayowakabili watu wa Sahel kwani pia wanakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha kutokuwepo kwa uhakika wa chakula na sasa janga la COVID-19 limeongeza zahma  zaidi kwa mamilioni ya watu.

Patrick Youssef Mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa ICRC amesisitiza,  “hatua za haraka zinahitajika ili kuwasaidia watu ambao hali yao ni mbaya sana na kuweka mazingira ambayo yatawezesha kuwepo kwa maendeleo katika ukanda huo.”

Ameongeza kuwa katika eneo la Sahel vita, uhaba wa chakula, uwepo wa uongozi dhaifu au kutokuwepo kwa uongozi kabisa na mgogoro wa kiuchumi vimesababisha watu zaidi ya milioni moja kutawanywa huku wengine wakiamua kujiunga na makundi ya wapiganaji.

Taarifa hiyo ya ICRC inasema "vita hii isivyo na mipaka Sahel imezifanya familia nyingi kufurushwa zaidi ya mara moja na hofu kubwa iliyopo sasa ni kushindwa kubadili hali hiyo tete ambayo inafanya maisha ya mamilioni ya watu kuwa hatarini kila wakati."

Kwa mantiki hiyo ICRC inasema “hatua za kibinadamu ndio njia pekee ya kuwasaidia waliotawanywa na mgogoro wa Sahel lakini hatutaweza kumudu mahitaji yao yote sisi peke yetu. Suluhu ya kiusalama pekee haitoshi kuna haja ya kuchagiza maendeleo ili kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Sahel.