Utalii barani Afrika: Safari za mitandaoni zaanza huku mataifa yakijiandaa kuwapokea tena watalii

Get monthly
e-newsletter

Utalii barani Afrika: Safari za mitandaoni zaanza huku mataifa yakijiandaa kuwapokea tena watalii

Afrika Upya: 
26 August 2020
Zebra na twiga tatu

Huku mamilioni ya nafasi za ajira zikiwa zimepotea kutokana na janga la COVID-19, sekta ya usafiri na utalii barani Afrika inatumia ubunifu na kutafuta usaidizi ili kuinuka tena

Kundi kubwa la pundamilia linatembea katika nyika pana. Baada ya muda mfupi, wanasimama ili kula nyasi na hivyo kuwafanya swalapala wakimbie na wanatorokea upande wa kaskazini. Karibu katika Hifadhi ya Wanyama ya Sabi Sand iliyo Mpumalanga na ambayo inasemekana kuwa mojawapo ya maeneo bora ya utalii Afrika Kusini.

Umbali wa kilomita chache katika Hifadhi ya Madikwe, kuro na swara wanakata kiu katika kidimbwi cha maji. Ndege wanaimba katika kichaka kilicho karibu huku wakisubiri zamu yao. Hali ni tulivu hadi kundi la ndovu watatu wanapoibuka ghafla kutoka katika kichaka wakielekea kidimbwini.

Mandhari haya yanaonekana na kusikika halisi, ilhali yote yako mtandaoni. Hapana watalii hapa, wakiwa na au bila ya barakoa. Kwa hakika, Afrika Kusini na mataifa mengine ya Afrika yaliyo maarufu kwa watalii yalifunga mipaka yao COVID-19 ilipozuka.

Huku wakiwa na mbuga na hoteli bila wateja, waandalizi wa safari wa Afrika wanapiga hatua kidijitali kuhudumia mamilioni ya watu waliosalia majumbani mwao ulimwenguni kote. Kwa majuma kadhaa sasa, maelfu ya wapenzi wa safari za mitandaoni wamethamini uzuri wa wanayamapori wa Afrika, fuo za bahari na maeneo mengine ya watalii mitandaoni.

Nchini Kenya, Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Najib Balala, mwezi wa Juni 2020 alizindua kampeni ya utalii wa kupeperushwa moja kwa moja mitandaoni kutangaza safari za wanyamapori kama sehemu ya kampeni inayoendelea ya #MagicAwaits ikiongozwa na Bodi ya Utalii ya Kenya inayolenga kuhakikisha kwamba ulimwengu wote na hasa  watalii, wanaendelea kuunganishwa na Kenya hata katika kipindi hiki cha kusalia majumbani cha Covid-19 ambapo kutembea kumedhibitiwa kimataifa.

Akizungumza alipokuwa akizindua utalii huo wa mtandaoni katika Mbuga ya Wanyama ya Nairobi, Bwana Balala alieleza kwamba janga la COVID-19 limewafundisha wadau katika sekta mbalimbali kuwa wabunifu zaidi ili kuhifadhi biashara zao wakati huu mgumu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Utalii ya Kenya Betty Radier, aliambia AfrikaUpya kwamba safari za mitandaoni zingehakikisha kuwa walimwengu wameunganishwa na maeneo ya utalii katika kipindi hiki.

Mikakati yetu ya kutangaza itaendelea kurekebika kulingana na hali za sasa zibadilikazo kila mara. Kwa sasa tunaendeleza kampeni kuhakikisha kwamba Kenya inasalia chaguo la msafiri wa hapa nyumbani na wa kimataifa sasa na baada ya COVID-19.

“Unaweza kufuatilia mitandao yetu ya kijamii ‘Magical Kenya’ ili kupeperusha video za safari na vivutio vingine mbashara. Tunataka kuifanya ari ya wateja katika maeneo haya kusalia juu,” alisema Bi. Radier.

Kumbi zetu za mitandao ya kijamii zinatoa njia mbalimbali kwa watumizi kutagusana na safari, ikiwa ni pamoja na kuweza kuuliza maswali na nafasi ya kuitalii Kenya katika mtandao.

“Mikakati yetu ya kutangaza itaendelea kurekebika kulingana na hali za sasa zibadilikazo kila mara. Kwa sasa tunaendeleza kampeni kuhakikisha kwamba Kenya inasalia chaguo la msafiri wa hapa nyumbani na wa kimataifa sasa na baada ya COVID-19,” alisema Bi. Radier

Janga la COVID-19 lilisitisha utalii kimataifa. Maeneo yote ya Shirika la Dunia la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) yameshuhudia kufungwa kwa zaidi ya 65% ya vivutio vyao vya utalii: Afrika (74%), eneo la Marekani (86%), Asia na eneo la Pacific (67%), Uropa (74%) na Mashariki ya Kati (69%). Shirika hilo linatabiri didimio la 20-30% la watalii wa kimataifa mwaka huu.

Kabla ya COVID-19,  Afrika ilichukua nafasi ya pili katika kasi ya ukuaji wa utalii. Kwa mfano mnamo 2018, watalii wa kimataifa milioni 67 walizuru mataifa ya Afrika, na kuzalisha dola za Marekani bilioni 38 kwa bara hili, kulingana na UNWTO. Ongezeko la 4.2% la watalii lilishuhudiwa mwaka 2019 na 3-5% lilikuwa limetabiriwa kwa mwaka 2020.

Janga hili pamoja na hatua za kulidhibiti limeathiri pakubwa sekta ya usafiri na utalii Afrika. Kulingana na Baraza la Dunia la Usafiri na Utalii (WTTC) takribani nafasi za ajira za usafiri na utalii milioni nane zimepotea katika bara Afrika pekee kwa sababu ya COVID-19.  Hali hii, pamoja na kupotea kwa mapato, kulichochea wito wa kimataifa kuiokoa sekta hii kutoka kwa mashirika ya uchukuzi wa angani na utalii mwezi wa Mei.

Muungano wa Kimataifa wa Uchukuzi wa Angani (IATA), UNWTO, WTCC, Muungano wa Mashirika ya Ndege ya Afrika (AFRAA) na Muungano wa Mashirika ya Ndege ya Kusini mwa Afrika (AASA) iliomba dola bilioni 10 kutoka kwa mashirika ya kifedha ya kimataifa, washirika wa maendeleo wa mataifa na wafadhili wa kimataifa kama msaada wa kuisadia sekta ya usafiri na utalii na kulinda ajira.

Baadhi ya mataifa yaliyoathirika ni Côte d’Ivoire na Zimbabwe, Kenya, Morocco, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, ambazo chumi zao hunufaika pakubwa sana kutokana na utalii. Maeneo mengine maarufu kama  Botswana, Cape Verde na Rwanda, Misri, Uhabeshi, Mauritius, Namibia, Ushelisheli na Gambia pia yameathirika.

Kujitoa katika hatari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alitoa ujumbe wa video kimataifa mwezi Juni akiuunga mkono utalii na nafasi yake, kwa kusema, “Utalii waweza kuwa jukwaa la kulishinda janga hili. Kwa kuwaleta watu pamoja, utalii waweza kuimarisha mshikamano na uaminifu – viambata muhimu katika kuendeleza ushirikiano wa kimataifa unaohitajika sana sasa.”

Mataifa yanapoanza kulegeza vikwazo vya usafiri vya COVID-19, baadhi yanaweka mipango kufungua sekta zao za utalii, iwapo hayajafungua tayari.

Tanzania inawakaribisha watalii, ilhali Namibia imefungua tena mbuga zake za wanyama. Morocco ilitangaza mipango ya kufungua Julai, na Afrika Kusini inatarajia kuwakaribisha watalii kufikia Septemba 2020. Uganda na Mauritius zaweza kusubiri kidogo zaidi.

Kenya na Zambia zinatumia fursa hii kuendeleza utalii wa nyumbani huku zikisubiri kuondolewa kwa vikwazo vya usafiri katika majuma yajayo kwa kuzingatia miongozo na kanuni zitolewazo na wataalamu.

Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololikashvili anasema kuondolewa kwa vikwazo vya usafiri kwa wakati mwafaka kutasaidia kurejesha manufaa mengi ya kijamii na kiuchumi ya utalii kwa njia endelevu.

Hata hivyo, licha ya matumaini ya kufunguliwa kwa utalii, Mkuu huyo wa UNWTO ametoa wito kwa kanuni na taratibu zilizoshirikishwa kati ya mataifa, sekta ya kibinafsi, na jamii kuhusu usimamizi mipakani, uchukuzi wa angani, sekta ya ukarimu, mashirika ya usafiri, shughuli na vivutio.

“Kwa hivyo, ni muhimu, kwamba kufunguliwa upya kwa utalii kupewa kipaumbele na kusimamiwa kwa njia ya uwajibikaji, kuwalinda walio katika hatari zaidi na afya na usalama ukizingatiwa sana katika sekta hii.

Huku UNWTO ikisisitiza haja ya uangalifu, uwajibikaji na ushirikiano wa kimataifa ulimwengu unapofungua tena taratibu, shirika hilo limeahidi kusidia Afrika kukua tena kwa njia thabiti na bora na kwa utalii kuibuka katika janga hili kama nguzo muhimu kwa chumi, nafasi za ajira na uendelevu.

Mapema Juni 2020, mawaziri wa utalii kutoka Afrika na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na sekta ya kibinafsi walikutana kwa njia ya mtandao kuweka mwongozo wa pamoja kuhusu sekta thabiti na bora ya utalii. Karibu washiriki 140 kutoka kwa mataifa 30, pamoja na mawaziri 24 walijadili changamoto ya sasa inayoletwa na COVID-19, ukombozi na unyumbufu. Aidha walijadili maeneo muhimu ya Ajenda UNWTO kwa Afrika, mkakati unaokusudia kuongoza sekta hiyo katika ukuaji endelevu.

Kabla ya mkutano huo, mataifa wanachama yalishiriki katika uchunguzi mtandaoni ambapo yaliaalikwa kutoa maoni yao kuhusu namna Ajenda ya UNWTO kwa Afrika inavyoweza kutumiwa kuongeza kasi ya ujenzi upya kutokana na athari za janga la COVID-19 na kuweka unyumbufu kwa  manufaa ya siku za usoni.

Uchunguzi huu ulidhihirisha maeneo matano makuu ambako Mataifa Wanachama ya Afrika yangependa kuyapa kipaumbele ili kuyasaidia vyema yanapojikomboa kutoka kwa athari za COVID-19. Maeneo hayo yanajumuisha:

Kufungulia ukuaji kwa kuwezesha uwekezaji na ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi;

Kuwezesha ubunifu na teknolojia; Kuwezesha usafiri, pamoja na kuunganishwa kulikoimarishwa na sera za visa za utalii; Kuimarisha unyumbufu, pamoja na kuwezesha juhudi za usalama na ulinzi na mawasiliano katika hali ya hatari; na Kupigania “Brand Africa”

Bw. Pololikashvili anasema kuwa majibu haya kutoka kwa Mataifa yetu Wanachama ya Afrika yatasaidia UNWTO kuiongoza biashara utalii katika miezi ijayo yenye changamoto.

Mada: