Tunaweza kufanya lolote iwapo tu majasiri- Profesa Bande

Get monthly
e-newsletter

Tunaweza kufanya lolote iwapo tu majasiri- Profesa Bande

UN News
25 September 2019
By: 
Tijjani Muhammad-Bande (centre), President of the seventy-fourth session of the United Nations General Assembly, opens the general debate of the seventy-fourth session of the General Assembly.
UN /Kim Haughton
Ufunguzi wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Profesa Tijjani Muhammad-Bande amerejea tena kauli yake ya kusihi ushirikiano wa kimataifa ili kuweza kunasua mamilioni ya watu kutoka lindi la umaskini.

Akifungua mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani, Profesa Bande amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa utokomezaji umaskini unasalia changamoto kubwa inayokumba dunia hivi sasa.

“Ingawa mataifa mengi  yamefanikiwa kunusuru mamilioni ya watu wao kutoka kwenye umaskini, tunapaswa kuchukua hatua zaidi kuwanusuru mamilioni zaidi kutoka kwenye umaskini uliokithiri, machungu na mazingira duni,” amesema Bande ambaye pia ana wadhifa wa ubalozi.

Rais huyo wa Baraza Kuu amesihi nchi hizo wanachama wa Umoja wa Mataifa vile vile kuangalia ni vipi zinaweza kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii ili hatimaye serikali iweze kuelekeza fedha kwenye mifuko hiyo na iwe na manufaa kwa hohehahe.

Halikadhalika amesema, “nchi zinapaswa kushirikiana katika kuendeleza uwezo wa kijasiriamali na kuboresha sekta ya kilimo.”

Mabadiliko ya tabianchi na umaskini

Akihusisha mabadiliko ya tabianchi na umaskini na ukosefu wa chakula, Balozi Bande amesema, “tunahitaji mwelekeo makini zaidi katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi; kwa kuwa madhara ya kutochukua hatua yanaleta madhara makubwa sasa na kwa vizazi vijavyo.”

Amekumbusha kuwa madhara hayo ni dhahiri kifedha na kibinadamu yakiwekwa bayana na majanga kama vile vimbunga, ukame, mioto ya nyika duniani kote.

“Hebu na tutumie maarifa na teknolojia tulizo nazo ili tuhakikishe kuwa hatuwatumbukizi watoto wetu kwenye dunia ambayo haiwezi kurekebishika,” amesema Balozi Bande.

Tunaweza kufanya lolote iwapo tu majasiri

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema licha ya changamoto kubwa bado kuna ushadi kuwa, “tunaweza kufanya mambo makubwa iwapo tuna ujasiri, tunachukua hatua haraka na kuonesha huruma. Kuanzia Mahatma Ghandi aliyeongoza kampeni ya uhuru wa India hadi kwa binti mdogo Greta Thunberg anayeongoza hatua kwa tabianchi: kuanzia Nelson Mandela aliyesimama kidete kupinga ubaguzi wa rangi hadi mwa Malala Yousafzai ambaye licha ya yote amesisitizia elimu kwa mtoto wa kike.”

Kwa mantiki hiyo amekumbusha wajumbe kuwa ingawa wamo kwenye ukumbi maridadi kujadili jinsi ya kufanikisha ndoto yao ya pamoja, ana uhakika kuwa katika vikao vytoe na hadi mwisho watapatia kipaumbele matumaini ya wakazi wa dunia akihitimisha kuwa, ”lazima tujitahidi pamoja kuwahudumia watu wote.”

Mada: