Nzige wakizidi kutotoa mayai yao Ethiopia, wakulima waomba msaada, FAO halikadhalika

Get monthly
e-newsletter

Nzige wakizidi kutotoa mayai yao Ethiopia, wakulima waomba msaada, FAO halikadhalika

UN News
27 February 2020
By: 
Nzige wanaweza kuharibu mazao na nyasi za mifugo
FAO/Giampiero Diana
Nzige wanaweza kuharibu mazao na nyasi za mifugo

Msimu wa upanzi  ukianza nchini Ethiopia, serikali nayo inahaha kudhibiti kuenea kwa nzige wavamizi wa jangwani  huku wakulima nao wakilalama vile ambavyo wadudu hao waharibifu wanaleta hofu na shaka kubwa hivi sasa.

Miongoni mwao ni Awuno Menka, mkulima mwenye umri wa miaka 60 na mkazi wa kijiji cha Dereba, kwenye ukanda Gamugofa eneo la SNNP ambaye ameshuhudia uharibifu mkubwa uliofanywa na wadudu hao.

“Makundi mawili ya nzige yalivamia eneo letu na kuharibu mazao yote ya mahindi. Ijapokuwa baadaye waliweza kudhibitiwa, bado makundi zaidi yanawasili kutoka Kenya. Nina hofu na msimu wa sasa wa upanzi,”  amesema Menka hoja ambayo inaungwa pia na mkulima mwingine Argueta Belachew.

Belachew, mwenye umri wa miaka 45 anasema kuwa “katika siku tatu pekee, nzige hawa wamekuwa wakitotoa mayai  yao, na wanakula mioto ya kijani. Tunatoa wito wa kusaidiwa kuwadhibiti.”

Akizungumzia hali hiyo, Mwakilishi wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO nchini Ethiopia, Fatouma Seid amesema kuwa “tupo katika hatua muhimu sana ambapo tunahitaji kuhifadhi mavuno yajayo na yatakayofuata na kulinda mbinu za kujipatia kipato kwa wananchi hawa.”

Mambo 7 unayopaswa kuyafahamu kuhusu nzige

Pengo la fedha za kudhibiti nzige laongezeka

Hadi sasa FAO imepokea dola milioni 6.5 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF, Serikali  ya Marekani, Saudi Arabia na Ubelgiji kwa ajili ya operesheni za kutokomeza nzige hao.

Mazungumzo yanaendelea ili kupata dola milioni nyingine 10 wakati huu ambapo FAO imeomba dola milioni 138 ikiwa nyongeza kwa takribani asilimia 50 kutoka ombi la mwezi mmoja uliopita.

Fedha hizo zinalenga kusaidia mataifa 8 ya Mashariki mwa Afrika yaliyoathiriwa na nzige ambapo dola milioni 50.5 kati ya hizo ni kwa ajili ya Ethiopia.

Bi. Seid ameshukuru kwa mchango uliokwishatolewa huku akisihi wahisani wajitokeze zaidi akisema kuwa, “iwapo  hatuchukui hatua haraka, mahitaji ya rasilimali yataongezeka na itakuwa vigum uzaidi na gharama kudhibiti hali ilivyo.”