Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Nimeongeza uzalishaji sabuni, nikapunguza bei, ili kupambana na COVID-19 -Havyarimana

Get monthly
e-newsletter

Nimeongeza uzalishaji sabuni, nikapunguza bei, ili kupambana na COVID-19 -Havyarimana

UN News
15 May 2020
By: 
Pichani iliyopigwa kutoka angani inaonyesha sehemu ya makazi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya
Picha/Siegfried Modola
Pichani iliyopigwa kutoka angani inaonyesha sehemu ya makazi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya

Ili kusaidia kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona, mkimbizi kutoka Burundi, Innocent Havyarimana anayeishi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya na ambaye kwa miaka mitano amekuwa akijihusisha na utengenezaji wa sabuni za maji, hivi sasa ameongeza uzalishaji na kupunguza bei ya sabuni ili watu wengi waweze kunawa mikono yao.

Ni katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyoanzishwa mwaka 1992 kaskazini magharibi mwa Kenya, Innocent Havyarimana mkimbizi kutoka Burundi anaonekana akikoroga mchanganyiko ambao unaanza kukolea rangi ya waridi au pinki, katika kuelekea kutengeneza sabuni ya maji. 

Havyarimana anasema watu wengi sasa wako katika uhitaji mkubwa wa sabuni, “kwa sababu ya virusi vya corona, uzalishaji sabuni umeongezeka sana kwa kuwa hivi sasa kila mtu yuko katika uhitaji wa sabuni.” 

Innocent Havyarimana akishirikiana na mfanyakazi wake, wanaendelea kukoroga mchanganyiko wa sabuni huku wakipima uzito wa kimiminika katika kutafuta ulaini wanaoutaka. Bwana Havyarimana anasema,“kwa upande wangu kama mtengenezaji wa sabuni, kwanza niliamua kuweka bei ndogo ili kila mmoja aweze kuimudu sabuni.”

Sasa ni wakati wa kuijaza sabuni katika chupa za ujazo tofautitofauti. Kwa muonekano, sabuni za Havyarimana hazina tofauti na sabuni zinazozalishwa katika viwanda vikubwa.Bwana Havyarimana anaeleza kuwa virusi vya corona vimeleta mwelekeo mpya wa biashara yake,“hivi sasa, kwa sababu ya virusi vya corona, mahitaji ambayo ni makubwa ni sabuni za kunawa mikono, vitakasa mikono na sabuni zile za matumizi ya kila aina.”

Sasa sabuni inaonekana iko tayari kwa matumizi na Bwana Havyarimana anaonesha alivyoweka karatasi za utambulisho katika chupa. Anasema sabuni iko tayari kwa matumizi na soko lake la kwanza ni wakimbizi wenzake kambini Kakuma,“virusi vya corona vimeiathiri dunia ikiwemo Kambi ya wakimbizi ya Kakuma. Wakimbizi wengi wanaviogopa sana virusi hivi vya corona ndiyo maana huwezi kukuta zaidi ya watu watatu katika eneo moja.”

Kwa mkimbizi huyu kutoka Burundi, kila kukamilika kwa mzunguko mmoja wa utengenezaji sabuni, ni kuanza kwa mchakato wa mzunguko mpya. Na sasa yuko katika bustani yake ndogo akivuna mmea wa shubiri au Aloe Vera, tayari kutengeneza sabuni nyingine.