Misingi ya UN itaunganisha ulimwenguni kinachoendelea kwenye kuta za ofisi yangu -Bozkir

Get monthly
e-newsletter

Misingi ya UN itaunganisha ulimwenguni kinachoendelea kwenye kuta za ofisi yangu -Bozkir

UN News
23 June 2020
By: 
Rais mteule wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, Volkan Bozkir (kushoto) katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa UN António Guterres katika picha hii ya pamoja ya Januari 2020.
UN/Manuel Elias
Rais mteule wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, Volkan Bozkir (kushoto) katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa UN António Guterres katika picha hii ya pamoja ya Januari 2020.

Rais mteule wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Volkan Bozkir amesema chombo hicho kikiwa ni Bunge la Dunia kina uwezo wa kipekee wa kusongesha jitihada za kimataifa wakati huu wa changamoto za kidunia ikiwemi majanga ya kibinadamu, mizozo na ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID 19.

Akihutubia Baraza hilo kwa njia ya video wakati wa kikao kisicho rasmi kufuatia kuchaguliwa kwake wiki iliyopita kuongoza mkutano wa 75 wa Baraza hilo, Bwana Bozkir amesema kuwa ni kwa kuzingatia jukumu  hilo ataongoza chombo hicho kwa maslahi ya nchi zote wanachama.

Amegusia umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, akiongeza kwa, “juhudi zangu zitakuwa kuongezea katika ajenda na vipaumbele vya Guterres.”

Bozkir anakuwa raia wa kwanza kutoka Uturiki kuchaguliwa kuongoza Baraza hilo la Umoja wa Mataifa.Uchaguzi wake ulifanyika tarehe 17 mwezi huu wa Juni kwa kura ya siri iliyopitwa bila kufanyika kwa kikao cha wazi kutokana na janga la Corona.

Akizungumza COVID-19, Rais huyo mteule wa Baraza Kuu amesema kuwa “ni changamoto kubwa ya kwanza kiafya na kibinadamu lakini pia ni tishio likiwa na madhara kiuchumi, kisiasa na kijamii na katika haki za binadamu. Kutokana na changamoto za COVID-19, kuzingatia Katiba ya Umoja wa Mataifa na kurejesha imani ya watu kwenye taasisi za kimataifa na Umoja wa Mataifa ukiwa ni kitovu, ni jambo muhimu sana.”

Ameongeza kuwa atatumia mamlaka za kimaadili na mamlaka ya Rais wa Baraza  Kuu akisisitiza kuwa, “misingi ya uongozi wakati wa kipindi chake ni kutoegemea upande wowote, ufanisi, uwazi, na kutokuwepo kwa ubaguzi. Wakati wa uongozi wangu, misingi mikuu ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amani, usalama na maendeleo endelevu na haki za binadamu vitapatiwa kipaumbele sawa kutoka ofisini kwangu kama njia ya kutambua uhusiano wake na ulimwengu ulioko nje ya kuta hizi.”

Amesisitiza kuwa katika hatua za pamoja dhidi ya janga la Corona, lazima kuzingatia mahitaji muhimu ya wale walio hatarini zaidi kwa kuangazia misingi hiyo ya Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa, “lazima tujenge upya vyema zaidi na kutambua kuwa hakuna mtu aliye salama hadi pale kila mtu yuko salama.”

Wiki hii ni miaka 75 tangu kutiwa saini mkataba wa kuanzia UN - Profesa Muhammad-Bande

Naye Rais wa sasa wa Baraza hilo Profesa Tijjani Muhammad-Bande amesema kuwa wiki hii ni miaka 75 tangu kutiwa saini kwa mkataba ulioanzisha Umoja wa Mataifa, “wakati huu unatukumbusha tunahitaji kuweka upya ahadi yetu ya ushirikiano wa kimataifa kama binadamu, dunia moja na Umoja wa Mataifa.”

Amekumbusha kuwa dunia baada ya janga la Corona itahitaji hatua za dharura za kutoa hakikisho la kujenga jamii bora zaidi akisema kuwa “nimetiwa moyo na ahadi ya Rais-mteule wa Baraza hili la kuchagiza upya azma ya Baraza hili kuhusu ushirikiano wa kimataifa na hatua zake jumuishi katika kuhakikisha ushiriki wa wanachama wote wa Umoja wa Mataifa na wadau husika.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumzia kipindi cha Rais- mteule Bozkir amesema, “ataongoza wakati wa kipindi cha mwaka muhimu katika uhai wa shirika hili. Amesema kipaumbele ni kuendeleza hatua mbali mbali za Umoja wa Mataifa dhidi ya COVID-19 na kuongeza kuwa Baraza Kuu linapaswa kushughulikia changamoto zote za dunia kuanzia mabadiliko ya tabianchi hadi haki za binadamu, kuanzia usawa wa kijinsia na juhudi zetu za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”