Makazi ya wakimbizi Niger yashambuliwa, sasa wasaka hifadhi kwingineko

Get monthly
e-newsletter

Makazi ya wakimbizi Niger yashambuliwa, sasa wasaka hifadhi kwingineko

UN News
3 June 2020
By: 
Nchini Niger, watot milioni 1.6 waliohatarini wanathiriwa na changamoto na mizozo ya kibinadamu, pamoja na kufungwa kwa mipaka ili kuzuia kuenea kwa COVID-19.
UNICEF/Juan Haro
Nchini Niger, watot milioni 1.6 waliohatarini wanathiriwa na changamoto na mizozo ya kibinadamu, pamoja na kufungwa kwa mipaka ili kuzuia kuenea kwa COVID-19.

Watu 1,100 wakiwemo raia wa Niger na wakimbizi kutoka Mali wamewasili kwenye mji wa Telemces wakisaka hifadhi baada ya kufurumushwa na mashambulizi ya jumapili mchana kwenye mkoa wa Tahoua ulioko mpakani mwa Niger na Mali.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema kuwa zaidi ya watu 50 waliokuwa wakiendesha pikipiki huku wamebeba silaha walivamia eneo hilo la Intikane kwenye mkoa wa Tahoua nchini Niger, lililopo kilometa 72 kutoka mpaka wa nchi hiyo na Mali ambapo pamoja na kuua watu watatu, walichoma moto mali za watu hao na bidhaa za misaada.

 Msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video amesema kuwa, eneo hilo ni makazi ya wakimbizi 20,000 kutoka Mali na wakimbizi wa ndani 15,000 wa Niger.

 Bwana Mahecic amesema, “watu hao pia walichoma moto minara ya mawasiliano ya simu na kituo kikuu cha kusambaza maji na hivyo kusababisha eneo hilo kukosa siyo tu mawasiliano bali pia huduma ya maji.”

 Hivi sasa watu hao 1,100 waliowasili mjini Telemces, takribani kilometa 27 kutoka eneo lililoshambuliwa wanahitaji maji, chakula na misaada mingine muhimu ambapo mamlaka za eneo hilo na wadau wanawapokea na kuwasajili.

 UNHCR inasema kuwa, mashambulizi ya kikatili kama lile la jumapili limeshtua wakimbizi, wenyeji wanaowahifadhi na wafanyakazi wa kibinadamu na hofu ni kwamba, kuna uwezekano wa mashambulizi zaidi na hivyo watu wengine wanakimbilia maeneo ya ndani zaidi ya Niger.

 Shirika hilo pamoja na kulaani shambulizi hili la karibuni zaidi, linatoa wito kwa pande zote husika kuheshimu maisha ya raia na wahusika wa tukio hilo wafikishwe mbele ya sheria