Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Kwa utayari wa kisiasa na uwekezaji, bara la Afrika linaweza kujizatiti kupata chanjo yake ya COVID-19

Get monthly
e-newsletter

Kwa utayari wa kisiasa na uwekezaji, bara la Afrika linaweza kujizatiti kupata chanjo yake ya COVID-19

Afrika inawakilisha asilimia 26 ya idadi ya watu wote duniani lakini ina chini ya asilimia 0.1 ya uzalishaji wa chanjo duniani
Afrika Upya: 
26 March 2021
There are fewer than 10 African manufacturers with vaccine production and are based in five countries: Egypt, Morocco, Senegal, South Africa and Tunisia.
WHO
Kuna wazalishaji chini ya 10 wa Kiafrika walio na uzalishaji wa chanjo na wako katika nchi tano: Misri, Moroko, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia.

Afrika ina uwezo wa kuzalisha chanjo zake za virusi vya korona lakini utayari wa kisiasa na miundombinu ya uwekezaji inahitajika ili kusadia kufadhili sindano zinazookoa maisha na kukomesha janga hili, wataalamu wanahimiza.

Wakizungumza katika mjadala wa jopo la ngazi ya juu la Tume ya Kiuchumi ya Afrika (ECA) kama Afrika iko tayari kufadhili chanjo zake yenyewe, wataalamu wanaoongoza walihisi kwamba Afrika ilihitaji nia thabiti zaidi ya kisiasa na miundombinu ili kuzindua chanjo zake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliliambia jopo hilo kwamba utengenezaji wa chanjo kwa wakati unaofaa katika kupambana na COVID-19 uliipa dunia sababu ya kuwa na matumaini lakini matumaini hayo yanapaswa kuwa ya wote.

"Hakuna nchi inayoweza kutoa chanjo kwa watu wake tu na kuepukana na janga hili, hata nchi tajiri haziwezi, "Dkt. Ghebreyesus alisisitiza, akionya kwamba ilimradi virusi hivyo vinasambaa, vinaendelea kubadilika. Usambazaji wa chanjo kwa usawa ndiyo njia ya uhakika ya kulikomesha.

"Hata pamoja na chanjo hizo, bado tuna safari ndefu," alisema, huku akionya kwamba COVID-19 imeharibu uchumi, imevuruga biashara, usafiri na utalii, huku ikiacha nchi za Afrika ambazo zinategemea kuingiza bidhaa kutoka mabara ya nje katika hatari.

Akiitaja Benki ya Dunia, Dkt. Ghebreyesus alisema kwamba kwa kila mwezi ambao chanjo ilichelewa kufika Afrika, bara hili lilipoteza dola bilioni $13.8 katika GDP.

"Njia ya haraka ya kurejesha uchumi ni kutoa chanjo kwa usawa," Dkt. Ghebreyesus alisema, akiongeza kwamba, "Hatimaye Afrika inahitaji kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji yake yenyewe ya chanjo na bidhaa nyingine za muhimu. Hii inamaanisha uwezo wa kufadhili utengenezaji bidhaa za ndani, kanuni madhubuti na usambazaji wa bidhaa kwa njia endelevu."

Kushiriki ujuzi na Afrika

Dkt. Ghebreyesus alisema kwamba viwango vya uzalishaji wa chanjo vinapaswa kuongezwa katika nchi ambazo zinazalishwa na kampuni za dawa zinaombwa kuipatia Afrika haki za hati miliki, data na ujuzi kuhusu utengenezaji wa chanjo.

WHO imeunda Kitovu cha Ufikiaji wa Teknolojia (CTAP) kuhusu COVID ili kuharakisha utengenezaji wa bidhaa, ikiwemo chanjo za kupambana na COVID-19.

Janga hili limedhihirisha upungufu muhimu katika utengenezaji wa chanjo barani Afrika ambao unawakilisha asilimia 26 ya watu duniani lakini una chini ya asilimia 0.1 ya uzalishaji wa chanjo duniani.

"Hatimaye, mambo ambayo tunaweza kujifunza kutokana na janga hili ni kwamba afya si jambo la fahari lakini ni haki ya kimsingi ya binadamu na ndiyo msingi wa utulivu wa kijamii na kisiasa," alisema mkuu huyo wa WHO.

Hitaji la kuridhia Shirika la Dawa la Afrika (AMA)

Dr. Ghebreyesus alitoa wito kwa nchi za Afrika kuridhia mkataba wa kuunda Shirika la Dawa la Afrika (AMA) ili kudhibiti utengenezaji wa bidhaa za kimatibabu barani, pamoja na kuunga mkono pendekezo la Afrika Kusini na India la utoaji msamaha wa kutumia Hakimiliki ya Mali ya Akili katika Shirika la Biashara Ulimwenguni.

"Tuna mwaka mmoja na hili janga la dunia na ubaguzi wa chanjo unafanyika huku tukishuhudia," aliomboleza Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa kuhusu HIV/AIDS (UNAIDS).

Alisema kwamba tayari mwaka umepita, lakini hakuna mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kila mtu anapata chanjo ya COVID-19 na kukomesha janga hili, wakati miaka 25 iliyopita, ulimwengu ulichukua hatua ya kukomesha HIV/AIDS.

"Nchi tajiri zimetoa chanjo kwa watu kwa kiwango cha mtu mmoja kwa kila sekunde wakati nchi nyingi zinazoendelea hazijatoa hata dozi moja. Mpaka wiki iliyopita, chini ya asilimia 1 ya Waafrika walikuwa wamepata chanjo na wengi wao walikuwa katika nchi moja."

Bi. Byanyima alisikitika kwamba nia ya Afrika ya kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya watu wake ili kupata kinga haikushughulikiwa katika kiwango cha kimataifa.

Nchi tajiri na kampuni kubwa za dawa hazikushiriki kutoa ujuzi kuhusu chanjo huku nchi za Afrika zikilipia mara mbili ya bei kuliko nchi tajiri kwa ajili ya chanjo.

Akijibu maswali kuhusu kutumia pamoja hakimiliki ya mali ya akili, Susan Silbermann, Kiongozi wa Jopo Kazi la Kimataifa la COVID-19 na Rais wa Chanjo za Pfizer, alisema kwamba Pfizer ilikuwa tayari kufanya kazi na Afrika. Imebainisha mpango wa kushiriki ujuzi, data na zana kwa umma kuhusu utengenezaji wa dawa na katika uwezo wa utengenezaji.

"Kuna maswali mengi kuhusu hakimiliki ya mali ya akili, kuhusu uwezo wa kutengeneza, kuhusu kujenga vituo,"Bi. Silbermann alieleza.

"Vitu hivi huchukua muda. Hakuna fimbo ya miujiza, hakuna upigaji wa kidole. Hakuna hundi kubwa inayoweza kuandikwa ili kuruhusu mtu yeyote mahali popote duniani kufanya aina ya utengenezaji unaohitajika kwa chanjo kama zile ambazo Pfizer imetengeneza."

Stavros Nocolaou, Afisa wa ngazi ya juu anayeshughulikia Biashara ya Kimkakati katika kampuni ya dawa ya kimataifa, Aspen, alisema kwamba mpango bora wa urejeshaji wa uchumi kwa nchi yoyote ulikuwa ni kutoa chanjo kwa wengi ili ipatikane kinga inayotakiwa.

Alitoa wito wa kuwa na mpango wa muda mrefu wa kuwekeza katika kukuza uwezo na ujuzi. Kuu katika suala hili ni kutambua nguvu zake na kuchagua washirika sahihi ili kuanza kutumia rasilimali na maarifa yaliyopo.

Afrika iko tayari kuzalisha chanjo kwa sababu imeshazalisha chanjo kwa magonjwa mengine, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Afrika CDC), Dkt. John Nkengasong alisema.

Tunafahamu kwamba chanjo ndio nguzo muhimu katika usalama wa afya barani na tumewekeza katika hilo," Dkt. Nkengasong alisema, akiongeza kwamba, "Tusipofanya hivyo, tutaelekea kupata virusi visivyoisha barani na tutukuwa na madhara mabaya huko mbele."

Benedict Oramah, Rais wa Africa-Export Bank (Afreximbank) alisema kwamba Afrika haina jinsi bali kuwekeza katika kutengeneza chanjo zake.

Benki hiyo imetoa bilioni $2 kufadhili ununuzi wa dozi milioni 270 za chanjo. Afrika inahitaji zaidi ya bilioni $6 kununua chanjo ili kuongezea katika chanjo zinazotolewa na COVAX. 

Bw. Omarah alisema kwamba Afrika inapaswa kusaidia taasisi zake zenyewe kufadhili utengenezaji wa chanjo zake.

Masomo kutokana na Ebola

Tukiangalia masomo tuliyojifunza wakati wa kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Sierra Leone, Francis Kaikai, Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kiuchumi alizungumzia umuhimu wa kuzindua chanjo kwa muda muafaka na kuweka mipango ya muda mrefu.

"Kumekuwa na hali ya watu kusita kukubali chanjo hizo. Tunahitaji kuendesha kampeni za kuelimisha watu kukabiliana na taarifa potofu na taarifa za uwongo hasa katika maeneo ya vijijini,"Bw. Kaikai alihimiza.

Mwenzake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo pia imeathirika na virusi vya Ebola na sasa COVID-19 sawa na nchi nyingine duniani, Sele Yalaghuli, alisema kwamba makubaliano baina ya nchi na nchi yalihitajika ili kusaidia Afrika kununua chanjo. 

Dkt. Amadou Sall, Mkurugenzi wa taasisi ya Institut Pasteur de Dakar nchini Senegal, alisema kuwa kuna haja ya kutatua janga hili kwa haraka na kusaidia kuongeza utoaji chanjo.

Taasisi ya Institut Pasteur iliendesha jaribio la kwanza la upimaji COVID barani Afrika na ikatofautisha virusi hivi na homa ya manjano na kutengeneza chanjo yake ndani ya miaka kumi.

Aliliambia jopo hilo kwamba uratibu ni mbinu muhimu katika utafiti na utengenezaji wa chanjo, pamoja na ushirikiano mzuri na kuwa na mtandao mzuri wa usambazaji ili kupunguza vizingiti vya kibiashara pamoja na kuwa na kanuni thabiti.

"Tuna uwezo wa kuzalisha chanjo hii barani na tungeweka utaratibu mpya wa afya kwa umma," Dkt. Sall alisema.

Jopo lilikubali kwamba kukuza uwezo wa Afrika kutengeneza chanjo za COVID-19 kungekwenda pamoja na kusalidia bara hili kurejea katika hali yake ya awali.

 

 

Mada: