Kundi la kwanza la raia 15,000 wakirejea, Sudan yaongeza huduma za kiafya katika vituo vya kuingilia

Get monthly
e-newsletter

Kundi la kwanza la raia 15,000 wakirejea, Sudan yaongeza huduma za kiafya katika vituo vya kuingilia

UN News
6 July 2020
By: 
Taswira ya kutoka angani ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum
WFP/Abeer Etefa
Taswira ya kutoka angani ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum

Taarifa iliyotolewa hii leo mjini Khartoum, Sudan na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM inaeleza kuwa serikali ya Sudan kuanzia mwezi uliopita,ikishirikiana na IOM imeanza kuratibu kurejea nyumbani kwa kundi la kwanza la raia wanaokadiriwa kufikia 15,000 ambao walikuwa wamekwama katika mataifa mengine.

IOM imesema wengi wa raia hao wanaorejea wako katika uhitaji mkubwa. Maeneo ambako IOM na pia shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO yanaisaidia serikali ya Sudan kuimarisha hatua za ufuatiliaji wa afya ya watu katika vituo vya kuingilia ni pamoja na Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum, Uwanja wa kimataifa wa ndege wa Port Sudan pamoja na bandari ya Swakin.

IOM imekabidhi kwa serikali vifaa vya kujikinga yaani PPE, zikiwemo zaidi ya barakoa 50,000, glovu 63,000, vitakasa mikono 1,600 pamoja na vipima joto vitano kwa ajili ya matumizi katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum. 

"Alama za kuelekeza watu kuhusu umbali kati ya mtu na pia uelewa kuhusu COVID-19 pia vimetolewa." Imeeleza taarifa ya IOM.

Msaada zaidi kwa uwanja huo wa ndege utajumuisha pia ukarabati wa vituo vya uchunguzi, kutenga wagonjwa au wanaoshukiwa, na mafunzo kuhusu kukinga na kudhibiti ugonjwa kwa maafisa walioko mstari wa mbele katika mipaka.

Kutokana na mlipuko wa COVID-19, Sudan ilitangaza dharura ya kiafya kwa nchi nzima, ikafunga viwanja vya ndege, bandari na njia nyingine pia ikaweka katazo la kutotembea katika muda maalumu.

Wengi wa raia wa Sudan ambao wameonesha nia ya kurejea wako katika maeneo ya Mashariki ya kati, Afrika Kaskazini na Asia. Kipaumbele kinatolewa zaidi kwa wazee na wale ambao wako katika uhitaji mkubwa wa matibabu.