Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Kudorora kwa chanjo DRC kunayaweka maisha ya mamilioni ya watoto njiapanda -UNICEF

Get monthly
e-newsletter

Kudorora kwa chanjo DRC kunayaweka maisha ya mamilioni ya watoto njiapanda -UNICEF

UN News
15 May 2020
By: 
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
UNICEF/Thomas Nybo
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeonya kwamba kushuka kwa kiwango cha utoaji chanjo kilichoripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kitawaacha mamilioni ya watoto katika hatari kubwa ya kupata magonjwa yatakayokatili maisha yao ikiwemo polio, surua na homa ya manjano.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa shirika hilo Marixie Mercado "viwango vya kawaida vya chanjo kwa watoto vimeshuka kati ya asilimia 2 na 10 DRC katika mwezi wa Januari na Februari mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2019 na huenda  ni kutokana na changamoto kama mfumo duni wa usambazaji, kufikia eneo dogo na kutokuwa na akiba ya chanjo hizo."

Mercado ameongeza kuwa kwa ujumla watoto 86,905 hawakupata chanjo ya matone ya polio, wengine 84,676 hawakupata chanjo ya surua na watoto 107,010 hawakupata chanjo ya homa ya manjano katika kipindi hicho. Hivyo DRC huenda ikashuhudia visa zaidi vya polio, surua na homa ya manjano vikiibuka

Hata hivyo shirika hilo limeongeza kuwa sasa mpango wa DRC wa chanjo (EPI) unakabiliwa na changamoto mpya ambayo bila shaka itafanya hali kubwa mbaya zaidi, ambayo ni  janga la ugonjwa wa corona au COVID-19.

“Wahudumu wa afya wanaoendesha chanjo hiyo hawana vifaa vinavyostahili kujikinga wenyewe, wasaidizi na watoto dhidi ya virusi vya corona.”

Kwa mujibu wa UNICEF wazazi wanasita kuwapeleka watoto katika kampeni za chanjo kwa kuhofia kwamba watajiweka katika hatari Pamoja na watoto wao ya kupata COVID-19.

Takwimu za shirika hilo zinaonesha kwamba chanjo zote zinazopendekezwa kwa watoto wadogo dhidi ya magonjwa yote hatari ikiwemo pepopunda, homa ya ini, donda koo na magonjwa mengine imeshuka kwa asilimia 8 hadi 10 huku chanjo ya polio iikishuka kwa asilimia 8.4.

Mwakilishi wa UNICEF DRC Edouard Beigbeder ameonya kwamba “endapo mwenendo huu wa kushuka kwa chanjo utaendelea , basi utafuta mafanikio yote yaliyopatikana miaka miwili iliyopita katika kupambana magonjwa kama surua. Idadi kubwa ya watoto wasiopatiwa chanjo inamaanisha hatari kubwa zaidi ya milipuko ya magonjwa na hii itaongeza shinikizo katika mfumo wa afya ambao tayari umelemewa.”

UNICEF imeitaka serikali ya DRC kuzindua kampeni ya kuziba pengo la chanjo hizo nchi nzima ili kumfikia kila mtoto na chanjo za kuokoa maisha. Pia limewataka wahisani kunyoosha mkono zaidi kusaidia kwani chanjo zinahitajika pamoja na vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya.