Katika hospitali ya Benin, daktari mwanamke anaongoza mapambano dhidi ya COVID-19

Get monthly
e-newsletter

Katika hospitali ya Benin, daktari mwanamke anaongoza mapambano dhidi ya COVID-19

Mtaalam wa dharura za kimatibabu na majanga, Dkt. Babia aliwahi kukabiliana na majanga manne ya kiafya.
Afrika Upya: 
22 March 2021
Dr. Babio (left) and Dr. Amoussouvi preparing for the visit of all hospitalized patients.
Aboudou Souleymane
Dk Babio (kushoto) na Dk Amoussouvi wakijiandaa kwa ziara ya wagonjwa wote waliolazwa hospitalini.

Dkt. Rokhiatou Babio ni mmoja wa wanawake wachache Benin wanaoongoza kikosi cha watoa huduma wa afya kilicho mstari wa mbele kupambana na Covid-19. Anasimulia uzoefu wa kutisha sana alioupitia siku hiyo ya giza, mwezi mmoja baada ya kuanza kazi.

“Wakati wa maumivu makubwa sana katika kukabiliana na janga hili ulikuwa Juni 2020 pindi nilipopata wagonjwa watatu wa COVID-19. Wote walifariki siku hiyo hiyo,” anaeleza.

“Mmoja wa wagonjwa hao watatu alifariki mikononi mwangu”

Kimya kikubwa kinamtawala kabla ya kuendelea. “Kisha inabidi uwashughulike wazazi baada ya tangazo la vifo hivyo. Kigumu zaidi kwa wazazi hawa ni kushindwa kuchukua miili. Ni vigumu kuwafanya waelewe, hata kwa usaidizi wa mwanasaikolojia,” daktari anaeleza.

Dkt. Babio ni daktari mkuu katika kitengo cha dharura katika hospitali ya chuo Kikuu cha Borgou kaskazini mwa Benin. Amefanya kazi na vituo vingi vya afya, anasimamia kikosi cha wafanyakazi 40 wa afya katika kituo cha kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 cha hospitali ya maagizo ya kijeshi ya Borgou.  Kituo chake kinapokea wagonjwa wa Covid-19 kutoka vitengo vitano kati ya 12 vya Benin – Atacora, Borgou, Alibori, Donga na Colliness.

Mtaalam wa kushughulikia majanga

Kama mkongwe wa matibabu ya dharura na majanga katika vituo vya afya kaskazini mwa nchi, Dkt. Babio ameshughulikia majanga manne ya afya katika fani yake.  Baada ya kukabiliana na janga la Covid-19, dharura yake ya tano, aliwapa motisha wengine wasio na ujuzi katika kikundi chake.

“Punde tu baada ya kuanza kazi, lengo lilikuwa kuyaokoa maisha ya wagonjwa huku nikilinda maisha wahudumu wa afya, wengi wao hawajawahi kukabiliana na janga. Kwa hiyo, ilikuwa ni lazima tangu siku za mwanzo kutengeneza mazingira ya ujasiri na kuwafanya watake kuwashughulikia wagonjwa kwa COVID-19,” anasema.

Dkt.Babio, aliwagawanya wafanyakazi wake katika makundi matatu kwa kuzingatia taaluma mbalimbali na jinsia zote. Ili waweze kufanya kadri wawezavyo, alisikiliza masuala ya wafanyakazi wote, ya kikazi na binafsi.

“Kila mfanyakazi mwenzangu ana namba yangu ya simu na anaweza kunipigia wakati wowote kulalamika. Hili linapunguza msongo wa mawazo na kuhakikisha ushughulikiaji mzuri wa janga hilo,” anaongeza.

Lakini wakati mwengine inawashangaza watu wa Benini kumuona mwanamke akiongoza kitengo cha dharura na magonjwa ya mlipuko, achilia mbali  kuwa mratibu  wa kusimamia matibabu ya  Covid-19 .

“Baadhi ya watu huvuka mipaka na kusema kuwa nilichaguliwa kama mratibu kwa kuwa ni mwanamke na kwa sababu nilikuwa na urafiki na watu wenye madaraka, bila ya kuzingatia kwamba tangu mwaka 2016, nimekuwa nikisimamia majanga ya homa za hemorrhagic ya virusi (viral hemorrhagic fevers) huko Lassa na kwamba umahiri wangu umetambuliwa katika ngazi za kimataifa,” anasema.

Wanawake kushughulikia majanga

Daktari huyo anasisitiza kuwa wanawake ni wazuri katika kushughulikia majanga. Anasema: “kwanza kabisa sisi ni wamama, kwa hivyo, tumezaliwa kuonyesha huruma.”

Mfanyakazi mwenzake, Dkt. Hermes Melvis Amoussouvi, daktari mkuu anakubali kuwa uongozi hauna jinsia.

“Kiongozi anatakiwa kuweza kuwahamasisha wote wanawake na wanaume. Lakini ni muhimu, na inatambulika zaidi kuwa wanawake wanafahamu uwezo wao wa kufanya jambo vizuri zaidi kuliko wanaume. Wanawake wana uwezo wao, na ni lazima tulikubali swala hili. “Anasema Dkt Amoussouvi.

Shirika la Umoja wa Mataifa nchini  Benin, linafanya kazi  kwa karibu na serikali  ili kuwezesha  ujumuishaji  wa wanawake katika sekta zote za Jamii, ikiwemo udaktari.

“Hatuwezi kujenga maisha ya baadae tunayoyataka na kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu bila ya ushiriki kamili wa wadau wote katika jamii, hasa wanawake,” anasema Salvator Niyonzima, mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa Benin.

Anasisitiza umuhimu wa kujenga na kukuza usawa wa jinsia na haki za wanawake katika muktadha mpana wa kijamii.

“Usawa wa Jinsia, uliowekwa ndani ya lengo namba tano katika Maendeleo Endelevu mara kadhaa unapimwa kwa uwepo wa muongozo wa sheria kuhamasisha, kutekeleza na kufuatilia matumizi ya kanuni dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya jinsia,” ananukuu Bwana. Niyonzima

Kisa cha kwanza cha COVID-19 Benin

Tangu kisa cha kwanza cha COVID-19 kutangazwa nchini  Benin mnamo  Machi mwaka 2020, kituo kinachoendeshwa  na Dkt. Babio kimesajili  wagonjwa 117, ambapo  wagonjwa  96  wamepona huku watano wakiwa bado wanaendelea na matibabu.

Benini imerikodi visa 5,434 mpaka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, ikiwemo 4,248 waliopona, 1,116 wakiendelea na matibabu na vifo 70. Kufikia Machi 19, namba ya visa vilivyothibitishwa iliongezeka kufikia 6,501 na jumla ya vifo 81, kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani - WHO

Chini ya uongozi wa mwakilishi mkazi, mashirika yote ya Umoja wa Mataifa Benin na washirika wengine wa maendeleo wamekuwa wakichangia katika kupambana dhidi ya COVID-19, wakitoa msaada wa kila aina kwa serikali, zikiwemo bidhaa muhimu, vifaa vya matibabu, fedha na kujenga uwezo. Msaada huu wa Umoja wa Mataifa pia ulifika kwa vituo vyote vya kutoa matibabu ya COVID-19, kikiwemo kile cha Dkt. Babio huko Parakou.

Kwa msaada kama huu, Dkt. Babio, anaongoza kituo, akifuatilia matibabu na kushughulikia visa vyenye changamoto. Anasonga mbele kila wakati.

“Ni furaha iliyoje kuwaona wagonjwa wetu wakiendelea vizuri. Najihisi kupata nguvu sana wakiushukuru usaidizi wetu. Ndiyo, tunayaokoa maisha ya binadamu,” anasema kwa ushujaa.

Umahiri wa Dkt. Babio unatambulika vyema na wenzake na wagonjwa. “Natoa pongezi zangu kwa kikosi hiki chini ya uongozi wa mwanamke jasiri na mtaratibu,” anaeleza Bi. Hermine Fatoumbi, mgonjwa aliyetoka kupona COVID-19 hivi karibuni.

 

Mada: 
More from this author