Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka uchunguzi ufanyike kuhusu makaburi la watu wengi yaliyogundulika Libya

Get monthly
e-newsletter

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka uchunguzi ufanyike kuhusu makaburi la watu wengi yaliyogundulika Libya

UN News
17 June 2020
By: 
Mji mkongwe wa Benghazi, Libya Februari 2019
UN OCHA/GILES CLARKE
Mji mkongwe wa Benghazi, Libya Februari 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kushitushwa kwake kutokana na kugundulika kwa makaburi ya watu wengi nchini Libya katika siku za hivi karibuni, katika eneo ambalo hivi karibuni lilikuwa chini ya kile kinachofahamika kama wapinzani wa serikali wanaojiita Libyan National Army (LNA) wakiwa chini ya Jenerali Khalifa Haftar.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL imetangaza Alhamis ya tarehe 11 mwezi huu wa Juni kugundulika kwa takribani makaburi matano huko Tarhouma, kilomita kama 100 kusinimashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli na ambayo ilikuwa ngome ya vikosi vya Jenerali Haftar wakati wa kampeni za kuikamata Tripoli, kampeni ambayo imedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Katika taarifa aliyoitoa hii Jumamosi kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu Guterres anasema anatoa wito “ufanyike uchunguzi wa kina na wa wazi”, na waliotekeleza mauaji hayo wafikishwe katika mikono ya sheria.

Bwana Guterres amezitaka mamlaka nchini Libya kuyalinda maeneo yaliyogundulika kuwa na makaburi ya watu wengi, kuwatambua walioathirika, kutambua chanzo cha kifo na kuirejesha miili kwa ndugu zao. Aidha Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameihakikishia Libya kuwa Umoja wa Mataifa uko pamoja nao katika suala hili.

“Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena anazikumbusha pande zote katika mgogoro nchini Libya, jukumu lao chini ya sheria ya kibinadamu ya kimataifa na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu. Amerejelea kutoa wito wa kusitisha haraka mapigano nchini Libya ili kuokoa maisha na kumaliza mateso kwa raia.” Ameeleza Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Stéphane Dujarric.

Katika kkikao cha hivi karibuni cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mkuu wa UNSMIL Stephanie Williams alieleza kuwa raia wa Libya walikabiliwa na mabomu na kukatwa kwa maji na umeme karibia kila siku wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na akaongeza kuwa kwa namna silaha na wapiganaji kutoka nje walivyokuwa wakimiminika kuingia katika nchi hiyo, kuna wasiwasi kuwa hali itakuwa mbaya zaidi kwa watu wa Libya.