Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Hatua za haraka zahitajika kukomesha FGM, ndoa za utotoni na upendeleo -UNFPA

Get monthly
e-newsletter

Hatua za haraka zahitajika kukomesha FGM, ndoa za utotoni na upendeleo -UNFPA

UN News
30 June 2020
By: 
Kazi ya sanaa ya Fatma Mahmoud Salama Raslan
Artwork by Fatma Mahmoud Salama Raslan
Kazi ya sanaa ya Fatma Mahmoud Salama Raslan

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la idadi ya watu duniani UNFPA imesema ili kukabiliana na janga la kimyakimya la mila potofu hatua za haraka zinahitajika kukomesha ukeketaji (FGM), ndoa za utotoni na mila zingine ambazo zinathiri wanawake na wasichana.

Ripoti hiyo ambayo ni ya “Hali ya idadi ya watu duniani kwa mwaka 2020” inasema kila mwaka mamilioni ya wasichna wanakuwa waathirika wa mila potofu zinazowaumiza kimwili na kihisia kwa ufahamu na hiyari ya familia zao, marafiki na jamii zao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo imejikita zaidi katika mila tatu zilizomea mizizi ambazo ni ukeketaji, ndoa za utotoni na upendeleo kwa watoto wa kiume zaidi ya wa kike, kuna hulka au mila mbaya 19 kuanzia unyooshaji wa matiti, hadi upimaji wa bikra ambazo zinachukuliwa kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu .

Athari za mila potofu

Akizungumzia ripoti hiyo mkurugenzi mtendaji wa UNFPA Dkt.Natalia Kanem amesema “Mila potofu dhidi ya wasichana zinasababisha athari mbaya zinazodumu kwa muda mrefu na kuwapora wasicha hao haki ya kufikia kikamilifu uwezo wao. Mwaka huu pekee inakadiriwa kwamba wasichana milioni 4.1 kote duniani wamepitia ukeketaji. “

Ameongeza kuwa na leo hii wasichana 33,000 wa umri wa chini ya miaka 18 watashinikizwa kuingia katika ndoa za utotoni na kwa kawaida kwa wanaume ambao ni wakubwa sana kwao.

Pia upendeleo mkubwa wa wavulana dhidi ya wasichana katika baadhi ya nchi umechochea ubguzi wa kijinsia au kutelekezwa kwa watoto wa kike ambako kumesababisha vifo vya watoto na matokeo yake wasichana milioni 140 kutoweka.

Tabia zingine mbaya zimeanza kupotea katika nchi ambazo zilikuwa zimekita mizizi imesema ripoti. Lakini kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu katika nchi hizo idadi ya wasichana wanaoathirika na tabia hizo itaongezeka katika miongo ijayo endapo hatua za haraka hazitochukuliwa.

Nchi zinawajibika kwa mikataba ya kimataifa

Ripoti hiyo ya UNFPA inasema nchi ambazo zimeridhia mikataba ya kimataifa kama mkataba wa haki za mtoto zina wajibu wa kukomesha mila hizo ziwe zinashinikizwa kwa wasicha hao na ndugu wa familia, jumuiya za kidini, wahudumu wa afya, makampuni ya biashara au taasisi za serikali.

Nchi nyingi zimechukua hatua za kisheria lakini sheria peke yake haitoshi. Miongo ya uzoefu na utafiti inaonyesha kwamba mtazamo wa kuanzia chini hadi juu, na mtazamo wa mashinani ni bora zaidi katika kuleta mbadiliko.

Kwa mantiki hiyo Dkt. Kanem amesisitiza kwamba “Ni lazima tushughulikie tatizo hili kwa kukata miziz yake hususan mila zinazomkandamiza mwanamke. Lazima tufanye kazi nzuri zaidi ya kuziunga mkono juhudi za kijamii za kuelewa athari za mila hizo kwa wasichana na faida itakayopatikana kwa jamii nzima endapo watazikomesha mila hizo.”

Mabadiliko ya mifumo yahitajika

Chumi na mifumo ya kisheria inayounga mkono na kusaidia mila hizo inapaswa kurekebishwa na kufanyiwa mabadiliko ili kumuhakikishia kila mwanamke fursa sawa imesema ripoti hiyo.

Kubadilisha sheria za mirathi ya mali kwa mfano itaondoa faida kubwa kwa familia za kuwapendelea watoto wao wa kiume zaidi ya wasichana na itasaidia kutokomeza ndoa za utotoni.

Ripoti inasisitiza kuwa kutokomeza ndoa za utotoni na ukeketaji duniani kote inawezekana ndani ya miaka 10 kwa kuongeza juhudi za kuhakikisha wasichana wasalia shuleni kwa muda mrefu, kuwafundisha stadi za maisha na kuwajumuisha wanaume na wavulana katika mabadiliko ya kijamii.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa uwekezaji wa jumla ya dola bilioni 3.4 kwa mwaka hadi mwaka 2030 zitatokomeza mila hizi mbili potofu na kumaliza madhila kwa wasicha takribani milioni 84.

Wakati hatua zimepigwa za kutokomeza mila hizo kote duniani janga la COVID-19 linatishia kubadili mafanikio hayo imesema ripoti.

Tathimini ya hivi karibuni imeonyesha kuwa endapo huduma na program zinaendelea kufungwa kwa miezi sita wasichana wengine milioni 13 huenda wakalazimika kutumbukia kwenye ndoa za utotoni na milioni 2 zaidi kuingizwa kwenye ukeketaji kati ya sasa na 2030.

Hivyo Dkt. Kanem amesema “Janga hili linafanya kazi yetu kuwa ngumu zaidi na pia inayohitaji uharaka kwani wasichana wengi wako hatarini. Hatutosita hadi pale haki, maamuzi na miili ya wasichana wote itakapokuwa mali yao kikamilifu.”