Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

FAO imenijengea uwezo wa kufuga nyuki kisasa -Mkulima Kigoma

Get monthly
e-newsletter

FAO imenijengea uwezo wa kufuga nyuki kisasa -Mkulima Kigoma

UN News
5 June 2020
By: 
Mizinga ya nyuki ya kisasa, ijulikanayo kama Tanzania Top Bar Hives ikiwa imetengenezwa na mfugaji aliyepatiwa mafunzo na FAO kupitia KJP.ukua hatua na kutekeleza kwa vitendo.
FAO/Tanzania
Mizinga ya nyuki ya kisasa, ijulikanayo kama Tanzania Top Bar Hives ikiwa imetengenezwa na mfugaji aliyepatiwa mafunzo na FAO kupitia KJP.ukua hatua na kutekeleza kwa vitendo.

Mafunzo yaliyotolewa na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO,  kuhusu mbinu bora za ufugaji nyuki na matumizi ya mizinga bora huko mkoani Kigoma nchini Tanzania, yameanza kuzaa matunda baada ya baadhi ya wafugaji waliopata mafunzo kuchukua hatua na kutekeleza kwa vitendo.

Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo yaliyoendeshwa mwaka jana wa 2019 wilaya ya Kibondo kupitia programu ya pamoja ya Kigoma, ya Umoja wa Mataifa, KJP,  ni Hijja Katobagula mkazi wa wilaya ya Kibondo ambaye anasema kuwa, , “sasa baada ya kupata mafunzo yale ya siku tatu na kuelewa vizuri tasnia nzima ya ufugaji wa nyuki, faida na hasara, mazao yatokanayo na ufugaji nyuki, thamani na mambo yote katika ufugaji wa nyuki, ndio nikakata shauri na kuamua sasa kufuga nyuki kisasa."

Mafunzo yamenijenga sana

Katobagula ambaye pia ni mkulima anasema kuwa, "baada ya kupata mafunzo kimsingi tulifundishwa pia hata jinsi ya kuanzisha miradi midogo midogo ya ufugaji wa nyuki. Kwa hiyo baada ya mafunzo tukaanza mradi wetu wa kwanza mwaka jana mwezi Oktoba na tulitengeneza mizinga ya kisasa kabisa iitwayo Tanzanian Top Bar Hives.  Mwanzoni tulitengeneza mizinga 151 na tayari tumeshatega makundi kwa kutundika kwenye miti, lakini mafunzo pia yalituelekeza ufugaji wa kisasa ambapo tutakuja kujenga nyumba ya nyuki na nyuki watakuwa wanaishi pale bila kubughudhiwa.”

Eneo afugalo nyuki ni kwenye msitu wake wa asili ambao Bwana Katobagula aliuboresha pia kwa kupanda miti ili kuhifadhi mazingira na sasa kila mti wenye mizinga umepatiwa namba kurahisisha ukaguzi.

Mavuno ya uhakika zaidi mwezi Juni 2020

Alipoulizwa nini matarajio yake, Bwana Katobagula anasema kuwa, “tunatarajia hiyo mizinga tuliyotega makundi awali na baadaye tutahamishia kwenye nyumba ya nyuki, tunatarajia mwezi Oktoba na Novemba tunaweza kuanza kupata mavuno ya awali. Lakini kwa hii mizinga ya awamu ya pili, tunakwenda kutega makundi, na tunatarajia mwezi Oktoba au Novemba tutaenda kufanya ukaguzi.  Lakini mavuno mazuri tunatarajia mwezi Juni mwakani kwa kuwa tayari nyuki tutakuwa tumewahamisha na kuwaweka kwenye nyumba zao na uzalishaji utakuwa unaendelea kama kawaida.”

Kwa mujibu wa Bwana Katobagula, mipango yake ya muda mrefu ni kuongeza mizinga na kupanua ufugaji nyuki katika halmashauri 5 za mkoa wa Kigoma ambazo ni Kakonko, Kasulu, Buhigwe, Kibondo na Uvinza.

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.