Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

COVID-19 yadumaza tiba dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza -WHO

Get monthly
e-newsletter

COVID-19 yadumaza tiba dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza -WHO

UN News
3 June 2020
By: 
Wanawake walio na saratani ya matiti hupokea matibabu ya bure katika Taasisi ya Saratani ya Kitaifa huko Mexico City.
PAHO
Wanawake walio na saratani ya matiti hupokea matibabu ya bure katika Taasisi ya Saratani ya Kitaifa huko Mexico City.

Huduma za kinga na tiba dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs zimevurugwa kwa kiasi kikubwa tangu kulipuka kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, limesema shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO kufuatia utafiti uliofanyika katika mataifa 155.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, au NCDs ni pamoja na saratani, kisukari na magonjwa ya moyo ambapo WHO kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, imesema kuwa iliendesha utafiti huo katika kipindi cha wiki 3 za mwezi uliopita wa Mei na kubaini kuwa madhara ni makubwa duniani kote, lakini nchi za kipato cha chini ndio zimeathirika zaidi katika huduma za kinga na tiba dhidi ya NCDs.

WHO inasema kuwa hali hiyo inatia hofu zaidi kwa sababu watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza wako hatarini zaidi kuambukizwa COVID-19 na hata kufariki dunia.

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa, “matokeo haya yanathibisiha kile ambacho tumekuwa tukisikia kutoka mataifa mbali mbali kwa wiki kadhaa sasa. Watu wengi ambao wanahitaji tiba ya saratani, moyo na kisukari wameshindwa kupata huduma na dawa tangu janga la COVID-19 lianze. Ni muhimu kwa nchi kusaka mbinu bunifu kuhakikisha kuwa huduma kwa wagonjwa hao zinaendelea hata katika vita dhidi ya COVID-19.”

Utafiti umebaini kuwa huduma za afya zimevurugwa kiasi au kwa kiasi kikubwa katika nchi nyingi ambapo zaidi ya asilimia 53 za mataifa hayo 155 zina huduma kidogo au hazitoi kabisa huduma kwa wagonjwa wa moyo, asilimia 49 huduma kwa wagonjwa wa kisukari zimevurugika na asilimia 42 za huduma za saratani halikadhalika.

Wahudumu wa afya wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika asilimia 94 ya mataifa yaliyohusika kwenye utafiti, wamepangiwa majukumu kwa kiasi kidogo au kikubwa kuhudumia wagonjwa wa COVID-19.

WHO inasema kuwa suala la kusogeza programu za uchunguzi mathalani wa saratani ya titi au kizazi, limesambaa na kwa mujibu wa utafiti asilimia 50 ya mataifa yamesogeza mbele programu hizo, hii ikiwa ni  utekelezaji wa mapendekezo ya WHO ya kupunguza huduma zisizo za dharura wakati wa kushughulikia janga la Corona.

Hata hivyo WHO imebaini kuwa sababu kuu ilikuwa ni uhaba wa wahudumu, dawa na vifaa vya uchunguzi.

Tayari asilimia 70 ya nchi husika zimetangaza kuanza kutenga fedha za nyongeza ili kujumuisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye mipango ya kitaifa dhidi ya COVID-19.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza husababisha vifo vya watu miioni 41 kila mwaka ulimwenguni kote.