COVID-19, mabadiliko ya tabianchi vimetufunza tunachokichagua leo, ni muhimu kwa kesho pia

Get monthly
e-newsletter

COVID-19, mabadiliko ya tabianchi vimetufunza tunachokichagua leo, ni muhimu kwa kesho pia

UN News
23 September 2020
By: 
Wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wanazingatia umbali kati ya mtu na mtu wakati mikutano inayoendelea katika Umoja wa Mataifa
UN Photo/Eskinder Debebe
Wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wanazingatia umbali kati ya mtu na mtu wakati mikutano inayoendelea katika Umoja wa Mataifa

Janga la corona au COVID-19, changamoto za mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko yanayostahili baada ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa ni funzo tosha kwamba kile tunachokichagua leo ni muhimu pia kwa vizazi vya kesho amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antionio Guterres.

Ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani hali sio ile iliyozoeleka kila mwaka wakati wa ufunguzi wa mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu unaoambatana na mpishempishe ya kila aina, leo kwa wachache waliojumuika ndani ya ukumbi huu barakoa zimetawala na pia kujitenga kisa ni janga la corona au COVID-19 lililosababisha asilimia kubwa ya mjadala wa mwaka huu kufanyia kwa njia ya mtandao. 

Katibu Mkuu Guterres akizungumza katika ufunguzi wa mjadala huo amba leo umejikita katika mada ya“Mustakabali tunaoutaka, Umoja wa Mataifa tunaoutaka”kwa lengo la kusisitiza ahadi ya pamoja ya ushirikiano wa kimataifa kupambana na COVID-19 kupitia hatua za pamoja, amesema “Katika dunia hii ambayo imepunduliwa juu chini, ukumbi wa Baraza kuu umekuwa kitu kigeni kabisa, janga la COVID-19 limebadili mkutano wetu wa kila mwaka kiasi cha kutotambulika, lakini limeufanya kuwa wa muhimu kuliko wakati mwingine wowote.”

Akakumbusha masuala manne ambayo ni tishio kubwa kwa mustakabali wa pamoja “Mosi mivutano ya hali ya juu ya kijiografia ambayo imekuwepo kwa miaka mingi, pili mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, tatu ongezeko la kina la kutoaminiana duniani, na nne upande wa kiza wa ulimwengu wa kidijitali. Lakini kumbe mpanda farasi wa tano alikuwa kajificha kivulini, tangu Januari janga la COVID-19 limeughubika ulimwengu na kuzidisha adha kwa changamoto zilizopo.” 

Hakuna aliyesalimika na COVID-19 

Ameongeza kuwa janga hilo limegusa kila kona ya dunia na kila nyanja , kuanzia afya, uchumi, ajira na vitisho vipya kwa haki za binadamu. Lakini pia kupanua pengo la kutokuwepo kwa usawa, janga la mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la migawanyiko katika jamii na kukithiri kwa ufisadi na pia limetoia dosari kwenye hatua kubwa zilizopigwa kwa miongo kadhjaa katika kupunguza umasikini na maendeleo. 

“Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 umasikini unaongezeka, viashiria vya maendeleo ya binadamu vinashuka, tunakwenda kombo katika ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu. Wakati huohuo juhudi za kukomesha utengenezaji wa silaha za nyuklia zinakwenda mrama na tunashindwa kuchukua hatua katika maeneo kunakoibuka hatari hususan kwenye mitandao. Watu wanaumia, sayari yetu inateketea, dunia yetu inahaha, ina shinikizo na inasala uongozi wa kweli nah atua.” 

Amekumbusha kwamba waasisi wa Umoja wa Mataifa miaka 75 iliyopita waliishi kushuhudia vyote majanga, mdororo mkubwa wa kiuchumi wa dunia, mauaji ya kimbari na vita vya dunia. 

Walijua gharama za kutengana na tahamani ya umoja. 

Ni wakati wa kutafakari 

“Leo hii tuanakabiliwa na wakati wetu wa 1945, janga hili ni la aina yake ambalo hatujawahi kulishuhudia, lakini pia ni aina ya mgogoro mgogoro ambao tutaushuhudia katika mifumo tofautitena na tena. COVID-19 sio tu kengele ya kutuamsha , ni maandali kwa dunia ya changamoto zijazo. “ 

Guterres ameongeza kuwa ni “lazima tuende sanjari na hali halisi na kutambua kwamba virusi hivyo vimeiadabisha dunia. Lazima tuungane, kama tulivyoona wakati nchi zineshika kila moja njia yake virusi vinakwenda katika kila njia. Lazima tuchukue hatua kwa mashikamano, ni msaada kidogo sana ambao umepelekwa nan chi zisizoweza kumudu kukabili janga hili na tunapaswa kuongozwa na sayansi katika hali halisi. Tukishindwa kukumbatia ukweli basi ni hasara kwa kila mtu” 

Uhasana lazima usitishwe 

Kwa mara nyingine Katibu Mkuu amerejelea wito wa usitishaji uhasala kila kona ya dunia kwa faida ya amani ya kimataifa. 

“Leo hii natoa wito wa msukumo mpya kwa jumuiya ya kimataifa kufanya ndoto hii kutimia ifikapo mwisho wa mwaka huu. Tuna siku 100 tu zilizosalia. Kuna mshindi mmoja tu vita wakati wa janga la corona, ambaye ni virusi vyenyewe. Ombi la awali la usitishaji uhasama liliridhiwa na nachi wanachama 180, Pamoja pia na viongozi wa dini, wadau wa kikanda, mitandao ya asasi za kiraia na wengineo.” 

Na kuna sababu ya kuwa na matumaini amesema kwani katika hali nyingi kumeshuhudiwa hatua mpya za usitishaji uhasama , makubaliano mapya ya amani kama nchini Sudan, kuanza kwa majadiliano ya amani kama Afghanistan, na kwingineko muafaka wa amani umedumu . 

Lakini bado kuna sehemu kama Syria, Libya, Gaza, Mashariki mwa Ukraine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Yemen, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na Sudan Kusini hali bado ni tete katika baadhi ya maeneo 

Hata hivyo ameahidi“Hata katika maeneo ambako vita vinaendelea hatutokata tamaa kusaka amani. Na tusisahau gharama kubwa za vita kwa binadamu.” 

Chonde chonde jumuiya ya kimataifa ingilieni kati 

Guterres ameiomba jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zake ikiongozwa na Baraza la Usalama kufikia lengo la usitisghwaji uhasama wa kimataifa ifikapo mwisho wa mwaka huu. 

“Tuna siku 100 na saa zinakimbia dunia inahitaji usitishwaji mapigano wa kimataifa kote kwenye vita na wakati huohuo tunahitaji kufanya kila liwezekanalo kuepuka vita vipya baridi.Tunaelekea kwenye hatari kubwa , dunia yetu haiwezi kumudu mustakabali ambao mataiofa makubwa mawili kiuchumi yanaigawanya dunia , kila moja na sheria zake za biashara na fedha na uwezo wa intenaneti na akili bandia. Lazima tukwepe hili kwa gharama zozote.” 

Kuhusu kuzisaidia nchi zizisojiweza guterres amezitaka nchi zilizoendele ambazo amesema zimesaidia sana watu wake kuhakikisha nchi zinazoendelea hazitumbukii katika janga la kifedha , kuongeza umasikini na mgogoro wa madeni. 

Wanawake na wasichana wapewe kipaumbele 

Na wiki moja kuanzia sasa amesema viongozi wa dunia watakutana kusaka suluhu kwenye mkutano wa ufadhili a fedhja kwa ajili ya maendeleo wakati huu wa janga la COVID-19 na zaidi na msukumu safari hii utakuwa kwa wanawake na wasichana. 

Amesisitiza kwamba mamilioni ya wasichana wanapoteza fursa za elimu na ndoto zao kwani wakati huu wa COVID-19 wengi wameacha shule, ndoa za utotoni zimeongezeka na ukatili wa kijia umeshika kasi. 

Ametaka kuwepo na ujumuishwaji kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia, uwezeshaji na dira iwe ni malengo 17 ya maendeleo endelevu SDGs. 

Amesema baada ya miaka 25 ya jukwaa la hatua la Beijing ni wakati wasichana na wanawake waweze kufikia uwezo wao na kutimiza ndoto zao. 

Mabadiliuko ya tabianchi 

Katika changamoto ya mabadiliko ya tabianchi Katibu Mkuu amesema ili kukumbatia mabadiliko mapya endelevu inamaanisha ni kuhamia katika nishajti jadidifu na kufikia lengo la kutozalisha hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050. 

Ametoa mapendekezo kwa nchi wachama ya kuhakikisha lengo hilo linatimia . Ameziomba nchi zote kutilia maanani hatua sita chanya kuhusu mabadiliko ya tabianchi wakati zikiokoa, kujijenga upya na kufufua uchumi wao. 

“Mosi tunahitaji kuzifanya jamii zetu kuwa na mnepo na kuhakikisha mabadiliko yenye haki, pili tunahitaji ajira zinazojali mazingira na ukuaji endelevu, tatu kuziokoa sekta za usafiri wa anga, viwanda na usafirishaji wa meli kunapaswa kuwa na masharti yanayokwenda sanjari na malengo ya mkataba wa Paris, nne kukomesha ruzuku kwenye mafuta ya kiskuku, tano kuzichukulia hatari za mabadiliko ya tabianchi katika maamuzi ya masuala yote ya ufadhili wa fedha na sita kufanyakazi pamoja kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.” 

Agano jipya ni kuhakikisha kwamba mifumo ya kimataifa ya kisiasa na kiuchumi inawajibika kwa manufaa ya umaa hali ambayo haifanyiki kwa sasa. 

“Ili kuziba mapengo haya tunahitaji kuhakikisha kwamba mamlaka, utajiri na fursa zinagawanywa kwa wote na kwa usawa. Kuwe na utandawazi sawia kwa kuzingatia haki na utu wa kila binadamu na kuishi vyema na mazingira na kwa uwajibikaji wetu kwa mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo.” 

Nini cha kufanya 

 Bwana Guterres amesema changamoto zote hizi zinazoikabili dunia haziwezi kutatuliwa kwa kujitenga na kwa kurundi nyuma. 

Ili kuzikabili kunahitajika ushirikiano zaidi wa kimataifa na si pungufu, taasisi imara za kimataifa na sio dhoofu, utawala bora wa kimataifa na sio vurugu ambazo ni bure kwa wote. 

“Hebu na tuchagizwe na mafanikio tuliyoyapata katika historia ya Umoja wa Mataifa. Hebu tuchukue hatua kuelekea haki na utu, na hebu tuzikabili changamoto hizi tano na kujenga dunia tunayoihitaji, ya amani, jumuishi na endelevu. Janga limetufunza kwamba tunachochagua ni cha muhimu sana, na tukiganga yajayo hebu tuhakikishe tunachagua kwa busara.”