Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

COVID-19: IMF yasamehe deni la Tanzania la dola milioni 14.3, msamaha zaidi watarajiwa

Get monthly
e-newsletter

COVID-19: IMF yasamehe deni la Tanzania la dola milioni 14.3, msamaha zaidi watarajiwa

UN News
16 June 2020
By: 
Kutokana na janga la Corona lililosababisha shule kufungwa, nchini Tanzania wabunifu MITZ Group wamebuni kifaa cha kuwezesha wanafunzi (pichani) kufanya mafunzo ya sayansi kwa vitendo wakiwa nyumbani bila mwalimu.
UN Tanzania
Kutokana na janga la Corona lililosababisha shule kufungwa, nchini Tanzania wabunifu MITZ Group wamebuni kifaa cha kuwezesha wanafunzi (pichani) kufanya mafunzo ya sayansi kwa vitendo wakiwa nyumbani bila mwalimu.

Shirika la fedha duniani, IMF limeipatia Tanzania msamaha wa deni la dola milioni 14.3 ili kuwezesha nchi hiyo kuhimili athari zitokanazo na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Taarifa ya IMF iliyotolewa jijini Washington DC nchini Marekani imesema kuwa Bodi Tendaji ya shirika hilo imefikia uamuzi huo na fedha hizo ambazo Tanzania ilipaswa kulipa sasa zitatoka katika fuko la IMF la kudhibiti majanga na kuweka unafuu, CCRT.

IMF inasema deni hilo lilipaswa kulipwa kati ya sasa na tarehe 13 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020, na kwamba nyongeza ya msamaha  wa deni linalotakiwa kulipwa kati ya Oktoba 14 mwaka huu hadi Aprili 13 mwaka 2022 itategemea uwepo wa fedha kwenye fuko hilo.

IMF inasema kuwa COVID-19 imedhoofisha matarajio ya ukuaji uchumi wa Tanzania ambapo sasa nchi hiyo inakabiliwa na anguko kubwa la mapato kwenye sekta ya utalii, shinikizo kwenye bajeti na kuanguka kwa ukuaji wa pato la ndani la taifa, GDP, kutoka asilimia 6 hadi asilimia 4 katika mwaka huu wa fedha.

Mara baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo wa msamaha wa deni, Naibu Mkurugenzi Mwendeshaji wa IMF na Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo Tao Zhang amesema, “COVID-19 imekuwa na madhara makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania na kuongeza mahitaji ya kipekee katika ulipaji wa salio. Mamlaka zimetekeleza mikakati ya kudhibiti gonjwa hilo na kuepusha kutwama kwa uchumi. Wamesalia macho kwenye hatari za kusambaa kwa maambukizi na ukosefu wa uhakika utokanao na janga hilo.”

Ni kwa mantiki hiyo amesema fedha ambazo zingetakiwa kulipwa kwenye deni, sasa zitatumika kusaidia kukabiliana na janga la Corona.

“Mamlaka za Tanzania zimejizatiti kutumia rasilimali za ziada kwa malengo yaliyopangwa na kwa uwazi ikiwemo kufanyika kwa ukaguzi wa fedha zinazoelekezwa kwenye kukabili COVID-19,”  amesema Bwana Tao.

Tanzania inakuwa nchi ya 27 kunufaika na msamaha huo wa madeni kupitia mfuko wa CCRT wa IMF kutokana na janga la COVID-19, ambapo jumla ya fedha zilizotolewa kuziba pengo la malipo kwa nchi hizo ni dola milioni 243.

Mataifa mengine yaliyopata msamaha kupitia mfuko huo ni pamoja na Rwanda, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Afghanistan.