COVID-19 imetumbukiza wajane katika hali ngumu zaidi -Guterres

Get monthly
e-newsletter

COVID-19 imetumbukiza wajane katika hali ngumu zaidi -Guterres

UN News
23 June 2020
By: 
Ester Angello mwenye umri wa miaka 44 ni mjane mkazi wa Juba Sudan Kusini. Anajipatia kipato cha kulea wanae 8 kwa kuuza uturi huu anaotengeneza mwenyewe.
UNICEF/Gonzalez Farran
Ester Angello mwenye umri wa miaka 44 ni mjane mkazi wa Juba Sudan Kusini. Anajipatia kipato cha kulea wanae 8 kwa kuuza uturi huu anaotengeneza mwenyewe.

Ikiwa leo ni siku ya wajane duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuangaziwa zaidi kwa kundi linalosahaulika mara kwa mara, wajane, hususan wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Katika ujumbe wake siku ya wajane, Bwana Guterres amesema, “mwaka huu siku ya kimataifa ya wajane inafanyika wakati idadi ya vifo kutokana na COVID-19 inaendelea kuongezeka kila mahali hususan miongoni mwa wanaume. Hii ni fursa ya kipekee ya kuangazia kile ambacho husahaulika kila wakati kwenye majanga, yaani maisha na mustakabali wa wajane wanaobakia.”

Guterres amesema kifo cha mwenza katika wakati wowote ule huacha wanawake wengi bila haki ya kurithi mali na kwamba, “wakati wa janga la sasa, changamoto hizo huwa maradufu kwa wajane na huambatana na unyanyapaa na ubaguzi.”

Ameongeza kuwa kiwango cha kipekee cha kutengwa na machungu ya kiuchumi yatokanayo na COVID-19 vinaweza kuharibu uwezo wa mjane kujitunza yeye na familia yake, na hata kumtenga na jamii yake wakati ambao anakabiliwa na majonzi.

“Kadri tunavyojaribu kushughulikia COVID-19, serikali lazima zifanye kazi kujumuisha msaada kwa wajane kwenye mafungu ya kujikwamua, mathalani kwa kupatiwa msaada wa fedha,”  amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa, "na tunavyohaha kujenga upya na kwa ubora zaidi jamii zetu baada ya janga hili, hatua zozote za kujikwamua lazima ziendane na mabadiliko ya kimfumo, ikiwemo kuondokana na sheria za kibaguzi ambazo zinawanyima wanawake haki sawa na wanaume na pia zihakikishe zinatoa fursa ya kuwepo kwa hifadhi ya jamii ili wanawake hawaanzi upya maisha wakiwa tayari kwenye kundi la kukosa.”

Hata hivyo amezungumzia umuhimu wa takwimu akisema zinahitajika takwimu bora ambazo zimenyumbuliwa kijinsia na kiumri ili kuhakikisha kuwa wajane wanahesabiwa na wanasaidiwa sasa na siku za usoni.

Ni kwa mantiki hiyo amesema katika siku ya wajane duniani hii leo, “hebu na tuimarishe jamii, tuthamini familia na tujenge upya jamii zinazosaidia wajane katika maeneo yote.”

Tarehe 21 mwezi Desemba mwaka 2010, Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba A/RES/65/189 la Baraza Kuu la Umoja huo, ulipitisha tarehe 23 mwezi Juni kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya wajane kwa lengo la kuangazia sauti na uzoefu wa wajane na kuchagiza msaada wa kipekee kwa kundi hilo.