Askari waliokuwa wanapigana, wameungana na wanakaribia kuhitimu mafunzo ya pamoja Sudan Kusini

Get monthly
e-newsletter

Askari waliokuwa wanapigana, wameungana na wanakaribia kuhitimu mafunzo ya pamoja Sudan Kusini

UN News
8 July 2020
By: 
Maafisa wa UNMISS wakizungumza na wenyeji katika soko lililoko mpakani
Video Screen Shot
Maafisa wa UNMISS wakizungumza na wenyeji katika soko lililoko mpakani

Nchini Sudan Kusini, kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano ya amani mnamo Septemba mwaka 2018, takribani askari 5000 kutoka makundi mbalimbali ambayo awali yalikuwa yanapigana, walichaguliwa ili kuwa sehemu ya kikosi kipya cha usalama wa kitaifa. Na sasa wanakaribia kuhitimu kabla ya kupangiwa kazi ya kulinda usalama katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Ni katika eneo la Alel, Malakal nchini Sudan Kusini, kutoka katika pande tofauti zilizokuwa zinapigana wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe, ni wapiganaji waliokutanishwa katika kituo cha mafunzo ya kijeshi ili kuelimishwa na kuunda jeshi la pamoja la taifa.

Askari wa kike anaongoza wimbo wa gwaride ambao askari kutoka serikalini, upande wa upinzani na makundi mengine yaliyokuwa yakijihami kwa silaha, wanaufuta kwa kupiga kwata. Maafisa wa ngazi za juu za kijeshi wanaendesha mafunzo.

Waziri wa ulinzi Angelina Teny amesafiri kwenda katika kituo cha mafunzo kukutana na vikosi. Anavitaka vikosi vya wapiganaji kutoka pande zote, ili waweze kubadilika, kukubali kuwajibika kutokana na makosa yoyote ambayo waliyafanya wakati wa vita kama vile ubakaji, wizi na uharibifu wa nyumba.  ili waweze kubadilika.

 “Tuliwadharau wanawake zetu na watoto. Hatukuwaheshimu wake zetu. Hatukuwaheshimu watoto wetu-tuliwabaka. Huu ni uongo? Kama mtu anakubali mambo ya kutisha na mabaya aliyoyafanya, basi huu ni wakati muafaka kujirekebisha. Lakini ikiwa unaficha kichwa chako kwenye ardhi kama mbuni basi bado una tatizo.”

Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa ofisi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa ya mjini Malakal, Sudan Kusini,  Hazel De Wet anawasihi askari wote kuungana kwa amani kama jeshi moja la kitaifa lililoungana.  Anasema,

 “Kile ambacho tungependa kuona ni jeshi la pamoja kuanza bila kuchelewa. Kwa hivyo, na maneno hayo machache niseme UNMISS, kama Mkuu wa Ofisi ya Upper Nile, sisi ni mshirika wa amani, tumekuwa mshirika wa amani jana, na tutabaki mshirika wa amani kwa wote Sudani Kusini. "

Katika wiki chache zijazo, inategemewa kuwa askari wapya waliopata mafunzo katika kituo hiki cha Alel watahitimu na kutumwa katika maeneo mablimbali kote katika eneo la Upper Nile.