Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

AfCFTA: Wataalam, wafanyabiashara wataka ushiriki thabiti wa wanawake na vijana

Get monthly
e-newsletter

AfCFTA: Wataalam, wafanyabiashara wataka ushiriki thabiti wa wanawake na vijana

Ripoti ya Siku zijazo inayoangazia changamoto na fursa za biashara barani Afrika.
Kingsley Ighobor
Afrika Upya: 
21 December 2020
Akili ya Dijitali ni shirika la mawasiliano lililoko Niamey lililoanzishwa na Lisa na Ben...
UNCTAD/Monica Chiriac
Akili ya Dijitali ni shirika la mawasiliano lililoko Niamey lililoanzishwa na Lisa na Ben, wafanyabiashara wawili wachanga kutoka Benin.
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti hii iko kwa Kiingereza.

Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Wamkele Mene, tangu ateuliwe Machi 2020, ameendelea kusisitiza hitaji la haraka la utekelezaji bora wa makubaliano ya biashara ili kuchochea uchumi unaotishia kuporomoka.

Bwana Mene alirudia tena kauli hiyo katika uzinduzi wa Ripoti ya siku zijazo: Kuiwezesha AfCFTA kufanya Kazi kwa ajili ya Wanawake na Vijana uliofanyika kupitia mtandao tarehe 3 Desemba 2020. 

Ripoti hiyo iliyochapishwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Sekretarieti ya AfCFTA, yenye kurasa 100 inafafanua changamoto na fursa za biashara ndani ya Afrika, na inaonyesha maoni ya wataalam wengine wa maendeleo wa Afrika, watunga sera na viongozi wa biashara, pamoja na uzoefu wa moja kwa moja wa wafanyabiashara, ikijumuisha wanawake na vijana.

Waandishi wanaisifu ripoti hii kama "muhuri wa wakati, unaoangazia matarajio na juhudi za kuanzisha biashara chini ya masharti ya mkataba wa AfCFTA, uliopangwa kufanyika Januari 2021."

AfCFTA sio tu makubaliano ya biashara; bali pia ni nyenzo ya maendeleo inayokusudiwa kuinua Waafrika milioni 100 kutoka kwenye umaskini ifikapo mwaka 2035,  alisema Bwana Mene  wakati wa uzinduzi.

Wachangiaji wanajadili kwa makini ushiriki wa wanawake na vijana katika AfCFTA - kama washiriki na kama walengwa.

"AfCFTA ni fursa ya kugundua vipaji vya vijana wa Afrika na wanawake ili kuhakikisha faida jumuishi," alibainisha Bwana Mene.

Women and Youth in the AfCFTA chart

Edem Adzogenu, Mwenyekiti mwenza wa AfroChampions, jukwaa linaloendeleza kampuni za Afrika, anaonya katika mchango wake: "AfCFTA ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya Afrika katika karne ya 21, lakini itashindwa isipokuwa jumuishi - katika muundo na utekelezaji."

Suala la wanawake na vijana kama wadau wakuu katika maendeleo ya uchumi wa Afrika ni rahisi kuliongelea: Sekta isiyo rasmi inachukua asilimia 85 ya shughuli zote za uchumi barani Afrika; na wanawake ni asilimia 90 ya ajira katika sekta isiyo rasmi, na wanajumuisha asilimia 70 ya wafanyabiashara wasio rasmi.

Asilimia 60 ya idadi ya watu wa Afrika wako chini ya umri wa miaka 25, na kuifanya Afrika kuwa bara changa zaidi duniani.

Wakati lengo kuu la AfCFTA ni kuimarisha biashara ya ndani Afrika, kiwango cha sasa cha biashara ya ndani cha asilimia 18 kinasikitisha”, alieleza Ahunna Eziakonwa, Katibu Mkuu Msaidizi na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kikanda ya Afrika ya UNDP.

Moja ya matokeo ya kiwango hicho cha chini cha biashara ya ndani barani Afrika ni kupoteza kazi zenye malipo mazuri, Bi. Eziakonwa alisisitiza, katika taarifa yake ya ufunguzi katika uzinduzi huo.

Wanawake lazima washiriki kikamilifu katika biashara za kuvuka mipaka, lazima wawe na njia za kupata fedha, mtandao wa uzalishaji na masoko, alisema Bi. Eziakonwa na aliongezea kuwa UNDP, inafanya kazi ya kusaidia wanawake waweze kufikia masoko ya mtandaoni na kushiriki katika biashara kwa njia ya kielektroniki.

Godwin Benson, Mkurugenzi Mtendaji wa Tuteria, jukwaa la mafunzo mtandaoni nchini Nigeria, ni mmoja wa wafanyabiashara wachanga waliochangia kwenye ripoti hii. 

Sekta ya Huduma.

Bwana Benson anaeleza mafanikio yake machache katika kupanua biashara yake katika masoko mengine barani na anatoa orodha ya masuala ya kutekeleza ili kuboresha huduma za biashara mipakani.

Kwanza ni kuelewa "mahitaji na tofauti ya masoko mengine ya Afrika" ili bidhaa na huduma ziwe bora kwa watumiaji katika nchi kadhaa,  anaandika”.

Pili ni kushiriki katika ushirikiano wa kimkakati ili kuweza kufikia masoko ya nje.

Tatu, anapendekeza mfumo wa malipo wa mipakani usio na vikwazo. "Unapaswa kuwa rahisi kwa wateja Misri au Rwanda kulipia biashara Nigeria ... Bila kuwa na malipo yasiyo na vikwazo ya ndani ya Afrika, biashara kama Tuteria, haswa zile zinazoendeshwa na wafanyabiashara wachanga, hazitaweza kufanya biashara barani kote." 

Mwisho, Bwana Benson anapendekeza: “Inapaswa kuwa rahisi na kwa bei nafuu kwa Mkenya kusajili biashara na shughuli za kibiashara nchini Nigeria na kadhalika kwa mfanyabiashara wa Nigeria kusajili biashara Kenya. Itakuwa bora kama mchakato huu unaweza kukamilika mtandaoni.

Ripoti hii pia inaonyesha athari kali za COVID-19 kwa uchumi wa Afrika na inasisitiza fursa endelevu za kujiimarisha.

Mratibu wa Kituo cha Sera ya Biashara cha Afrika katika Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa, David Luke, anaandika kwamba AfCFTA inaweza kuendesha uimarishaji baada ya janga hili na kuwezesha "ukuaji mpana, unaojumuisha na kuingiza vijana wa Afrika katika shughuli za uzalishaji, na kuboresha usawa wa kijinsia.”

Akijikita katika uchambuzi wa Benki ya Dunia, Bwana Luke anasisitiza kuwa utekelezaji wa AfCFTA pamoja na Mkataba wa Uwezeshaji Biashara wa Shirika la Biashara Duniani" unaweza kusababisha kuongezeka kwa mishahara kwa asilimia 10 na kuchangia kuziba pengo la ujira kijinsia kutokana na ongezeko kubwa la wafanyakazi wasio na ujuzi na wanawake”.

Anatarajia kuwa kilimo na kuchakata vyakula vya kilimo vitatoa kazi zenye malipo mazuri kwa wanawake ambao ni karibu asilimia 50 ya waajiriwa katika sekta hizi. Wanawake pia watafaidika na kazi zilizotengenezwa katika elimu, afya, na huduma za elimu ya juu.

Angela Lusigi
Kuwezesha uwekezaji mpakani, kulinda haki miliki, kushirikiana katika forodha na ushuru, na kutekeleza uwezeshaji wa biashara kutahakikisha fursa za usawa na endelevu, ambayo ni muhimu kwa ufanisi wa ukombozi unaoendelea wa biashara ya huduma.
Angela Lusigi
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Ghana

Bwana Luke anaendelea kusema kuwa wakati wanawake wanaojihusisha na biashara isiyo rasmi ya mipakani wana hatari ya kunyanyaswa na kupitia ukatili, AfCFTA inaweza kupunguza changamoto kama hizo wakati shughuli hizo zitakapofanywa kuwa rasmi.

Kitakachobadilisha mambo kwa wanawake

Ongezeko la ajira katika utengenezaji bidhaa, biashara ya kilimo na zingine linaweza kubadilisha mambo kwa mamilioni ya wanawake na vijana wa Afrika, anakubali pia Angela Lusigi, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Ghana, katika mchango wake kwenye ripoti hii. 

Ili kupata faida kamili ya AfCFTA, Bi. Lusigi anasisitiza kwamba wafanyabiashara wanawake lazima wapate habari na fursa za mafunzo kwenye mitandao ya biashara na kwamba sauti zao lazima zisikilizwe katika "majadiliano ya AfCFTA, utungaji wa sera na maamuzi."

Anaongeza kuwa kutumia utajiri wa rasilimali watu katika AfCFTA kunahitaji kutafakari mahitaji ya wanawake na vijana katika mifumo ya kisheria na kiufundi ambayo inaanzishwa.

"Kuwezesha uwekezaji mipakani, kulinda hakimiliki, kushirikiana kwenye forodha na ushuru, na kutekeleza uwezeshaji wa biashara" kutahakikisha "fursa sawa na endelevu, ambayo ni muhimu kwa ufanisi wa ukombozi unaoendelea wa huduma za biashara," Bi. Lusigi anasisitiza.

Bwana Luke anaongeza kuwa, "Soko huru barani linalotolewa na AfCFTA linatoa fursa kwa uzalishaji wa ndani wa bidhaa za dawa na vifaa vya huduma za afya kwa kiwango."

Anasikitishwa na athari kali za mabadiliko ya hali ya hewa kwa uchumi wa Afrika, kwa sasa na katika siku zijazo, akisema kwamba, kwa mfano, katika hali ya joto kali, Sudan na Tanzania zinaweza kupoteza karibu asilimia 18.6 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2050.

Isitoshe, anasisitiza kuwa mabadiliko ya ulimwengu kuelekea nishati safi yanaweza "kuiacha Afrika ikiwa imekwama na mali za mafuta za thamani iliyopungua... Katika kupunguza kiwango cha joto duniani hadi nyuzi 2 °C, kwa asilimia 26, asilimia 34 na asilimia 90 ya gesi, mafuta na akiba ya makaa ya mawe, kwa pamoja, ya Afrika yanaweza kuachwa bila kutumiwa. ”

Hata hivyo, hasara kutoka katika akiba ya mafuta ghafi inaweza kufidiwa kwa fursa zitakazopatikana katika mfumo wa kuongeza thamani katika madini ya kijani. 

Kwa mfano, Bwana Luke anaandika, "Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina asilimia 47 ya Cobalt duniani kote (inayohitajika katika kutengeneza betri) na Namibia na Zimbabwe zina asilimia 100 ya akiba ya Cesium duniani na asilimia 89 ya akiba ya Rubidium duniani (zote zinatumiwa katika mifumo ya uundaji wa simu ya rununu). 

"Kadhalika, vitu 42 kati ya 63 vinavyotumiwa na teknolojia ya kiwango cha chini cha kaboni na katika Mapinduzi ya Viwanda 4.0 hupatikana barani Afrika," ikidhihirisha kuwa bara hili linakalia hazina ya fursa za kijani.

"AfCFTA inaweza kuwa njia mojawapo nzuri ya kurejesha mtazamo, ikileta matumaini ya kujiimarisha katika suluhisho za nyumbani kwa kuongeza mauzo ya nje na, kwa kufanya hivyo, kutawawezesha washiriki wote katika biashara za kuvuka mipaka, haswa wanawake na vijana," anatoa maoni Bi. Eziakonwa,  katika utangulizi wake wa ripoti hii.

Mada: