Zana za ubunifu zinazosaidia wanawake wa ngazi ya chini kupata ardhi barani Afrika

Get monthly
e-newsletter

Zana za ubunifu zinazosaidia wanawake wa ngazi ya chini kupata ardhi barani Afrika

Vikundi vya wanawake, vyama vya ushirika, ushawishi na uhusishaji unasaidia kutatua masuala ya ardhi
Christabel Ligami
Afrika Upya: 
5 December 2021
Wanawake wa Kaunti ya Homabay
Shibuye Community Health Workers
Wanawake wa Grassroots kutoka Kaunti ya Homabay wakionyesha mazoea yao katika kuendeleza usalama wa chakula na biashara ya Kilimo.
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti ya Kiingereza

Wanawake wa ngazi ya chini barani Afrika wamebuni nyenzo za kuwasaidia kupigania haki zao za ardhi na kupata ardhi, kitu ambacho wamenyimwa kwa muda mrefu.

Zana hizi pia zinawasaidia wanawake katika ngazi ya kijamii kujenga mshikamano kati yao wenyewe ili kuwawezesha kujadiliana na serikali zao, kuimarisha uelewa na kupaza sauti zao kuhusu masuala yanayohusu ardhi, kama vile kutorithishwa, unyakuzi wa mali, kufurushwa kutoka kwa ardhi.

Katika kikao ambapo wanawake katika ngazi ya chini walijadiliana na mifumo ya kitamaduni kwa ajili ya usimamizi bora wa ardhi kwa haki na usawa katika ngazi ya mitaa wakati wa Kongamano la nne la Sera ya Ardhi (CLPA) mjini Kigali, Rwanda, mapema mwezi huu, vikundi mbalimbali vya wanawake viliwasilisha zana wanazotumia kupata ardhi na kuimarisha uelewa kuhusu haki zao za ardhi. Vikundi hivi ni sehemu ya Tume ya kimataifa ya Huairou - muungano wa kimataifa, unaoongozwa na wanawake ambao unaboresha uwezo wa mashirika ya wanawake katika ngazi za chini.

Kutokana na mawasilisho yao, ilikuwa wazi kuwa ufumbuzi wa ndani kwa masuala nyeti kama vile haki za ardhi unaweza kupatikana ikiwa mamlaka za ndani, wanawake, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yataungana pamoja. 

Kwa mfano, Bi Violet Shivutse, kiongozi wa Shibuye Community Grassroots alisema vikundi vya wanawake katika maeneo ya mashambani magharibi mwa Kenya vimejipanga katika vikundi vinavyoitwa Collective Women Farmers ambavyo wanavitumia kama nyenzo ya kupigania upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula.

"Wanawake wanapofanya kazi kibinafsi, inakuwa vigumu kupata maafisa wa kilimo nyanjani kwa sababu ya uhaba wa maafisa hawa. Hii ni changamoto katika nchi za Afrika Mashariki. Hata hivyo, chini ya kikundi cha pamoja, wakulima wanawake wanaweza kutambua kituo cha maonyesho na kupata afisa wa kilimo nyanjani kuwahudumia mara kwa mara,” alisema Bi. Shivutse.

"Kikundi cha wanawake na afisa wa kilimo nyanjani wanaunda mpango wa kazi na kutumia sehemu ya ardhi yao kama kituo cha mafunzo na maonyesho ambapo wakulima wengine wanawake wanafika kuona na kujifunza na kisha kuiga matendo kama hiyo," aliongeza.

Nyenzo nyingine wanaotumia wanawake ni uhusishaji ili kufikia na kupata ardhi. Uhusishaji hutumiwa kushughulikia masuala yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa, kufurushwa na changamoto za urithi.

Ili kutumia uhusishaji kama nyenzo Bi. Shivutse anasema wanawake kwanza wanafaa kuunde kundi kuu la viongozi na msemaji wa kuongoza mchakato, kisha kuwashirikisha wanachama wengine ili kuhakikisha kuwa jamii inaungana nao. Hatimaye watatambua kile wanachotaka kuhusisha. Wanatumia michoro, video, picha, na ushuhuda wa kibinafsi, wanaotumia kutambua changamoto kama vile kufurushwa kutoka kwa ardhi yao na kutorithishwa.

Katika hali hiyo wanatambua masuala mengine ambayo yanahusiana kwa njia isiyo ya moja kwa moja na umiliki wa ardhi na uafikiaji kama vile idadi ya watoto ambao hawaendi shuleni kutokana na kufurushwa, au uhaba wa chakula.

"Tunafanya hivi ili tusiingize siasa katika masuala ya ardhi na wanawake. Kwa sababu ardhi inahusu mamlaka, watu wanadhani kuwa wanawake wanatafuta mali tu,” alisema.

“Mchakato wa uhusishaji unafichua masuala mengine ambayo yanadhoofisha maendeleo. Unapounganisha masuala ya ardhi na elimu yanayothaminiwa na kila mtu katika jamii, basi kunakuwa na mshikamano hata kutoka kwa viongozi wa jamii. Unapohusisha ardhi na usalama wa chakula, kila mtu anaunga mkono suala hilo ili kuhakikisha kuwa hakuna njaa.

Bi. Shivutse alieleza kuwa uhusishaji umekuwa msingi wa jinsi wanawake wa ngazi ya chini wanaweza kushirikisha jamii nzima kwa masuala yanayohusiana na ardhi.

Ushawishi na mazungumzo ya jamii, hufanywa kwa pamoja na uhusishaji. Kutokana na matokeo ya uhusishaji, wanawake wanaweza kuwashirikisha viongozi wa jamii kwa ajili ya mipango ya kazi inayojumuisha kuwapa makazi watu waliofurushwa, jinsi ya kuwasiliana kuhusu kufurushwa, jinsi ya kuhakikisha kuwa usalama na malipo au faragha ya wanawake na watoto wao inazingatiwa wakati wa kufurushwa.

Ripoti za uhusishaji pia husaidia kushawishi mijadala ya sera na kuweka vipaumbele vinavyohusiana na masuala ya wanawake na ardhi.

Matumizi ya kielelezo cha aina ya umiliki wa kijamii kama nyenzo inayotekelezwa katika nchi kama Zambia na Uganda, Bi. Shivutse alisema, huzua uhusishaji. Kisha wanawake hushirikisha kila mtu katika jamii, wakijumuisha vijana, kuhusu mfumo wa jadi wa usimamizi wa ardhi, ikiwemo wakati hatimiliki za ardhi hazipo. Hili limechochea utoaji wa hatimiliki wa pamoja ambapo wanaume, wake na watoto wao wanatambuliwa kumiliki sehemu katika ardhi ya familia. Hili ni muhimu kwa sababu mtu anapofariki, mwenzake anabakia salama kwenye ardhi yao.

Kikundi cha wanawake pia kimekubali ukodishaji wa ardhi, na mtu binafsi au kikundi. Kupitia ukodishaji wa vikundi, wanachama wanapata eneo la kutosha la ardhi ili kuwa na sehemu za maonyesho ambavyo wanaweza kufanya kilimo bora. 

Hata hivyo, changamoto iliyopo ni kwamba masuala ya ukodishaji wa ardhi hayajaratibiwa katika baadhi ya nchi za Afrika. Ili kukabili changamoto hii, kikundi cha wanawake katika ngazi ya chini cha Shibuye mnamo mwaka 2017 kilitayarisha miongozo kuhusu ukodishaji ardhi ili kuhakikisha upatikanaji wa ardhi kwa wanawake, na kutayarisha masuala muhimu waliyopitia katika ukodishaji wa ardhi, ambayo yalitumika kama masharti ya marejeleo ya miongozo hii.

Aidha, waliteua wawakilishi wa jamii kuandaa miongozo. Hili lilichangia miongozo ya ukodishaji wa ardhi kupitishwa.

Madagaska

Lilia Ravoniarisoa, kiongozi wa Shirikisho la Wakulima Wanawake nchini Madagaska, alisema kuwa katika nchi yake, takriban theluthi moja ya wakazi wa vijijini hawana ardhi kwa sababu ardhi nyingi ni ya serikali au ya jamii. Aidha, kama asilimia 70 ya kazi za familia hufanywa na wanawake, lakini wanawake hawarithi ardhi kutokana na mila na viwango vya juu vya kutojua kusoma na kuandika ambavyo vinawazuia kupata ardhi.

Vikundi vya wanawake vya Bi. Ravoniarisoa vimehusisha ardhi katika kila eneo nchini - ikijumuisha ardhi ya jamii ambayo wanailinda kwa kupanda miti ya mikoko.

Kisha wanauza bidhaa za mikoko ili kuzalisha mapato. Mbao zinatumika kujenga nyumba za pwani, huku mizizi na majani yakitumika kutengeneza dawa.

"Zaidi ya hekta 90 zimepatikana kutoka kwa mamlaka za mitaa na tumeomba hekta 300 ili kupanda miti tena. Lengo ni kupunguza hatari kwa wanawake kwa kuongeza mapato yao na usalama wa chakula,” alisema Bi Ravoniarisoa.

“Vikundi vya wanawake vinatumia ardhi ya jamii iliyokodishwa kutoka kwa mamlaka kushughulikia uhaba wa chakula na ukosefu wa rasilimali kupitia kilimo. Ukodishaji ni wa muda mrefu lakini huhawilishwa kila mwaka. Hili limeongeza mapato kwa wanawake pamoja na kufanya maamuzi katika nyumba zao,” Bi Ravoniarisoa alisema.

Bi. Ravoniarisoa alieleza kuwa wanawake hao wanapanga kuunda vyama vya ushirika katika ngazi ya chini ili kuwawezesha kuwa na nguvu zaidi katika majadiliano ya masuala ya ardhi. Wanafanya hivyo kwa kuunganisha rasilimali ambazo huwawezesha kujadiliana kuhusu umiliki wa ardhi na matumizi kwa sauti moja.

Katika eneo la Kusini Magharibi, kundi hilo limeshawishi mamlaka za mitaa kuwapa sehemu ya ardhi ya jamii bila malipo yoyote kwa ajili ya upandaji miti.

Katika maeneo mengine wana ardhi ambapo wanawake wanapanda mwani na kufuga samaki na kaa.

"Tuna fursa ya soko kwa sababu tunazalisha bidhaa za kienyeji," alisema, akiongeza kuwa kupitia mijadala, wanawake wanawezeshwa na wanafahamu zaidi haki zao za ardhi.

Masimulizi mengine kama haya: