Kuangamiza dhuluma dhidi ya wanawake - Waamini wahasiriwa. Chukua hatua sasa!

Get monthly
e-newsletter

Kuangamiza dhuluma dhidi ya wanawake - Waamini wahasiriwa. Chukua hatua sasa!

Taarifa ya Goretti, Kenya
Afrika Upya: 
30 Novemba 2021
UN Women/Luke Horswell
Goretti Ondola (kulia) azungumza na Caren Omanga wa Kituo cha Haki za Kijamii cha Nyando.

Karibu 1 kati ya wanawake 3 ameshuhudia dhuluma, kimataifa. Idadi hiyo yaweza kuwa hata juu zaidi nyakati za hatari. Dhuluma za kijinsia ndio ukiukaji mkuu wa haki za kibinadamu ulioenea zaidi, hata hivyo, sio wa asilia wala usioweza kutokea. Unaweza na ni sharti uzuiliwe.

Kuikomesha dhuluma hii kunaanza kwa kuwaamini wahasiriwa na kuchukua hatua, kila siku. kupitia misururu hii ya tahariri maalumu kwa Siku 16 za Uanaharakati, UN Women inaonyesha sauti za wahasiriwa, za mipango ya mageuzi yanayoleta athari halisi.

“Mwaka wa 2001, nilirejea [Magharibi mwa Kenya] kumzika mume wangu. Katika utamaduni wa huko, mume anaopfariki, mjane wake anastahili kusalia katika boma la familia,” anaeleza Goretti Ondola.

“Kama mmoja katika jamaa, unatarajiwa kuishi na mamamkwe iwapo huna ardhi yako. Hata hivyo, hawakunipa chakula. Kila kitu nilichotoka nacho Nairobi [jiji kuu] – nguo, vyombo vya nyumbani – kilichukuliwa na kugawiwa jamaa.”

Mahari – malipo ya fedha au mifugo kwa jamaa za mke kutoka kwa mume – bado ni maarufu nchini Kenya. Mahari iliyolipwa kwa familia ya Bi. Ondola ilimnasa katika maisha ya dhuluma kwa karibu miaka 20 baada ya kifo cha mumewe. Mwishoni mwa 2020, walimpiga vibaya sana mpaka akalazwa hospitalini na akashindwa kufanya kazi.

Katika maeneo ya mashambani nchini Kenya, mara nyingi watu husita kutoa ripoti kwa askari. Bi. Ondola alimwendea mtetezi wa haki za kibinadamu wa karibu badala yake.

“Mtetezi huyo wa haki za kibinadamu alinisaidia kuenda katika kituo cha afya na kutoa ripoti kwa kituo cha polisi cha karibu. Nilipowasilisha kesi askari walisema kwamba hawana gari la kwenda kuwatia mbaroni wahalifu hao. Aidha nilifahamu kwamba wahalifu hao walikuwa wamewasiliana na askari tayari. Hata [walighushi] makubaliano wakitumia jina langu kuiondoa kesi … lakini hata singeweza kuandika,” akumbuka Bi. Ondola.

Aghalabu watetezi wa haki za kibinadamu nchini Kenya ndio huitikia mwanzo ukiukaji wa haki za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na dhuluma za kijinsia. Tangu 2019, UN Women na Ofisi ya UN ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu (UN Human Rights) imekuwa ikisaidia kutoa mafunzo ya kisheria na uwezeshaji wa waratibu wa nyanjani ili waweze kuwasaidia wahasiriwa vyema.

Mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Italia, unakusudia kuongeza uwezo wa wahasiriwa kupata haki na kuwezesha uchaguzi wa amani mwaka 2022.

Caren Omanga ni mmoja kati ya watetezi wa haki za kibinadamu aliyepokea mafunzo haya. Yeye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Haki za Kijamii cha Nyando, kilicho takribani km 30 mashariki mwa Kisumu, jiji la tatu kwa ukubwa nchini Kenya.  

Alimsaidia Bi. Ondola na akatoa taarifa ya suala hilo kwa komanda wa kituo cha polisi cha karibu na kortini. Huku akifahamu kwamba mara nyingi mizozo ya kijamii hutatuliwa nje ya mikondo ya kisheria ya serikali, pia alishirikiana na wazee wa eneo husika.  

Jinsi unavyoweza kuchukua hatua
  • Wasikilize wahasiriwa, waelekeze kwa huduma faafu za msaada, na kuza habari zao kwa kutumia #OrangeTheWorld (amplify their stories using #OrangeTheWorld)
  • Yafadhili mashirika ya haki za wanawake. Anza kwa kuchukua changamoto ya #Give25forUNTF25 challenge
  • Ongea. Wape wanairimu wenzako changamoto ya kuwazia mienendo yao, yashutumu maoni ya kiubabedume na ongea mtu anapovuka mpaka.

“Nilikuwa karibu kutiwa mbaroni wakati nilipomkabili afisa husika,” aeleza Bi. Omanga. “Lakini nilijua kwamba jamii ingemhasimu, kwa hivyo, nilianza mchakato mbadala wa kutatua mizozo, huku nikiisukuma kesi mahakamani. Kulikuwa na hali nyingi zisizo za kawaida kuhusiana na namna kesi hiyo ilivyoshughulikiwa, kwa hivyo nilihakikisha haya yamewekwa bayana kwa hakimu na waendesha mashtaka.”

Hatimaye kesi hiyo ilitatuliwa nje ya mahakama kuku kukiwa na makubaliano yaliyompa Bi. Ondola ardhi yake na hatimiliki, na wahalifu walihitajika kulipa faini ili kuepuka vifungo gerezani.

“Ni kama kuyaanza maisha baada ya miaka 20. Mwanangu wa kiume anajihisi salama zaidi … ninawazia kuipanda miti kadhaa ili kuilinda ardhi hii na kujenga chumba cha kufuga kuku. Ninahitaji jikoni nyumbani kwetu ili kuayafanya maisha yawe mazuri kidogo,” asema Bi. Ondola.

Kuzuia dhuluma dhidi ya wanawake nchini Kenya

Kenya hushuhudia ongezeko la visa vya dhuluma za kimapenzi na za kijinsia nyakati za uchaguzi. Misukosuko huongezeka, na wanawake ndio wanaostahimili dhuluma hizo. 

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (The Kenya National Commission on Human Rights) iliripoti visa 201 vya dhuluma za kimapenzi (201 sexual violence cases) katika uchaguzi wa 2017, kati ya Agosti na Disemba. Ni asilimia 22 pekee ya visa hivi vilivyoripotiwa kwa polisi, na asilimia 54 ya uhalifu ulioripotiwa ulitekelezwa na maafisa wa usalama na askari.

Tangu 2019, kwa usaidizi wa serikali ya Italia, mashirika ya UN Women Kenya na UN Human Rights yamekuwa yakifanya shughuli zao Magharibi mwa Kenya na Nairobi kuhusu uzuiaji na njia za uwajibikiaji ili kupunguza dhuluma dhidi ya wanawake nyakati za uchaguzi.

Uimarishaji wa uwezo wa watetezi wa haki za kibinadamu, ambao ni watu wa kujitolea katika jamii kuwasaidia wahasiriwa, ni moja kati ya mikakati mikuu ya mradi huo.

Wangechi Kahuria, ambaye ni afisa wa UN Women nchini Kenya, anaeleza kwamba “moja kati ya viuongo muhimu vya mradi huo ni kuiwezesha jamii katika kuwajibikia dhuluma za kimapenzi na za kijinsia.

“Aghalabu wao ndio wanaoitikia mwanzo na wanastahili kujihami ili kukabiliana na visa hivyo. Hili lina maana ya kuwapa mafunzo ya kuwawajibikia wahasiriwa, kuelewa mikondo iliyopo ya kuwaelekeza kwa mkabala wa kisheria, lakini pia kuhakikisha kwamba watetezi wa haki za kibinadamu wana msaada wanaohitaji, ili kuepusha uchovu mwingi,” anasema.

Mradi huo umewapa mafunzo watetezi wa haki za kibinadamu zaidi ya 38 katika eneo la Magharibi mwa Kenya na katika jiji kuu Nairobi. Wahasiriwa 555 wamepokea msaada wa kisheria na ushauri wa kisaikolojia na kijamii katika mwaka wa 2020. 

Mradi huo unashirikiana na maafisa wakuu wa askari nchini ili kuimarisha njia za kutoa taarifa kwa ndani na kuwezesha mageuzi chanya katika sekta ya haki.

Mwongozo wa haki kuhusu jinai umetengenezwa, unaowaongoza askari, maafisa wa msaada wa kiafya na wa kisheria katika usimamizi wa kesi za dhuluma za kijinsia.