Pata programu za rununu za bure

Pata habari mpya kutoka kwetu kwenye programu zetu.

Download app from Android Download app from Apple

Kung'ang'ania chanjo ya COVID-19: Afrika lazima sasa iamke

Get monthly
e-newsletter

Kung'ang'ania chanjo ya COVID-19: Afrika lazima sasa iamke

Waafrika lazima wahusike katika majaribio ya chanjo, na wajitayarishe kuwa katika mstari wa kwanza ianzapo kutumika
Afrika Upya: 
28 August 2020
COVID-19 Dashboard by the Center for Systems Science and Engineering (CSSE)
Jernej Furman
Dashibodi ya COVID-19 na Kituo cha Sayansi na Uhandisi wa Mifumo (CSSE) katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins (JHU) kufikia tarehe 28 Agosti 2020.

Katika ulimwengu halisi, jamii hazifai kuwa watazamaji tu bali wadau wakuu katika maamuzi ya afya yanayoathiri ustawi wao. Wasiwasi kuhusu majaribio ya chanjo unafaa kushughulikiwa, na watafiti wanapaswa kuweka kipaumbele katika ushirikishwaji wa jamii.

Je, majaribio ya chanjo yanamaanisha nini kwa jamii? Ni kwa nini wahangaike? Serikali za Afrika lazima zifanye nini, haswa?

Tunaposubiri kwa hamu kudhibitiwa kwa COVID-19, tuanze kwa kuelewa kinga ya umma na pia umuhimu wa chanjo. Kwa usemi rahisi, kinga ya umma ni wakati ambapo idadi kubwa ya watu katika jamii wameambukizwa na kwa hivyo wana kinga dhidi ya ugonjwa, katika hali hii, COVID-19.

Kulingana na makadirio, kinga ya umma ya COVID-19 itafikiwa wakati watu zaidi ya 60% wataambukizwa. Idadi hiyo ni Waafrika milioni 780! Mnano 23 Agosti, 2020, takriban miezi mitano tangu kisa cha kwanza kuripotiwa barani, Afrika ina visa milioni 1.18, vifo 27,610 watu 900,584 waliopona. Bado tuko mbali sana kufikia kinga ya umma! Kwa hiyo, haiwezekani kufikia kinga ya umma kwa njia ya asilia.

Hata hivyo, tunaweza kuwapa watu kinga kupitia chanjo na kuharakisha kufikia kinga ya umma. Ni wazi basi kuwa hitaji la chanjo bora na salama ni la dharura. Hii ndiyo sababu chanjo ya COVID-19 inasalia kuwa tumaini letu la pekee la kudhibiti janga hili.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kufikia tarehe 25 Agosti kulikuwa na zaidi ya aina 170 za chanjo za COVID-19 zilizokuwa zinajaribiwa. Takriban 138 ziko katika hatua ya awali ya majaribio (bado hazijafikia majaribio kwa binadamu), huku 27 zikiwa katika hatua ya kwanza (majaribio salama kwa watu wachache), 17 ziko katika hatua ya pili (majaribio salama kwa watu wengi), 7 ziko katika hatua ya tatu (majaribio ya ufanisi wao kwa watu wengi) na hakuna ambayo tayari imeidhinishwa kwa matumizi ya jumla.

Prof Joachim Osur
Prof Joachim Osur

Kwa kawaida, chanjo huhitaji miaka mingi kuundwa na kujaribiwa na huhitaji hata muda zaidi kuzizalisha. Hata hivyo, watafiti wako mbioni kuunda chanjo ya COVID-19 katika muda wa miezi 12 hadi 18. Afrika Kusini ndiyo nchi ya pekee barani Afrika inayoshiriki katika majaribio ya chanjo.

Uundaji wa chanjo huanza kwa uchunguzi wa kimsingi katika maabara juu ya virusi na maingiliano yake na seli za mwili. Matokeo yake husaidia uchunguzi wa awali ambapo chanjo inajaribiwa kwa wanyama na usalama wake kurekodiwa. Mmenyuko wa seli za mwili wa mnyama huandikwa chini na husaidia katika hatua nne za majaribio kwa binadamu.

Hatua nne za majaribio ya chanjo

Katika hatua ya kwanza ya majaribio, usalama wa chanjo na uwezo wake wa kuchochea mwili wa binadamu kuzalisha kinga hubainishwa. Kipimo, njia bora ya kutoa chanjo na uwezo kamili hubainishwa.

Hatua ya pili ya majaribio ya chanjo inahusisha idadi kubwa ya watu, kubainisha matokeo, ikiwemo uwezo wa mwili wa mtu kuunda kinga dhidi ya COVID-19 pamoja na madhara yoyote ya chanjo.

Hatua ya tatu ya majaribio inathibitisha tena ufanisi na usalama wa muda mrefu wa chanjo na inahusisha kutoa chanjo hiyo kwa idadi kubwa ya watu, na kuwachunguza kwa kipindi cha muda mrefu. Chanjo inapopita hatua ya tatu ya majaribio, inapatiwa leseni ya uzalishaji wa kibiashara na matumizi ya umma.

Majaribio ya hatua ya mwisho, hatua ya nne yanahusisha ufuatilizi wa karibu chanjo inapotolewa kwa jamii.

Lolem B. Ngong
Lolem B. Ngong

Majaribio haya yanaweza kusitishwa katika hatua yoyote, kuanzishwa tena, kurekebishwa, nk kutegemea kinachotokea. Ili kuchunguza vizuri mmenyuko cha chanjo kwa mwili wa binadamu, pande zote za ulimwengu lazima zihusike katika majaribio. Chanjo lazima zijaribiwe katika mazingira tofauti na kwa watu wenye maumbile tofauti. Kwa hivyo, Waafrika lazima washiriki katika majaribio ya chanjo.

Jinsi Afrika inavyoweza kujitayarisha kwa chanjo ya COVID-19

Afrika sio lazima ihusike tu katika majaribio ya chanjo, nchi za Afrika lazima zijitayarishe sasa kwa siku ya kwanza ya kuwepo kwa chanjo. Matayarisho yatahakikisha kwamba chanjo inatoka kwa eneo la uzalishaji na kutua katika uwanja wa ndege huko Lagos, Addis Ababa, au Ndjamena nk, na mwishowe kufika katika kituo cha afya huko Maridi, Kumbo na Khayelitsha.

Kujitayarisha kwa chanjo ya COVID-19 kunahitaji nchi: (i) kuamua vigezo vya kustahiki - ni nani atakayepatiwa kipaumbele na kwa nini; kwa kukumbuka kuwa ratiba nyingi za chanjo kwa sasa zinalenga watoto; (ii) kuunda mkakati madhubuti wa usambazaji wa chanjo; (iii) kutambua sehemu ambayo chanjo hiyo itatolewa na atakayeitoa (madaktari, wauguzi, n.k); (iv) kuunda njia madhubuti za ununuzi, usambazaji na mpango wa usambazaji huo; na mwishowe (v) kuwa na mpango endelevu wa kuhakikisha upatikanaji na ufikiaji wa chanjo ya COVID-19.

Kwa hivyo, serikali za Afrika lazima:

Ziunganishe na kupaza sauti za AfrikaUtaifa wa chanjo unazidi kuimarika. Nchi zinazounda chanjo zinaweka kipaumbele kwa raia wao na huenda zikashikilia chanjo. Kwa bahati mbaya, kwa magonjwa ambukizi, hakuna aliye salama hadi sote tuwe salama.

Wakati uo huo, Afrika lazima indeleze juhudi zake za pamoja ili kukabiliana na janga hili kwa pamoja – ikiwa ni pamoja na kuunda, kuzalisha na kusambaza chanjo ya COVID-19. Ndani ya mfumo wa Umoja wa Afrika wa Muungano wa Majaribio ya Chanjo ya COVID-19 na kuweka pamoja jukwaa la ununuzi, mataifa wanachama yanafaa kutetea makubaliano bora ya upatikanaji wa chanjo. Kuunga mkono msaada wa kifedha na kiufundi kwa nchi kama vile Afrika Kusini, Kenya na Senegali miongoni mwa nyingine kwa kuwa uzalishaji wa ndani wa chanjo utakuwa faida kubwa.

Dr George Kimathi is an accomplished health development specialist with over 20 years’ experience in design and implementation of integrated public health programmes.
Dr George Kimathi

Kusawazisha na kutaasisisha utayari wa nchi-Mbali na juhudi za kiwango cha bara, hatua zinazofaa za kujitayarisha kwa chanjo ya COVID-19 ni muhimu sana. Hii inajumuisha kuanzisha miundo ya sekta nyingi kuwezesha mikakati ya uzalishaji na usambazaji, kujenga uwezo wa wafanyakazi wa huduma ya afya kutoa na kufuatilia usalama wa chanjo, kuandika na kuhifadhi matokeo ya chanjo, na kutafuta rasilimali za ndani na nje kuwezesha uzalishaji wa haraka na usambazaji wa chanjo.

Kuunda mikakati kuhamasisha jamii – watafiti ulimwenguni wanaharakisha uundaji wa chanjo. Kikwazo kitakachofuata, ila kishughulikiwe sasa, kitakuwa watu kusita kupata chanjo, woga usio na msingi kama mtu akipatiwa chanjo. Jamii lazima ziwe katika mstari wa mbele wa majaribio ya chanjo ya COVID-19 na juhudi zinazolenga matumizi kamili.

Jamii zinapaswa kuchukua jukumu muhimu katika kutambua na kufikia watu walioko hatarini wakati wa kampeni za chanjo. Huu ni wakati wa kushirikisha jamii kupitia walinzi wa jamii, wakiwemo Wahudumu wa Afya katika Jamii, viongozi wa kidini na kitamaduni, ili kuondoa woga wa chanjo.

Uhamasishaji bora wa jamii utasababisha ushiriki mzuri katika majaribio ya chanjo na hivyo kukubali chanjo ya COVID-19.

Kumekuwa na utetezi mwingi unaolenga ufadhili, upatikanaji na uwepo wa chanjo. Kwa bahati mbaya, Afrika imekuwa mtazamaji katika majaribio ya chanjo ya COVID-19. ‘Kung'ang'ana’ huku kunakoendelea kwa chanjo ambayo bado haijaidhinishwa kumeibua wasiwasi ambao utanyima watu walioko hatarini katika nchi zenye mapato ya chini na ya kati bidhaa hii ya kuokoa maisha.

Serikali za Afrika lazima ziendelee kufanya kazi kwa umoja na kuwa na msimamo wa kimkakati wa bara letu ili kuhakikisha upatikanaji wa chanjo ikipata kuidhinishwa. Hii inahitaji hatua za dharura za bara na nchi, na kuweka jamii katika nafasi ya kati ili chanjo hii dhidi ya COVID-19 ikubalike ifaavyo. 


* Amref Health Africa ni shirika lisilo la kiserikali lililo na Makao yake makuu jijini Nairobi. Shirika la Amref lililoanzishwa mnamo 1957, linasaidia jamii katika nchi 35 za Afrika kujenga mifumo ya afya yenye uhimilivu.

Prof Joachim Osur ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Mipango katika Shirika la Amref Health Africa, na pia Profesa Msaidizi wa Afya ya Kijinsia na Uzazi na Mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amref. Yeye ni mtaalamu wa afya ya umma, afya ya uzazi, na mtaalamu wa dawa ya ngono aliye na tajriba pevu katika programu ya afya katika muktadha wa Afrika.

Dkt George Kimathi ni mtaalamu wa maendeleo ya afya aliye na tajriba ya zaidi ya miaka 20 katika kuunda na kutekeleza mipango jumuishi ya afya ya umma. Yeye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Ujenzi wa Uwezo ya Amref Health Africa(ICD), akitoa uongozi wa jumla katika Ajenda ya Rasilimali Watu wa Afya (HRH) ya shirika hili.

Lolem B. Ngong ni mtaalamu kiulimwengu wa Afya ya Umma, aliye na zaidi ya miaka 15 ya uongozi katika diplomasia ya afya ya ulimwengu na uratibu wa ushirikiano wa kimkakati kushughulikia vitisho kwa afya ya umma. Bi Ngong ni Mtaalamu wa magonjwa na Mkuu wa Wafanyakazi katika shirika la Amref Health Africa.

More from this author