Tunapoadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, ni lazima tushirikiane kufanikisha nafasi zilizomo katika umoja wa Afrika

Get monthly
e-newsletter

Tunapoadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, ni lazima tushirikiane kufanikisha nafasi zilizomo katika umoja wa Afrika

— Bi. Fatima Kyari Mohammed Mchunguzi wa Kudumu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa.
Africa Renewal
Afrika Upya: 
29 September 2020
Fatima Kyari Mohammed
UN Photo/Manuel Elias
Fatima Kyari Mohammed, Permanent Observer of the African Union to the United Nations, briefs the Security Council meeting on peace and security in Africa, with a focus on countering terrorism and extremism in Africa.

Bi. Fatima Kyari Mohammed Mchunguzi wa Kudumu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa. Alizungumza na AfrikaUpya kuhusu athari ya janga la COVID-19, kuadhimisha mwaka muhimu katika kupigania haki za wanawake na kutafakari kuhusu uhusiano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika mwaka wake wa 75. Hapa kuna madondoo:

. Fatima Kyari Mohammed
Bi. Fatima Kyari Mohammed Mchunguzi wa Kudumu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa.

Je, COVID-19 inaathiri vipi vipaumbele vya Afrika kama Malengo ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Afrika ya 2063?

Kama unavyofahamu, Ajenda ya 2030 na ya 2063 zinafungamana sana. Maeneo ya kipaumbele kama kuangamiza umaskini na njaa, kutimiza utoshelevu wa chakula na kushughulikia baadhi ya changamoto pana za kijamii na kiuchumi katika afya, elimu na ajira, haswa kwa wale walio katika hatari mno, yameathiriwa sana kwa njia ambazo hazikuwa zimetabiriwa hata mwaka mmoja uiopita. Janga hili limetulazimisha kuweka upya makini yetu katika maeneo tofauti na kuzigawa upya raslimali. COVID-19 imetuonyesha namna ulimwengu ulivyounganika. Hakuna mtu, taifa au kanda isiyoweza kuathiriwa na uhalisia huu.

Imeathiri vipi kazi yako?

Kama kila mtu, tumelazimika kupanga upya ili kuhakikisha kuwa tunaweza kutimiza wajibu na majukumu yetu. Tulibadilisha baadhi ya vipaumbele. Ilikuwa muhimu kulielewa janga hili pamoja na athari zake na kujaribu kuvishinda vizingiti vinavyoandamana nalo. 

Uwajibikiaji janga hili Afrika kote ulipunguza usambaaji wake mapema mwaka huu. Je, kwa namna gani mataifa yanaweza kuikabili changamoto hii vyema?

Heri ya Afrika dhidi ya janga hili ni mara mbili. Kwanza, huku yakipata mafunzo kutokana na mkurupuko wa Ebola, mataifa mengi ya Afrika yaliweka upesi hatua za kuukabili usambaaji wa COVID-19 mapema. Pili, kuhusu wakati, janga hili lilianza kuliathiri bara hili wakati maeneo mengine yalikuwa yakiathirika vibaya na janga hili. Kwa hivyo tulikuwa na wakati wa kutosha kujifunza kutokana na tajriba za wengine.

Huku tukisonga mbele, kupitia kwa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Afrika, Umoja wa Afrika (UA) unazisaidia asasi za matibabu za umma katika bara zima kupitia kwa ubunifu na ushirikiano wa kimkakati.

Tunashirikisha na kutoa masuluhisho jumuishi kwa upungufu katika mifumo yetu ya afya ya umma kama ukosefu wa miundomsingi ya kutosha, mafunzo na vifaa ili mataifa yajiandae vyema kushughulikia dharura na majanga ya afya katika siku za usoni.

Afrika yaweza kujikomboa vyema vipi kutoka katika janga hili?

Pigo kuu kwa mataifa mengi ya Afrika ni kwamba hatua kubwa za maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi zimekwazwa. Athari yake kwa maendeleo ya kiuchumi ni mbaya mno. Zaidi ya athari zake kwa afya na elimu, mfadhaiko wa kiuchumi kwa watu unatia wasiwasi mkubwa.

Mataifa yanastahili kuitumia tajriba hii kujijenga upya vyema na kwa njia thabiti. Athari yake kwa ajira, biashara na mapato ya familia ina maana kwamba hatua na mikakati tunayoweka inastahili kulenga mbinu na njia za kuwasaidia wale walioathiriwa zaidi na janga hili. Tunahitaji uwekezaji stadi na sera zinazoweza kumaliza lindi la umaskini na kutoa nafasi kwa watu wote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anahimiza haja ya kupunguza tafauti za kiuchumi katika kipindi cha maaendeleo ya baada-COVID-19. Je, Umoja wa Afrika, pamoja na ofisi yako, unawezaje kusaidia kutimiza ruwaza ya Katibu Mkuu kwa manufaa ya bara hili?  

Tunaupa kipaumbele ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Mwenyekiti wa Muungano wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, anauunga mkono kwa dhati wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuwa na hatua za pamoja dhidi ya janga hili na kutuliza hali kimataifa. Tunaweza kufaulu katika kulikabili janga hili ikiwa tutashirikiana. Ujumbe wa Utazamaji wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa utaendelea kuisaidia ruwaza na mambo yanayopewa kipaumbele na asasi zote mbili.  

Chunguzi mbalimbali zinaonyesha kwamba wanawake ndio walioathiriwa zaidi na janga hili la COVID-19. Je, wajibu wa wanawake ni upi katika kujiimarisha upya?

Ni kweli kwamba hata kabla ya janga hili kujitokeza, tulipigania haja ya wanawake kushirikishwa kikamilifu katika kufanya maamuzi. Chumi ni thabiti na michakato ya amani ni fanifu zaidi  wanawake wakishirikishwa kikamilifu. Wanawake wanaweza kupata ufanisi, kuanzia katika viwango vya chini vya kijamii hadi juu. Nitawahimiza wanawake waendelee kuzungumza dhidi ya dhuluma na kwa manufaa ya kila mmoja wao. Janga hili limeongeza visa vya dhuluma za kijinsia, ambavyo havistahili kuvumiliwa. Iwapo kwa hakika tunataka kufanya mabadiliko, sisi wanaume kwa wanawake, ni lazima tuendelee kupigana dhidi, kuelimisha na kuwaweka wazi watu wanaoendeleza dhuluma za kijinsia.

2020 ni mwaka muhimu kwa wanawake—na Beijng+25, Azimio 1325+20 la UNSC, na miaka 15 tangu Mwafaka wa Maputo ulipoanza kutekelezwa—yote yanayokabili mitazamo potofu kuhusu wajibu wa wanawake katika jamii. Mataifa ya Afrika yamepiga hatua kiasi gani katika kutimiza usawa wa kijinsia?

Hatua zilizopigwa na Bara Afrika tangu Kongamano la 4 la Beijing kuhusu Wanawake mwaka wa 1995 zinapongezwa, lakini bado tuna mengi ya kutimiza. Tuna sera za kimataifa na za kibara thabiti na endelevu, mikakati na mipango tekelezi kuhusu wanawake, amani na usalama. Ilhali wanawake na wasichana wanaendelea kuathiriwa zaidi na mizozo katika bara Afrika. Wao ndio wahasiriwa wa vurugu za kimapenzi na dhuluma nyinginezo na hawawakilishwi kikamilifu katika michakato ya kuleta amani katika viwango vya kijamii, kitaifa na kibara. Mkakati wa Umoja wa Afrika kuhusu usawa wa kijinsia unafungamana na Azimio 1325 la UNSC kuhusu ajenda ya wanawake, amani na usalama.  

Hata hivyo, utekelezwaji ungali changamoto, ikiwa ni pamoja na ushiriki kikamilifu wa wanawake katika harakati za amani na usalama. Hatua hii muhimu inastahili kutia nguvu mpya haja ya sauti ya wanawake kusikilizwa kataka ajenda ya amani na usalama. Hapana shaka kwamba ushirikiano wa Umoja wa Afrika na mashirika ya wanawake katika bara hili ndio njia ya kutimiza hatua muhimu. 

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilikubali juzi Mwafaka wa Kibara kuhusu Vijana, Amani na Usalama. Je, unawazia vipi wajibu wa vijana katika kutimiza amani na usalama katika Afrika?

Licha ya kukubaliwa kwa mwafaka ambao unarejelea, bado tuko katika hatua za mwanzo kabisa ya safari hii. Vijana wa sasa — idadi kubwa zaidi ya kizazi cha vijana katika historia —wametengwa, wamebaguliwa, wamenyonywa na kuingizwa katika mizozo kwa njia rahisi. Vijana wengi, haswa wanawake wachanga, hawana raslimali na fursa za kutimiza uwezo wao na kushiriki katika michakato ya kisiasa, amani na usalama. Badala yake, wamo hatarini, haswa wakati wa mizozo.  

Mwafaka wenyewe unahimiza haja ya kuchukuliwa hatua kuhusu vijana, amani na usalama barani Afrika. Kukubaliwa kwake ni utambuzi kwamba vijana ndio raslimali kuu zaidi ya Afrika. Unasaidia kupanua uwezekano wa vijana kushiriki kikamilifu katika michakato ya kuyafanya maamuzi pamoja na kupanga na kuratibu.

Umoja wa Mataifa unaisaidia kampeni ya Umoja wa Afrika kuhusu ‘Kuzinyamazisha Bunduki Barani Afrika kufikia 2020.’ Hili lina umuhimu gani kwa Afrika wakati bunduki zikinyamaza, na ofisi yako inashirikianaje na jamii ya kimataifa kulitimiza lengo hili?

Wacha niliweke swali hili katika muktadha wake: mpango wa Kuzinyamazisha Bunduki (STGs) barani Afrika uliahidiwa na viongozi wa Afrika mwezi Mei 2013 kumaliza vita vyote katika bara Afrika kufikia mwaka 2020. Kama unavyojua, STGs ni kipengele muhimu mno kwa Ajenda 2063 ya Afrika, na Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika baadaye lilikubali Mpango Mkuu wa Hatua Tekelezi kuzinyamazisha bunduki kufikia mwaka wa 2020. Mpango huo unasisitiza usaidizi wa kimuundo katika maeneo kama vile maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi, uwezeshaji wa vijana na wanawake, ajira, elimu, mabadiliko ya tabianchi na utawala.  

Tunafanya kazi na washirika wetu kubadilisha mwelekeo na kuhakikisha amani endelevu katika bara hili. Ila bado tuna mengi ya kufanya katika kusonga mbele na jamii ya ulimwengu. Kuzinyamazisha bunduki barani Afrika kuna maana ya kuwa na uwezo wa kuendelea na kusonga mbele na kulijenga bara lenye amani na lenye ustawi kwa manufaa ya watu wetu.

Huku Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75, je, ni kwa namna gani shirika hili limekuwa muhimu kwa amani, usalama na maendeleo ya Afrika?  

Ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika amani na usalama ni muhimu mno. Mashirika haya mawili yanashirikiana katika maeneo mengi. Tuna mashauriano ya kila  mwaka, jopokazi la pamoja, tunayazuru maeneo ya nyanjani na kufanya juhudi za upatanishi pamoja. Tunashirikiana pia katika masuala ya uchaguzi na utawala, ulinzi wa haki za kibinadamu miongoni mwa mambo mengine.   

Afrika inaendelea kupigania uwakilishi zaidi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC). Ni ipi sababu yake kuu ya kupigania huko?

Kama unavyofahamu, Afrika ina msimamo mmoja kuhusu mageuzi ya UNSC. Afrika imekuwa ikipigania uwakilishi katika kategoria ya “Kudumu” ya Baraza hilo kwa msimamo mmoja. Aidha, kuna haja ya uwakilishi zaidi wa Afrika katika kategoria “isiyo ya Kudumu” ili kutimiza mageuzi ya kweli na muhimu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Uwakilishi sawa kijiografia kulingana na kanuni, malengo na maadili ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaweza tu kuelekeza kwa ulimwengu wenye haki na usawa zaidi. 

Wakati wowote ule, kuna mataifa mtatu ya Afrika yanayoshikilia viti vya uwakilishi usio-wa-kudumu, katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, maarufu kama A3. Je, unaweza kusema ni mambo gani matatu makuu ambayo A3 imetimiza hivi karibuni katika kuendeleza ajenda ya Afrika?

Kwanza, kumekuwa na ushirikiano thabiti kati ya wanachama hao, haswa miaka miwili iliyopita. Hili limesaidia kupigia debe misimamo inayofanana ya Afrika, maslahi na wasiwasi kuhusu masuala ya amani na usalama yaliyo katika ajenda ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  

Pili, sasa tumeanzisha mikutano ya kila mwaka kati ya AUPSC [Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika] na UNSC. Hili linadhihirisha kujitolea kati ya mabaraza haya mawili kushirikiana katika masuala kuhusu amani na usalama katika Afrika. A3 yanahakikisha kuna mashauriano ya kufana

Tatu, A3 imesaidia kubuni fursa za miungano na mataifa mengine wanachama wa UNSC, na kuhakikisha kwamba yanasaidia azimio letu la kuwa na amani ulimwenguni.

Soko Huru la Bara Afrika (AfCFTA) linazingatiwa kuwa muhimu mno kwa bara Afrika. Ni kwa nini Waafrika wawe na matumaini?

Lengo la AfCFTA ni kutumia fursa ya idadi kubwa ya watu ya takribani bilioni 1.3 na mapato yaliyojumishwa ya kitaifa $ trilioni 3.4 kwa kuunda soko moja la bidhaa na huduma, kuwezesha usafirishaji huru wa bidhaa na watu, kuongeza kasi ya uwekezaji na hatimaye kuwa na uwezekano wa kuunda Shirika Moja la Forodha.  

AfCFTA linaweza kuwainua watu milioni 30 kutoka katika lindi la umaskini kufikia mwaka wa 2035. Kwa hivyo, ni kwa nini Waafrika wasiwe na matumaini? AfCFTA ndilo tumaini letu kuhusu haja ya kupiga hatua na kupata maendeleo pamoja. Bila shaka, kuna sera na hatua za kiudhibiti zinazostahili kubuniwa, lakini baadhi ya hatua hizi tayari zinabuniwa katika mataifa na katika kanda ndogondogo.

Ni ujumbe upi wa matuaini unaowapa Waafrika katika kipindi hiki kigumu?

Tunapoadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, tunastahili kuwazia janga la COVID-19 na kufanya kazi pamoja kulikabili na kushirikiana kufanya uimarishaji endelevu. Kama nilivyosema hapo awali, janga hili limedhihirisha mianya mingi, lakini pia limeimarisha uhalisi kwamba tunaishi katika ulimwengu uliounganika. Kama Waafrika, ni sharti tuutambue uwezo na nafasi katika umoja wa Afrika na tushirikiane.   

Sisi sote ni sehemu ya ubinadamu. Hatuwezi kuupuuza ukweli kwamba ulimwengu unaumia. Hatua za pamoja, kuheshimiana, na kuzingatia sheria na desturi za kimataifa ni muhimu ikiwa tunataka kutimiza malengo yetu yanayofanana. Kwa ufupi, ushirikiano wa kimataifa ni muhimu.